Morice mikononi mwa mabosi wa Simba

Muktasari:
- Unamkumbuka Morice Abraham? Kiungo kijana wa Kitanzania aliyekuwa akifanya mazoezi na Simba kwa muda wa takribani miezi miwili. Taarifa zinasema kuwa aliomba kufanya mazoezi na timu hiyo ili kujiweka fiti, lakini sasa mambo yanaonekana kubadilika.
KLABU ya Simba imetoa mapumziko kwa wachezaji wake, lakini kabla ya kurejea na kuanza maandalizi ya msimu mpya, jambo moja kubwa linaendelea chini kwa chini katika suala la usajili.
Unamkumbuka Morice Abraham? Kiungo kijana wa Kitanzania aliyekuwa akifanya mazoezi na Simba kwa muda wa takribani miezi miwili. Taarifa zinasema kuwa aliomba kufanya mazoezi na timu hiyo ili kujiweka fiti, lakini sasa mambo yanaonekana kubadilika.
Inaelezwa kuwa kiwango alichokionyesha katika kipindi hicho kimemkosha kocha wa timu hiyo, Fadlu Davids, ambaye sasa anamhitaji kiungo huyo abaki kikosini rasmi.
Fadlu pamoja na benchi lake la ufundi wameridhishwa na uwezo wa Abraham, ambaye awali alikuwa anakipiga katika klabu ya Spartak Subotica ya Serbia, japo hadi sasa bado hajasaini mkataba na Simba, lakini dili lake limeshapita.
Kwa mujibu wa chanzo cha kuaminika, tayari mchezaji huyo, kocha na scout wa timu wamekubaliana juu ya mpango wa kumjumuisha Abraham kwenye kikosi, lakini uamuzi wa mwisho uko mikononi mwa uongozi wa Simba.
“Mchezaji ameridhishwa na mradi wa kocha, lakini hajapewa mkataba rasmi hadi sasa. Tunaangalia ndani ya siku chache kama hakuna kitakachoendelea, inabidi Simba waangalie chaguo lingine, lakini tayari kocha ameshasema asajiliwe kutokana na ubora ambao ameuonyesha mazoezini kwa kipindi kifupi,” kilisema chanzo hicho.
Abraham ni kiungo anayeweza kucheza nafasi zote za katikati kwa ufanisi mkubwa. Kama atafanikiwa kusaini mkataba na Simba, huenda akaongeza nguvu kwenye kikosi hicho kilichosheheni nyota wa kimataifa.
Kinda huyo alijizolea sifa wakati akiwa sehemu ya kikosi cha timu ya taifa ya vijana ‘Serengeti Boys’ kilichoshiriki mashindano ya Kombe la Mataifa Afrika kwa vijana wa chini ya umri wa miaka 17 mwaka 2019.