Yanga yaharibu hali ya hewa, Mbeya City hali tete

Muktasari:

  • Mbeya City ilipanda Ligi Kuu msimu wa mwaka 2013/14 chini ya Juma Mwambusi na kuanza msimu kwa kishindo baada ya kumaliza msimu nafasi ya tatu wakati Azam ikitwaa ubingwa na Yanga ikishika nafasi ya pili huku Simba nafasi ya nne

Sare ya mabao 3-3 iliyopata Mbeya City leo Jumanne Juni 6 dhidi ya Yanga imezidi kuwaweka katika hali mbaya kwenye msimamo wa Ligi Kuu.

Sare hiyo imeifanya Mbeya City kufikisha alama 31 huku mchezo wa mwisho ikikutana na KMC ambayo leo imecheza na Tanzania Prisons.

Mchezo wa kwanza msimu huu Novemba 22, 2022 Uwanja wa Mkapa Yanga ilishinda mabao 2-0 yote yakifungwa na Fiston Mayele dakika ya 24 na 78.

Katika michezo 16 walizokutana Mbeya City imeshinda mchezo mmoja uliochezwa Uwanja wa Sokoine, Novemba 2, 2016 ukiwa msimu wa pili kwa Mbeya City Ligi Kuu hata hivyo imepoteza michezo nane na sare saba.

Baada ya kutamba msimu wa kwanza msimu uliofuata (2014/15) ikiamaliza nafasi ya nne wakati Yanga ikitwaa ubingwa na Mwambusi kuachia ngazi na kwenda kuibukia Yanga.

Msimu huu imekuwa na mwenendo mbaya kwani katika michezo 29 imeshinda michezo saba pekee na kuwaweka nafasi ya 12 ikiwa na alama 31 alama tano nyuma ya Polisi Tanzania inayokwepa kushuka daraja moja kwa moja.

City inashika nafasi ya pili kwa kuruhusu mabao mengi 43, huku Mtibwa Sugar ikiongoza kwa kufungwa mabao 44.

Tayari Mbeya City imetimua baadhi ya watu kwenye benchi lake la ufundi akiwemo kocha msaidizi, Anthony Mwamlima na kocha wa makipa, Ally Mustapha 'Barthez' na sasa kocha mkuu, Abdallah Mubiru ndiye aliyesalia.

kabla mchezo huu Mbeya City ilikuwa imepishana alama moja na KMC pamoja na Mtibwa Sugar ambazo zipo nafasi ya kucheza hatua ya mtoano na kama zitamaliza nafasi hizo na baadaye itakayofungwa itakutana na Mashujaa ambayo imeshinda michezo yake dhidi ya Pamba huko Ligi ya Championship.

Mchezo ujao wa kufungia msimu itacheza na KMC katika Uwanja wa Majimaji, Songea na kutoa taswira kamili juu ya timu hizo.

Kikosi kilichoanza katika mchezo wa leo upande wa Mbeya City ni Haroun Mandanda, Keneth Kunambi, Brown Mwankemwa, Juma Shemvuni, Abdulrazack Hamza, David Mwasa, Richardson Ng'ondya, Hassan Nassor, Tariq Seif, George Sangija na Sixtus Sabilo.

Upande wa Yanga alianza, Erick Johola, Kibwana Shomary, Bryson, Mamadou Doumbia, Zawad Mauya, Khalid Aucho, Denis Nkane, Farid Musa, Clement Mzize, Chrispin Ngushi na Ambundo Dickson.