Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kipa Pamba amtaja Manula

Muktasari:

  • Yona aliyetua Pamba msimu huu akitokea Tanzania Prisons baada ya kuhusishwa kwa muda mfupi na Yanga, amesema viwango walivyokuwa navyo makipa hao waliowahi kuwa ‘Tanzania One’ kwa vipindi tofauti ndio waliomfanya apende kudaka na anaamini ipo siku atafikia mafanikio yao.

KIPA wa Pamba Jiji, Yona Amos aliyemaliza nafasi ya nne kwa makipa waliokuwa na ‘clean sheets’ nyingi baada ya Moussa Camara wa Simba, Diarra Djigui na Patrick Munthari ameshindwa kujizuia na kuwataja Aishi Manula, Juma Kaseja na Ivo Mapunda kuwa walichangia kuipenda nafasi hiyo.

Yona aliyetua Pamba msimu huu akitokea Tanzania Prisons baada ya kuhusishwa kwa muda mfupi na Yanga, amesema viwango walivyokuwa navyo makipa hao waliowahi kuwa ‘Tanzania One’ kwa vipindi tofauti ndio waliomfanya apende kudaka na anaamini ipo siku atafikia mafanikio yao.

Kipa huyo anayeshika namba mbili ya makipa wazawa waliofanya vizuri msimu huu nyuma ya Munthari wa Mashujaa kwa kuwa na clean Sheet 11, tatu pungufu na alizokuwa nazo mwenzake, alisema Manula, Mapunda na Kaseja wamejijengea heshima mbele ya wadau wa soka kwa kucheza kwa muda mrefu wakiwa katika viwango vya juu.

“Mapunda na Kaseja enzi zao walikuwa wakicheza unatamani wanachokifanya jinsi ya kuokoa hatari, kupanga timu, uongozi ndani ya uwanja, kudaka penalti na nidhamu kubwa ambayo iliwasaidia kila msimu unawaona ni bora,” alisema Amos na kuongeza:

“Kuhusu Manula bado ni kipa mzuri ndio maana ameitwa timu ya taifa. Naamini msimu ujao atarejea kwa ushindani. Binafsi kwao nimejifunza vitu vingi hasa ninapofanya vizuri kutojibweteka na kujipanga kwa kuongeza ubora zaidi msimu unaofuata.”

Mbali na hilo, alisema msimu ulioisha unatoa picha jinsi ambavyo ule ujao Ligi Kuu itakavyokuwa ngumu na kama mchezaji anajipanga kuhakikisha anaendeleza alipoishia.

“Kitu ninachokikumbuka msimu ulioisha ni kuokoa shuti la Ibrahim Ajibu wa Dodoma Jiji mechi hiyo ilipigwa Mwanza. Kila mtu alijua nafungwa pia Ligi Kuu ilikuwa nzuri na ushindani mkubwa,” alisema Amos ambaye nje na soka ana fani ya udereva.

Kipa huyo ni mmoja wa nyota walioisaidia Pamba iliyorejea katika Ligi Kuu msimu huu baada ya kuisotea kwa miaka 23, kusalia kwa msimu ujao baada ya awali kuanza vibaya kiasi cha kubadilisha makocha kabla ya kumpa kazi Fred Felix ‘Minziro’ aliyeibadilisha kiuchezaji katika duru la pili.

Pamba ilimaliza nafasi ya 11 ikiwa na pointi 34 ikishinda mechi nane kati ya 30 ilizocheza, ikitoka sare 10 na kupoteza 12, huku ikifunga mabao 22 na kufungwa 33, ikiiacha timu iliyoanda nao KenGold ikishuka sambamba na Kagera Sugar.