Prime
Yanga yaanza mkakati mpya

Muktasari:
- Ndio, mabosi hao katika kuimarisha kikosi kwa msimu ujao wa mashindano, wameanza mambo kwa kumnasa kiungo mshambuliaji anayejua boli ambaye wamempa mkataba wa miaka miwili.
YANGA inaendelea kujifua kwa ajili ya mechi tatu za kufungia msimu zikiwamo mbili za Ligi Kuu Bara na moja ya Kombe la Shirikisho, huku ikiipoteza Dabi ya Kariakoo lakini mabosi wa klabu hiyo wanaendelea kufanya mambo yao kimya kimya.
Ndio, mabosi hao katika kuimarisha kikosi kwa msimu ujao wa mashindano, wameanza mambo kwa kumnasa kiungo mshambuliaji anayejua boli ambaye wamempa mkataba wa miaka miwili.
Baada ya kuwepo kwa tetesi za muda mrefu Yanga kuhitaji huduma ya kiungo mshambuliaji wa Tabora United, Offen Chikola inadaiwa amemalizana na klabu hiyo kwa kupewa mkataba wa miaka miwili, ikiwa na maana msimu ujao ataonekana na uzi wa vijana wa Jangwani.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Yanga kinasema kuwa, Chikola aliyeitibulia watetezi hao wa Ligi Kuu kwa kufunga mabao mawili wakati wanaizamisha kwa mabao 3-1 katika mechi ya mkondo wa kwanza, ameshasaini mkataba huo wakatui anasubiri dirisha lifunguliwe atambulishwe.
Chanzo hicho kililiambia Mwanaspoti kuhusiana na usajili huo utakavyoongeza nguvu katika nafasi wanayocheza Maxi Nzengeli, Clement Mzize na Farid Mussa anayetajwa huenda akatolewa kwa mkopo kati ya Singida Black Stars na Mbeya City.
Katika msimu huu Chikola kafunga mabao saba, washindani wake wa namba ambao anakwenda kukutana nao Yanga, Maxi ana mabao matano, asisti tisa na Mzize ana mabao 13 na asisti tatu, hivyo ushindani utakuwa mgumu.
“Yanga ina mchakato wa kukifumua kikosi chake, kuna wachezaji ambao watapelekwa kwa mkopo kama Farid ndio maana Chikola anaingia, kuna wengine ambao wamemaliza mikataba yao kama kiwango chao hakikuisaidia timu watapewa mkono wa baibai,” kilisema chanzo hicho na kuongeza:
“Lakini wapo wachezaji waliomaliza mikataba bado wanahitajika na timu, hao tutakaa nao mezani kufanya mazungumzo ya kuwaongezea mipya na tayari tumefanya hivyo kwa baadhi yao kama Nzengeli na Dickson Job.”
Mwanaspoti lilifahamu kabla ya Yanga kukamilisha dili la Chikola, Simba na Azam zilikuwa zinafukuzia huduma yake.
Mbali na Chikola Mwanaspoti liliandika kuhusiana na Yanga kumalizana na kiungo mshambuliaji wa Azam FC, Gibril Sillah ambaye hadi sasa kafunga mabao tisa na ndoto yake ni kumaliza msimu huu akiwa na mabao 10.
Kabla ya kutua Tabora United msimu huu inayoshika nafasi ya tano kwa sasa, Chikola alishaitumikia Geita Gold kwa misimu miwili kabla ya kujiunga na Nyuki hao wa Tabora.