Yanga yapaa, Manji bado

Wachezaji wa timu ya Yanga
Muktasari:
- Hadi jana mchana, Manji alikuwa akishikiliwa na Polisi, huku ofisi yake ikienda kupekuliwa kwa ajili ya kutafuta ushahidi kutokana na kutajwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuwa anahusika na unga.
WAKATI msafara wa Yanga wenye watu 30 wakiwamo wachezaji 20 ukipaa asubuhi ya leo kuelekea Comoro, huku nyuma Mwenyekiti wa klabu hiyo, Yusuf Manji bado alikuwa akishikiliwa na Polisi katika sakata la dawa za kulevya.
Hadi jana mchana, Manji alikuwa akishikiliwa na Polisi, huku ofisi yake ikienda kupekuliwa kwa ajili ya kutafuta ushahidi kutokana na kutajwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuwa anahusika na unga.
Manji alishikiliwa na polisi tangu juzi Alhamisi alipojipeleka mwenyewe kuitikia wito wa Makonda aliyemtaka aripoti jana, lakini yeye akawahi mapema.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Siro alisema Manji na Mchungaji wa Kanisa la Ufufuo, Josephat Gwajima walilala rumande huku wakiendelea kuhojiwa na watatoka watakapojiridhisha na mahojiano yao.
“Manji na Gwajima bado tunawashikilia, wapo rumande, si kila mtu anayekuja kuhojiwa hapa analala rumande, kuna waliokuja tumewahoji na kuwaachia wakati baada ya kujiridhisha,” alisema Kamanda Siro.
Wengine waliotajwa pamoja na Manji ji Mwenyekiti wa zamani wa DRFA na aliyekuwa Mbunge wa Kinondoni, Idd Azan ambaye alifika Kituo Kikuu ca Polisi jana saa 3 asubuhi na Siro alisema atatoa maelezo zaidi ya mtuhumiwa huyo na wenzake Jumatatu.
Baadhi ya wanachama wa Yanga akiwemo mwenyekiti wao wa zamani, Francis Kifukwe, makamu mwenyekiti, Clement Sanga walikuwa miongoni mwa walifika kituoni hapo kujua hatma ya mwenyekiti wao.
TIMU YAPAA
Yanga ambayo juzi ilifanya mazoezi ya mwishomwisho Uwanja wa Taifa leo imepaa kuelekea Comoro kuumana na Ngaya de Mbe, huku viongozi wakiapa kwenda kuua ndege wawili kwa jiwe moja.
Sanga, alisema wanaenda kupambana ili kupata ushindi kumfariji bosi wao, lakini kufanya vema katika mechi zao za kimataifa.
Kikosi cha wachezaji 20 na viongozi wanane na wakuu wa msafara wawili wamepaa kuelekea Comoro kwa mchezo huo utakaopigwa kesho Jumapili alasiri.
Wachezaji waliondoka ni; Deo Munishi, Ally Mustafa, Deus Kaseke, Mwinyi Haji, Thabani Kamusoko, Haruna Niyonzima, Amissi Tambwe, Simon Msuva, Geofrey Mwashuiya, Said Makapu, Hassan Kessy, Juma Mahadhi na Yusuf Mhilu.
Wengine ni Obrey Chirwa, Nadir Haroub, Justine Zulu, Kelvin Yondani, Juma Abdul, Oscar Joshua na Emmanuel Martin.
Benchi ni pamoja na makocha George Lwandamina, Noel Mwandila, Juma Mwambusi na Juma Pondamali, Dk. Edward Bavu, meneja Hafidh Saleh Mohamed Mwaliga na Jacob Onyango, viongozi wa msafara ni Mussa Kisoki (TFF) na Paul Malume (Yanga).
Kocha Mwambusi aliliambia Mwanaspoti kuwa; “Kikosi kipo vizuri tumewaandaa wachezaji kisaikolojia kupambana na kushinda, wote wanaokwenda wapo vizuri kasoro wanaoumwa na ndio maana tumewaacha,” alisema.
WAOKOA MAMILIONI
Uamuzi wa Yanga kuondoka leo na kurejea Jumanne umeokoa mamilioni ya fedha kutokana na gharama za maisha zilizopo nchini humo kama Yanga ingewahi siku mbili kabla.
Yanga imeamua kuondoka nchini leo Alfajiri na jioni itafanya mazoezi mepesi kabla ya kesho kuwavaa wenyeji wao Ngaya.