Yanga yaitosa Arusha

Muktasari:
Yanga ilialikwa na Arusha FC pamoja na Madini kwa ajili ya kucheza mechi mbili za kirafiki na timu hizo zinazojiandaa na ligi daraja la pili msimu ujao.
Yanga yaitosa Arusha
Bertha Ismail, Mwananchi
Arusha. Mabingwa watetezi Ligi Kuu Bara, Yanga imeshindwa kutimiza ahadi yake ya kucheza mechi ya kirafiki Mkoani Arusha.
Yanga ilialikwa na Arusha FC pamoja na Madini kwa ajili ya kucheza mechi mbili za kirafiki na timu hizo zinazojiandaa na ligi daraja la pili msimu ujao.
Yanga ilitaraji kucheza mechi zake mbili hizo kati ya Aprili 29 na Mei 5, lakini baada ya kipigo cha Mbao na kuondolewa katika Kombe la FA imeshindwa kutimiza ahadi yake kwa mashabiki wake wa mkoa huo.
Katibu Mkuu wa Yanga, Boniface Mkwasa alisema wameshindwa kupita Arusha kama walivyokubalia kutokana na sababu zilizokuwa nje ya uwezo wao.
"Tulikuwa tupitie Arusha baada ya Mwanza, lakini mambo yamekwenda ndivyo sivyo hivyo tumehairisha hadi tukamilishe mechi tano za Ligi Kuu maana macho na masikio yetu kwa sasa yapo huko."
Katibu mkuu wa AFC, Charles Mwaimu alisema walitegemea kucheza mechi hiyo kabla ya kuanza kambi yao lakini sasa limeshindikana hivyo wanaendelea na ratiba zao.
"Tunajiandaa na ligi daraja la pili msimu ujao hivyo tumeingia kambini mapema ila tuliwaalika Yanga tucheze mechi ya kirafiki kama kuzindua kambi, lakini ratiba yao imekuwa ngumu mechi hiyo haitakuwepo tena."