ZA NDAANI KABISA: Huko Yanga kuna mtu anautaka urais
UCHAGUZI Mkuu wa Yanga unatarajiwa kufanyika Julai 10, huku habari Za Ndaani Kabisa zinasema kuwa mmoja wa vigogo wanaoifadhili timu hiyo anakipigia hesabu kitu cha urais wa klabu hiyo.
Habari kutoka ndani ya Yanga zilizopenyezewa kwenye kona hii, zinasema kigogo huyo anayetoka kwenye moja ya kampuni zinazoidhamini klabu hiyo ameanza kusuka mipango hiyo kitambo hata kabla mchakato wa Katibu Mpya ya klabu hiyo iliyohama kutoka kuendeshwa na wanachama na kuwa ya wanahisa (kampuni).
Inaelezwa kigogo huyo (jina limehifadhiwa kwa sasa) ameshaweka mipango yake mapema kwa baadhi ya watu wake wa karibu kwamba anakitaka kiti cha urais ambacho kwa sasa ni uenyekiti unaoshikiliwa na Dk Mshindo Msolla anayedaiwa hana mpango wa kukitetea.
“Kama unabisha subiri zoezi la kuchukua na kurudisha fomu zitakapoanza ndo utajua kwa undani ukweli huu, japo kuna baadhi ya wanachama wamejipanga kutafuta mtu wanayeamini atawafikisha nchi ya ahadi,” kilisema chanzo chetu.
Inadaiwa, kigogo huyo amekuwa akifanya kila kitu kwa sasa ili kutengeneza mazingira mazuri ya kuonekana kwa wanachama.