Yanga yamfungulia mlango Fei Toto
Uongozi wa Yanga leo Machi 6, 2023 umemwandikia barua mchezaji Feisal Salum 'Fei Toto' kumtaka aripoti kambini haraka iwezekanavyo na kuendelea kuutumikia mkataba wake kama mchezaji halali wa Yanga mpaka Mei 2024.
Yanga imemuandikia mchezaji huyo barua hiyo baada ya maamuzi ya Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuamua Fei Toto ni mchezaji halali wa Yanga.
Katika taarifa iliyotolewa na Yanga imesema klabu hiyo ipo tayari kumpokea Fei Toto na kumjumuisha kwenye kikosi, pia kwa kuzingatia sera na utaratibu wa klabu katika kuwaongezea mikataba wachezaji wake wanaofanya vizuri wapo tayari kuendelea na mazungumzo na mchezaji huyo na wawakilishi wake ili kuboresha mkataba wake kama wataridhia.
Klabu hiyo pia imesema ipo tayari kumruhusu mchezaji huyo kuondoka kwa kuzingatia matakwa ya mkataba ya mkataba na utaratibu wa sheria za uamisho wa wachezaji zinazotambulika na TFF na FIFA.
"Ikiwa pia kuna klabu yoyote inahitaji huduma ya mchezaji huyu, klabu ya Yanga iko tayari kufanya mazungumzo wakati wowote," imeeleza taarifa hiyo