Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Singida BS yapoteza tena dhidi ya Simba, vita bado mbichi

Muktasari:

  • Hiyo ilikuwa katika mechi ya kiporo ya Ligi Kuu Bara iliyopigwa leo Mei 28, 2025 kwenye Uwanja wa KMC Complex, Mwenge jijini Dar es Salaam ambapo Simba imeendeleza ubaya ubwela wake ndani ya ligi.

MSHAMBULIAJI wa kimataifa kutoka Uganda, Steven Mukwala, ameendelea kuonyesha thamani yake ndani ya Simba SC kwa kufunga bao pekee lililoiwezesha timu hiyo kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Singida Black Stars.

Hiyo ilikuwa katika mechi ya kiporo ya Ligi Kuu Bara iliyopigwa leo Mei 28, 2025 kwenye Uwanja wa KMC Complex, Mwenge jijini Dar es Salaam ambapo Simba imeendeleza ubaya ubwela wake ndani ya ligi.

Mukwala ambaye kwa sasa anaonekana kuwa moto wa kuotea mbali, aliendelea kutoka alipoishia kwenye mechi iliyopita ya ligi kwa kufunga bao lake la 12 msimu huu, likiwa ni la tatu mfululizo katika mechi mbili za karibuni kwenye ligi.

Katika mechi hiyo, Mukwala alianza kwa mara ya pili mfululizo kwenye mashindano yote mbele ya mshambuliaji mwenzake, Leonel Ateba, akahakikisha anaipa Simba kile kilichohitajika ushindi muhimu uliopunguza tofauti ya pointi dhidi ya vinara Yanga kutoka nne hadi moja.

Bao hilo lilifungwa dakika ya 43 baada ya pasi safi kutoka kwa Jean Charles Ahoua ambaye sasa amefikisha asisti nane.

Mukwala aliitumia nafasi hiyo kwa ustadi mkubwa kuuweka mpira wavuni, alimdanganya kipa wa Singida Black Stars, Obasogie Amas, kwa chenga kabla ya kutupia wavuni kwa ufanisi mkubwa na kuwapa mashabiki wa Simba sababu ya kushangilia kabla ya mapumziko.

Ingawa alikosa nafasi mbili za wazi ndani ya dakika 30 za mwanzo, lakini kasi ya Mukwala iliwatesa mabeki wa Singida Black Stars wakiongozwa na Frank Kwabena na Anthony Tra Bi Tra, ambao walionekana kushindwa kumdhibiti Mganda huyo kila alipogusa mpira.

Uchokozi wake ulifanya safu ya ulinzi ya Singida Black Stars kuwa na kazi kubwa hadi mapumziko.

Kwa upande wa Singida Black Stars, ilipoteza nafasi mbili muhimu kipindi cha kwanza kupitia kwa Jonathan Sowah, huku moja ya nafasi hizo akiangushwa kwenye eneo la hatari, tukio lililoibua mjadala kwa mashabiki waliodai ilistahili kuwa penalti, lakini mwamuzi Elly Sasii hakuamua hivyo.

Kipindi cha pili kilianza kwa Singida kufanya mabadiliko ya haraka, akitolewa Kelvin Nashon aliyekuwa na kadi ya njano, nafasi yake ikachukuliwa na Damaro Camara. Mabadiliko hayo yaliongeza kasi kwa upande wa timu hiyo, waliotawala sehemu ya kiungo na kupeleka mashambulizi mfululizo.

Hata hivyo, Kocha wa Simba, Fadlu Davids hakukaa kimya. Alifanya mabadiliko ya kimkakati kwa kumtoa mshambuliaji Ellie Mpanzu na kumuingiza beki wa kati Abdulrazak Hamza, hatua iliyowawezesha kubadili mfumo kutoka wachezaji wawili wa kati hadi watatu wakicheza Che Malone Fondo, Chamou Karaboue, na Hamza.

Mabadiliko hayo yalizidi kuimarisha ukuta wa Simba huku Mohammed Hussein na Shomari Kapombe wakipewa uhuru zaidi wa kupeleka mashambulizi kutoka pembeni, jambo lililowafanya Singida washindwe kupata mwanya wa kusawazisha.


SINGIDA YAPOTEZA TENA, SIMBA YAVUNA ALAMA ZOTE SITA

Kwa mara ya pili mfululizo msimu huu, Singida Black Stars imeangukia mikononi mwa Simba. Katika mechi ya duru la kwanza, ilifungwa pia bao 1-0 nyumbani kwao kupitia Fabrice Ngoma. Sasa ni wazi, Simba imefanikiwa kuvuna pointi zote sita dhidi ya Singida Black Stars, jambo linalowapa ari kubwa kuelekea mechi zao tatu za mwisho.


VITA HAIJAISHA

Licha ya Simba kuibuka na ushindi mara mbili dhidi ya Singida Black Stars kwenye ligi, bado timu hizo hazijamalizana. Mei 31, zitakutana kwenye nusu fainali ya Kombe la FA pambano linalotarajiwa kuwa la kisasi kwa upande wa Singida Black Stars, huku Simba ikilenga fainali nyingine msimu huu.


CAMARA, MUKWALA WAONGEZA NAMBA

Kumalizika kwa dakika tisini huku Simba ikishinda bao 1-0, imemfanya kipa Moussa Camara kufikisha clean sheet 17 akiendelea kuongoza kwa tofauti ya mbili dhidi ya Djigui Diarra wa Yanga mwenye 15.

Katika mechi tatu zilizobaki, Camara anahitaji mechi mbili pekee kutoka na clean sheet kujihakikishia utawala wake kwani akifikisha 19 hazitafikiwa na kipa mwingine msimu huu.

Kwa upande mwingine, Steven Mukwala amefikisha mabao 12 sawa na Leonel Ateba ambaye naye anacheza Simba. Nyota hao wapo nyuma ya kinara Jean Charles Ahoua kwa mabao matatu kwani hivi sasa anayo 15. Chini ya Ahoua kuna washambuliaji wawili wa Yanga, Clement Mzize na Prince Dube ambao kila mmoja amefunga mabao 13.

Jonathan Sowah ambaye alianza kikosi cha kwanza katika timu ya Singida Black Stars, ameshindwa kutumia fursa ya kuongeza mabao, hivi sasa amefunga 11 wakati Elvis Rupia wa Singida Black Stars naye akifunga mabao 10.