Yanga yaivuruga Simba 2021

Muktasari:
SIMBA ndio timu bora Tanzania kwa misimu minne mfululizo sasa na msimu huu inajiaandaa kubeba taji lao la 22 tangu Ligi Kuu Bara ianzishwe mwaka 1965.
SIMBA ndio timu bora Tanzania kwa misimu minne mfululizo sasa na msimu huu inajiaandaa kubeba taji lao la 22 tangu Ligi Kuu Bara ianzishwe mwaka 1965.
Mchakato wa mabadiliko ya kiuongozi ambao umempa Mohammed ‘Mo’ Dewji mamlaka ya kuwa Mwenyekiti ya Bodi ya Wakurugenzi ya Klabu ya Simba, umeleta mabadiliko makubwa kwa klabu ya Simba na soka la Tanzania kwa ujumla.
Licha ya kwamba mchakato huo haujakamilika ukikwama kwenye Tume ya Ushindani (FCC), lakini Simba tayari imepiga hatua kubwa sana ndani na nje ya uwanja.
Uwanjani kwa mara ya pili ndani ya miaka mitatu imefika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika huku ikiwafunga mabingwa watetezi Al Ahly ya Misri na kumvimbia kila mpinzani wake mkubwa.
Simba ya sasa ni Next Level. Inaweza kumpiga yeyote Afrika. Sio timu inayokwenda kinyonge tena kwenye mechi yoyote ile na mpinzani yeyote ni lazima aingie uwanjani akitambua kuwa anapambana na Simba kweli, mfalme wa mbuga ambaye usipojipanga atakurarua vipande vipande.
Chini ya bilionea Mo Dewji, Simba imekuwa na hadhi ya klabu kubwa huku juhudi zikifanywa na viongozi wasiolala kuhakikisha inaondoka kwenda mbali zaidi ya Simba ile ya zamani iliyokuwa ikiendeshwa kiujanja ujanja kwa kutegemea mifuko ya watu, bila ya kupigia magoti watu, wachezaji hawapati mishahara.
Kuna mengi ambayo bado hayajafanyika ili kuilinganisha na klabu kubwa nyingine za Afrika kwa kuangalia miundombinu na mafanikio Afrika, lakini hapa ilipo imefika mbali sana ukiangalia kule ilikotoka.
Kikosi kipana kilichojaa nyota ambao kwenye klabu nyingine wangekuwa tegemeo la kikosi cha kwanza, Simba iko katika njia sahihi ya kulifikisha mbali soka la Tanzania.
Ibrahim Ajibu ambaye amekaa benchi msimu mzima Simba, ndiye aliyekuwa nahodha wa Yanga kabla hajatimka Jangwani kurejea Msimbazi na unaweza usiamini kwamba Bernard Morrison ‘Mzee wa Kuwakera’ ambaye ameishia kuwa ‘supet sub’ wa Simba akianzishwa katika mechi chache tu, ndiye aliyekuwa ‘supastaa’ wa kikosi pale Yanga.
Hata kipa wa akiba Simba, Benno Kakolanya na beki wa kushoto chaguo la pili Msimbazi, Gadiel Michael wote walikuwa chaguo la kwanza katika kikosi cha Yanga kabla ya kuhamia mtaa wa pili.
Na wakali wengine wanaoanzia benchi kama Meddie Kagere, Chris Mugalu, Erasto Nyoni, Mzamiru Yassin, Said Ndemla, Miraj Athuman na wengine wengi wangeweza kuwa kikosi cha kwanza cha timu nyingi za Ligi Kuu Bara. Hiyo ndiyo levo ya Simba kwa sasa na ubingwa wa nne mfululizo wa Ligi Kuu wanaojiandaa kuutwaa msimu huu ni matunda ya mchakato wao wa mabadiliko ya kiuendeshaji na wanastahili kila kitu kwa juhudi zao.
YANGA WABABE WAO
Mahasimu wao Yanga wamezinduka baada ya kuona wanazidi kuachwa mbali. Misimu minne bila ya ubingwa wa Ligi Kuu ni jambo linalowaumiza sana mashabiki wao.
Mchakato wa mabadiliko waliouanza kwa kushirikiana na Ligi Kuu ya Hispania (Laliga) na klabu ya Sevilla, umerejesha matumaini kwa Wanajangwani ambao mwezi uliopita walipitisha rasimu ya mabadiliko ya uendeshwaji.
Ndio, Yanga ndo mabingwa wa kihistoria wakilitwaa taji la Ligi Kuu mara 27, lakini wameachwa mbali na Simba katika mambo mengi kwa sasa na wanayahitaji sana mabadiliko haya ili kwenda levo zile.
Kwa msimu huu, licha ya kutokuwa ma mwenendo mzuri, Yanga haijapotea sana na inaweza kujipanga kuifuata Simba.
Ukiachana na ukweli kwamba Yanga ndio timu ya kwanza kuanzishwa, kisha ikameguka ikaundwa Simba, wanajangwani bado wanajivunia rekodi bora dhidi ya Simba. Katika mechi za Ligi ya Bara tangu ilipoanzishwa 1965, Yanga imeifunga Simba mara 38, huku Simba ikiwafunga wanajangwani mara 31 na zimetoka sare mara 37.
Kipigo cha Jumamosi iliyopita cha 1-0 kinaifanya Yanga kuhitimisha msimu wa 2020-21 ikiwa na matokeo bora zaidi ya Simba kwani kufikia sasa zimekutana mara tatu katika mashindano yote, Yanga imeshinda mara mbili (ikiwamo Kombe la Mapinduzi) na sare moja. Simba ina nafasi ya kuboresha rekodi baina yao kwa kuifunga Yanga katika fainali ya Kombe la Shirikisho (ASFC) Julai 25 mjini Kigoma, lakini matokeo yoyote hayatabadili rekodi bora ya Yanga dhidi ya Simba msimu wa 2020-21 ambayo ni ushindi mara mbili.
Mechi nyingine watakayokutana watani hao mwaka huu, haitakuwa ya msimu huu, itakuwa ni ya ufunguzi wa msimu ujao wa 2021-22 katika mechi ya Ngao ya Jamii.
Msimu huu, Yanga tayari ina kombe moja la Mapinduzi, Simba inajiandaa kulitwaa lao la kwanza msimu huu la Ligi Kuu Bara, kisha zote mbili zitashindania na la pili zitakapokutana katika fainali ya Kombe la Shirikisho (ASFC) utaochezwa Julai 25, mkoani Kigoma.