Fei Toto atinga TFF kuomba kuvunja mkataba Yanga
Muktasari:
- Kiungo Feisal Salum amekuwa na mvutano na klabu ya Yanga juu ya sakata la mkataba ambapo aliamua kuvunja mkataba, huku uongozi wa timu ukimshtaki kwa mamlaka za michezo kutaka ajieleze kwa kutofuata taratibu.
Dar es Salaam. Kiungo wa Yanga, Feisal Salum ‘Fei Toto’ amewasili ofisi za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) akiwa na mwakilishi wake, Jasmine Razack ambapo amewasilisha barua ya kuomba kuvunja mkataba na timu yake ili awe huru.
Fei Toto amefika TFF na mwakilishi wake, Jasmine Razack ambaye alizungumza na waandishi wa habari na kueleza nia ya mchezaji huyo.
"Ninaomba tuvute subira, leo Feisal kaleta ombi lake ninaimani kama litashughulikiwa na TFF, chombo pekee kinachoweza kuvunja mkataba wa mchezaji ni TFF," amesema Razack
Yanga awali ilipeleka shauri kwenye kamati ya sheria na hadhi za wachezaji ya Shirikisho la Soka nchini (TFF) ikimtaka Feisal kutoa maelezo kwanini ameondoka ndani ya kikosi hicho na kuandika barua ya kuaga akiichapisha katika ukurasa wake rasmi wa mitandao yake ya kijamii, Desemba 24, 2022 bila mazungumzo ya pande zote mbili.
Baada ya hapo shauri hilo kwa mara ya kwanza lilisikilizwa Ijumaa ya Januari 6 mwaka huu na baada ya hapo TFF ilitoa barua iliyoeleza Feisal bado ni mchezaji halali wa Yanga kimkataba na kutoa nafasi ya upande wa Feisal kuomba mapitio (review) ya shauri hilo kama hawataridhika na uamuzi uliotolewa.
Hata hivyo, upande wa Feisal kupita kwa mawakili wake Nduruma na Makubi hawakukubaliana na majibu ya TFF na kuomba mapitio ambayo yalisikilizwa Machi 4, mwaka huu katika ofisi za makao makuu ya TFF ambapo ombi lao liligonga mwamba.