Yanga yala vichwa simba

Muktasari:
- Anzia nafasi ya kipa ambako, Daniel Agyei anachukua nafasi ya Angban, hapo kati James Kotei anachukua jezi ya Jonas Mkude au Mwinyi Kazimoto, mbele Juma Liuzio anasimama kwa Muivorycoast Fredrick Blagnon. Pastory Athanas ana nafasi kubwa ya kukabidhiwa majukumu ya Ibrahim Ajib.
KAMA usajili wa Simba ukikamilika freshi kwenye siku ya mwisho leo Alhamisi, inamaanisha kuwa inaweza kuwa na mabadiliko ya wachezaji wanne hadi watano katika kikosi cha kwanza kilichocheza dhidi ya Yanga, Oktoba Mosi mwaka huu.
Anzia nafasi ya kipa ambako, Daniel Agyei anachukua nafasi ya Angban, hapo kati James Kotei anachukua jezi ya Jonas Mkude au Mwinyi Kazimoto, mbele Juma Liuzio anasimama kwa Muivorycoast Fredrick Blagnon. Pastory Athanas ana nafasi kubwa ya kukabidhiwa majukumu ya Ibrahim Ajib.
Angban na Blagon wamerejeshwa kwao lakini pona ya hao wengine imetokana na kwamba ni wazawa hivyo hawataigharimu klabu fedha nyingi na watasubiri benchi. Angban ndiye aliyemleta Bongo straika Mu-Ivory Coast mwenzake, Blagnon na wote panga limewapitia, Pata picha wakiwa katika ndege wakirejea kwao Abidjan watakuwa na mazungumzo gani?
Ikaushie kwanza Simba. Yanga haikuwa na mbwembwe dirisha hili la usajili linalofungwa leo saa 6.00 usiku, ilimwongeza kiungo Mzambia, Justine Zulu na hadi jana ilikuwa katika mazungumzo ya mwisho na JKU ya Zanzibar kuhusu usajili wa straika, Emmanuel Martin aliyewapiga mabao mawili wikiendi iliyopita.
Ujio wa Zulu ni majibu ya kilio cha muda mrefu kwa Yanga ambayo ilikuwa inakosa kiungo wa chini kama Athuman Iddi ‘Chuji’ na Frank Domayo ambao waliachana na timu hiyo mwaka 2014. Kifupi ni kwamba nafasi ya Zulu iko wazi kikosi cha kwanza.
Hata hivyo Kocha George Lwandamina atakuwa na wakati mgumu kuamua amtumie Zulu na Thaban Kamusoko ambaye ndiye mchezaji bora wa kigeni nchini pamoja na Niyonzima au kumtupa mmojawao benchi. Ili kuwatumia Zulu, Kamusoko na Niyonzima pamoja, kocha atalazimika kumpumzisha Deus Kaseke ili atumie mfumo wa 4-2-3-1 ama 4-2-3-1 ambao unaruhusu uwepo wa viungo watatu.
Kama Yanga watamalizana na Martin ni ishara kuwa wataongeza ushindani kwa mastraika wazawa, Malimi Busungu na Matteo Antony ambao hawana nafasi kikosi cha kwanza kwani washambuliaji wenzao, Donald Ngoma na Amissi Tambwe wapo katika kiwango cha juu.
Simba hadi jana jioni ilikuwa imewasajili wachezaji watatu; Waghana, Daniel Agyei (kipa), kiungo Daniel Kotei na mshambuliaji Pastory Athanas aliyetokea Stand Utd. Katibu Mkuu wa Simba, Patrick Kahemele alithibitisha kuwa wamemnasa straika, Juma Liuzio atakayetua kwa mkopo akitokea Zesco ya Zambia. Simba pia ilikuwa katika mazungumzo na Ally Shomary wa Mtibwa ambaye alisema Simba imebaki kumalizana na waajiri wake ili avae jezi nyekundu.
Ujio wa nyota hao umesababisha kuchomolewa Angban, kiungo Mussa Ndusha na Blagnon. Wengine ni straika, Ame Ali aliyekwenda Kagera Sugar, kiungo Awadhi Juma na beki Malika Ndeule aliyerejea Mwadui. Usajili huo unamaanisha Agyei ni moja kwa moja kikosi cha kwanza akisaidiwa na Manyika Jr ambaye tayari ameletewa kocha Mkenya, Rama Salim ili kumnoa. Kotei anaibua ushindani eneo la kiungo na Kocha Joseph Omog atalazimika kumuweka benchi nahodha, Jonas Mkude au kuwachezesha pamoja na kumuweka benchi Mzamiru Yassin au mkongwe, Mwinyi Kazimoto ambaye mkataba wake unaisha mwisho wa msimu. Safu ya ushambuliaji Simba inaweza kuwa na mwonekano mpya, Liuzio anaweza kuanza na Mavugo au Pastory ambaye anamudu pia kucheza winga. Omog pia atakabiliwa na changamoto ya kuamua nani anaweza kuwa kikosi cha kwanza kwani Ajib na Mohammed Ibrahim ‘MO’ nao wanaonekana kuwa vizuri. Hata hivyo MO an nafasi kubwa kuwa ‘super sub’ nafasi aliyokuwa akifanya vizuri mzunguko wa kwanza.
Shomary pia ana faida kwani anamudu kucheza nafasi ya beki wa kulia na winga hivyo anaweza kuanza badala ya Janvier Bokungu ama kusubiri benchi na kuwa mbadala wa Shiza Kichuya ambaye ndiye anatokea upande wa kulia kwa Simba.
TIMU NYINGINE
Azam hadi jana jioni ilikuwa katika hatua za mwisho za kumsainisha beki Mghana, Yakub Mohammed anayechukua nafasi ya kiungo, Jean Mugiraneza. Beki huyo aliyetokea Aduana Stars ya Ghana ataungana na nyota wengine kutoka Ghana, Yahya Mohammed, Samuel Afful na Enock Agyei.
Klabu ya Majimaji ya Songea tayari imemsajili straika Kelvin Sabato ambaye atakwenda kuimarisha safu ya ushambuliaji ya timu hiyo huku pia wakiwa katika mazungumzo na beki wa zamani wa Azam, Waziri Salum.
African Lyon imekubali kumchukua kipa Denis Richard kwa mkopo kutoka Simba huku ikiwa katika harakati za kuongeza wachezaji kadhaa wa kigeni ambao walikuwepo katika majaribio klabuni hapo. Lyon imeachana na nyota wake raia wa Uganda, Samuel Ottong, Hood Mayanja na Titto Okello.
AZAM YOTE MPYA
AZAM imefanya usajili mwingine wa kutisha baada ya kuwatia kitanzini wachezaji watatu ambao ni beki wa kati Yakubu Mohammed, kiungo mkabaji Stephan Kingue Mpondo na winga Joseph Mahundi.
Mabingwa hao watetezi wa Kombe la Kagame waliingia mikataba na nyota hao jana Jumatano jijini Dar es Salaam chini ya usimamizi wa Ofisa Mtendaji Mkuu, Saad Kawemba, Meneja Mkuu, Abdul Mohamed, Kocha Mkuu Zeben Hernandez, Meneja wa timu, Phillip Alando. Wakati Mohammed, 20, amesaini mkataba wa miaka mitatu akitokea Aduana Stars ya Ghana, akiziba nafasi ya Pascal Wawa, Mpondo anayetokea Coton Sports ya Cameroon, alisaini mwaka mmoja.
Katika kuongeza makali kwenye eneo la ushambuliaji, Azam FC ilimaliza ngebe kwa kumpa mkataba Mahundi, ambaye amesaini miaka miwili akitokea Mbeya City. Mahundi ni zao la timu yao ya vijana.