Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Zahera awapa msala mastaa Yanga

KIKOSI cha Yanga kimeingia kambini kujiandaa na mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Azam FC, huku Mkurugenzi wa Ufundi wa Yanga kwa soka la vijana, Mwinyi Zahera akiwaachia msala mastaa wa timu hiyo.

Zahera aliyewahi kuwa kocha mkuu wa Yanga misimu miwili iliyopita, alisema nyota wa Yanga wakiongozwa na nahodha Bakari Mwamnyeto, Yannick Bangala, kipa Diarra Djigui na wengine kikosini kama watakaza mechi mbili zijazo za ligi haoni kitu cha kuizuia msimu huu kubeba ubingwa.

Kauli ya Zahera ilifanana na ile aliyoitoa kiungo wa zamani wa Simba na Taifa Stars, Mtemi Ramadhani ambaye naye alisema kwa kikosi kilichopo Jangwani msimu huu haoni cha kuwazuia kubeba ndoo.

Tuanze na Zahera. Kocha huyo Mkongoman alisema wachezaji wa Yanga chini ya benchi la ufundi lililoongozwa na Kocha Nasreddine Nabi wakiongozwa na kina Fiston Mayele, Djugui Diarra, Bakari Mwamnyeto na wengineo kila mmoja akicheza kwa kiwango chake mpaka mwisho ni wazi ubingwa wa ligi utaenda kwao.

“Yanga itaanza na Azam kisha Simba kama itashinda zote mbili itakuwa na asilimia 85 kubeba ubingwa na kutimiza malengo ya msimu huu,” alisema Zahera.

“Simba inapambana kupunguza pengo la pointi, ikifungwa hakuna timu nyingine ya kuizuia Yanga msimu huu. Pia ikishinda mechi hiyo itaongeza pengo la pointi na morali zaidi kwa wachezaji.”

“Pia hata kama Yanga itaambulia pointi nne kwa mechi hizo kwa maana ya kushinda moja na sare, itakuwa na asilimia 65 za kutangaza ubingwa japo itapata presha zaidi kutoka Simba iliyopo nyuma yao,” alifafanua Zahera.

Kocha huyo alisema kwa aina ya wachezaji waliopo kikosini kwa sasa wanaojituma uwanjani, ni wazi watampa kitui sahihi Nabi.

Zahera alisema: “Nimepata nafasi ya kuongea na wachezaji wote, kila mmoja kwa nafasi yake nimewaeleza jambo hilo na umuhimu wa mechi hizo mbili kabla ya kuzipigia hesabu mechi nyingine saba zitakazosalia kabla ya kumaliza msimu.”

Koch alisema kitu kingine kinachomfanya aamini Yanga inaenda kubeba ubingwa msimu huu kama itatoboa mbele ya Azam na Simba ni jinsi inavyocheza kwa bidii mechi za ugenini tofauti na misimu minne iliyopita.

“Yanga kuna baadhi ya mechi za ugenini msimu huu inatanguliwa kufungwa bao ila wachezaji wanatulia kwa kujipanga na kusawazisha mwisho wa mechi wanafunga la ushindi na kuondoka pointi zote tatu,” alisema Zahera na kuongeza;

“Sina shaka Yanga wanapocheza hapa Dar es Salaam, hivyo kama ugenini wanafanya vizuri naona dalili njema kwao ya kutwaa ubingwa wa ligi baada ya muda mrefu sasa na siyo sifa nzuri ya timu kubwa.”


MSIKIE MTEMI

Naye kiungo mkabaji wa zamani wa Simba na timu ya taifa, Taifa Stars, Mtemi Ramadhan amesema ameiangalia Ligi Kuu Bara msimu huu na kisha kuipa nafasi kubwa Yanga kubeba taji baada ya kulikosa kwa misimu minne mfululizo.

Mtemi aliyekuwa mmoja ya wachezaji walioshiriki Fainali za Afcon 1980 zilizofanyikia Nigeria, alisema haoni timu ya kuizuilia Yanga kubeba ubingwa msimu huu kwa aina ya kikosi ilichonacho na namna inavyocheza uwanjani.

“Wanacheza vizuri, sioni kama wanaweza kupoteza mechi tatu mfululizo ni timu nzuri inapambana kupata matokeo na naona msimu huu ni wao, upepo upo kwao labda washindwe wenyewe,” alisema Mtemi.

Hata hivyo mkongwe huyo alitoa ushauri kwa Kocha wa Yanga Nasreddine Nabi akimtaka kumpunguzia majukumu kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’, kwani amekuwa akikimbia sehemu kubwa ya uwanja bila sababu za msingi.

“Angalia uchezaji wa Aucho (Khalid) na Bangala (Yannick) hawatembei sana na mpira ila wanapiga mipira kwenye maeneo haraka, Sure Boy apewe jukumu maalum sio kukimbia kimbia, ni mchezaji mzuri lakini atachoka mapema,” alisema.

Mtemi alimzungumzia Clatous Chama wa Simba akisema jamaa anamkosha kwani amekamilika idara zote kuanzia kupiga pasi zenye uzito na anayeituliza timu, pia ni mbunifu.