Prime
Yanga yafuata kocha Sauzi, kuhusu Hamdi iko hivi!

Muktasari:
- Katika kumpata mbadala wa Hamdi, imeelezwa kuwa mabosi wa Yanga wametua Afrika Kusini kwa ajili ya kufanya mazungumzo na kocha Jose Luis Riveiro ambaye kwa sasa anaifundisha Orlando Pirates ya nchini humo.
WAKATI kukiwa na taarifa kwamba Yanga ina mpango wa kuwa na benchi jipya la ufundi kwa msimu ujao, taarifa zinadai kuwa mabosi wa timu hiyo wameshaanza harakati za kusaka mbadala wa Kocha Miloud Hamdi.
Katika kumpata mbadala wa Hamdi, imeelezwa kuwa mabosi wa Yanga wametua Afrika Kusini kwa ajili ya kufanya mazungumzo na kocha Jose Luis Riveiro ambaye kwa sasa anaifundisha Orlando Pirates ya nchini humo.
Kupitia Mwanaspoti, iliwahi kuripoti kuwa kocha Jose huu ni msimu wake wa mwisho ndani ya Orlando Pirates kwani tayari amewaambia mabosi wa timu hiyo hataongeza mkataba utakapofikia tamati Juni 30, mwaka huu.
Taarifa za ndani ya Yanga zinasema kuwa kuna mazungumzo yanafanyika kati ya uongozi wa timu hiyo na kocha huyo raia wa Hispania.
“Yanga inafanya mazungumzo na Kocha Jose wa Orlando Pirates ili aje kuwa kocha mkuu kwa msimu ujao.
“Kilichowavutia zaidi ni rekodi zake ikiwemo msimu huu kuifikisha Orlando Pirates nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa, lakini hata kwa upande wa ligi ya ndani anafanya vizuri,” kilisema chanzo hicho.
OFA ZAKE
Mbali na Yanga, pia kocha huyo ana ofa ya Saudi Arabia, huku pia akihusishwa na Al Ahly ambayo hivi karibuni iliachana na kocha Marcel Koller baada ya kushindwa kuifikisha timu hiyo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
“Kocha huyo ni kama ameshawishika na Yanga, kama mazungumzo hayo yataenda vizuri huenda akawa mrithi wa Miloud Hamdi,” kisema chanzo hicho.
Kocha Jose tangu ametua Orlando Pirates Julai 1, 2022, amefanikiwa kushinda mataji matatu ya Kombe la MTN na mawili ya Kombe la Nedbank huku msimu huu timu hiyo ikiishia nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikipoteza mbele ya Pyramids.
KUHUSU HAMDI
Yanga kwa sasa inaongozwa na kocha Miloud Hamdi ambaye ametua kikosini hapo Februari mwaka huu kuchukua nafasi ya Sead Ramovic.
Taarifa za ndani zinasema Yanga inataka kuachana na Hamdi kisha kupata kocha mwingine ambaye wanaamini ataipa mafanikio makubwa zaidi kwenye mashindano ya kimataifa msimu ujao.
“Yanga inataka kocha mwenye rekodi kubwa za hivi karibuni ndiyo maana kuna mchakato wa kumpata mrithi wa Hamdi mapema kabla ya kuanza msimu ujao,” kilifichua chanzo.
Tangu ameanza kuifundisha Yanga, Hamdi amesimamia mechi tisa za Ligi Kuu Bara akishinda nane na sare moja huku timu hiyo ikiwa kileleni mwa msimamo wa ligi na pointi 70 zikibaki mechi nne.
Pia hivi karibuni ameshinda Kombe la Muungano baada ya kuifunga JKU bao 1-0, huku akiifikisha Yanga nusu fainali ya Kombe la FA.