Yanga yarejea kileleni Ligi Kuu

Muktasari:

  • Mchezo huo ulikuwa ni wa 17 kwa Yanga na 20 kwa Namungo katika Ligi Kuu Bara msimu huu.

MUDATHIR Yahya amefunga bao lake la sita katika mechi saba za michuano yote wakati Yanga ikiilaza Namungo 3-1 kwenye Uwanja wa Majaliwa uliopo Ruangwa, Lindi na kurejea kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara.

Clement Mzize alifunga bao la pili baada ya kuiba mpira na Stephane Aziz Ki akaweka chuma cha tatu kwenye Uwanja wa Majaliwa na kuwa bao lake la 11 la Ligi Kuu msimu huu akiendelea kubaki katika nafasi ya pili ya chati ya vinara wa mabao wa ligi nyuma ya Feisal Salum 'Fei Toto' wa Azam FC mwenye mabao 12.

Wenyeji Namungo walipata bao la kufutia machozi kupitia kwa beki wa Yanga, Ibrahim Abdallah 'Bacca' aliyejifunga akiwa kwenye harakati za kuokoa katika dakika ya 70.

Ushindi uliirudisha Yanga kileleni mwa msimamo kwa kufikisha pointi 46, mbili juu ya Azam FC inayoshika nafasi ya pili kwa pointi 44, lakini Azam ikiwa imecheza mechi 20, ambazo ni tatu zaidi ya Yanga iliyocheza mechi 17.

Mchezo huo ulikuwa ni wa 17 kwa Yanga na 20 kwa Namungo katika Ligi Kuu Bara msimu huu.

Simba inayoshikilia nafasi ya tatu ikiwa na pointi 36 baada ya mechi 16, itacheza dhidi ya Coastal Union kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga Jumamosi hii Machi 9, 2024.

Kipindi cha kwanza cha mechi ya Yanga na Namungo kilimalizika bila bao huku timu zote zikishambuliana kwa kupokezana lakini hata hivyo hakuna iliyopata bao kwenye dakika 45 za mwanzo.

Yanga ilirejea kipindi cha pili kwa kasi na kuandika mabao matatu ya haraka haraka akianza kufunga Mudathir Yahya dakika ya 54, akafuata Clement Mzize dakika ya 57 na msumari wa mwisho kugongelewa na Stephane Aziz Ki katika dakika ya 63.

MABADILIKO YA GAMONDI
Katika mchezo huo, kocha mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi ilifanya mabadiliko ya wachezaji sita kwenye kikosi chake kutoka kile kilichocheza mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly ugenini na kufungwa 1-0.

Kipa Metacha Mnata alichukua nafasi ya Djigui Diarra, Nickson Kibabage akiingia eneo la Joyce Lomalisa, Salumu Abubakar akisimama nafasi ya Khalid Aucho, Maxi Nzengeli akichukua nafasi ya Kennedy Musonda, Clement Mzize akicheza eneo la Joseph Guede na Agustino Okrah kuingia nafasi ya Pacome Zouzoua.

Wakati huo, kikosi cha Namungo hakikuwa na mabadiliko ya mchezaji yeyote kutoka kile kilichocheza na Kagera Sugar mechi ya ligi Machi, 5 mwaka huu na kushinda bao 1-0.

Wakati mechi inaendelea kipindi cha pili, Yanga ilimtoa Okrah, Mudathir Yahya, Maxi Nzengeli na nafasi zao kuchukuliwa na Shekhan Khamis, Jonas Mkude na Bakari Nondo huku Namungo ikiwatoa Hamis Khalifa, Meddie Kagere, Hassan Kabunda na Pius Buswita nafasi zao zikichukuliwa na Hamad Majimengi, Kelvin Sabato, Hashim Manyanya na James Mwashinga.

NAMBA ZA MOTO
Yanga imeongeza namba karibu kwenye kila eneo ambapo imejikita kileleni mwa msimamo na alama 46 baada ya mechi 17 ikiiacha Azam nafasi ya pili na pointi 44 baada ya mechi 2o huku Simba ikikaa nafasi ya tatu na alama 36 baada ya mechi 13.

Aidha, Yanga imeongeza namba kwenye mabao ya kufunga ikifikisha 42, matatu nyuma ya Azam iliyofunga 45.

Kiungo mshambuliaji, Stephane Aziz Ki amefunga bao lake la 11, na kuendelea kumsogelea Feisal Salum 'Fei Toto' wa Azam anayeongoza kwa mabao akiwa amecheka na nyavu mara 12 huku asisti aliyoitoa kwa Mudathir Yahya ikiwa ya tatu kwake msimu huu.

Bao la Mudathir limekuwa la saba kwake kwa msimu, lile la Mzize likiwa la tatu kwake huku pasi ya mwisho aliyopiga Koassi Attohoula Yao ikiwa ya saba kwake, moja nyuma ya kinara, Kipre Junior wa Azam mwenye asisti nane.

Matokeo hayo yameifanya Namungo kusalia katika nafasi ya saba na alama 23 baada ya mechi 20.

Mchezo ujao, Namungo itacheza Machi 15 mwaka huu ugenini Mwanza dhidi ya Singida Fountain Gate iliyo nafasi ya 11 na alama 21, wakati Yanga itakuwa nyumbani Machi 11, kuikaribisha Ihefu inayoshika nafasi ya nane kwenye msimamo.

WASIKIE WENYEWE
Kocha Migel Gamondi wa Yanga alisema mchezo huo ulikuwa mgumu lakini anawapongeza wachezaji wake kwa kuipatia timu alama tatu muhimu.

"Lengo ni kuchukua ubingwa, kila mechi kwetu ni muhimu na tunacheza ili kushinda na nafurahi kwa matokeo ya leo.

"Nawapongeza wachezaji wetu kwa kujitoa na kuipa timu ushindi. Kama tutaendelea kucheza kama hivi, tutakuwa kwenye njia sahihi," alisema Gamondi.

Kocha msaidizi wa Namungo, Shedrack Nsajigwa 'Fuso', alisema timu yake imepoteza mchezo huo kutokana na ubora wa Yanga.

"Tulizidiwa na Yanga na tunawapongeza kwani walitumia makosa yetu na kupata mabao.

"Yanga ni timu inayojiamini pia ina uzoefu mkubwa, imefuzu robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ni timu nzuri. Hii mechi imeisha na sasa tunaenda kujipanga kufanya vizuri kwenye mechi zijazo," alisema Nsajigwa, ambaye beki wa kulia na nahodha wa zamani wa Yanga na timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars.

VIKOSI
Yanga: Metacha, Yao, Kibabage, Bacca, Job, SureBoy, Maxi, Mudathir, Mzize, Aziz Ki, Okrah.

Namungo: Nahimana, Kibailo, Charles, Mukombozi, Nyoni, Nyenye, Kabunda, Masawe, Kagere, Buswita, Mkoko.