Yanga wajitoa Kagame, Serikali yanawa
Muktasari:
- Uongozi wa Yanga, ulikuwa unakutana jana Ijumaa usiku kujadiliana mambo mbalimbali ikiwa pamoja na ushiriki wao katika mashindano ya Kombe la Kagame, ingawa Mwanaspoti linatambua kuwa mabingwa hao hawatakwenda tena Sudan kutokana na hali tete ya usalama.
MABINGWA wa Kombe la Kagame, Yanga wapo katika hatua za mwisho za kujitoa katika michuano ya Kombe la Kagame, ambayo itafanyika Sudan kuanzia Juni 18 mwaka huu, huku Simba ikisikilizia kwanza.
Hata hivyo, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mkumbwa Ally amesema suala la Simba na Yanga kwenda nchini Sudan kushiriki mashindano ya Kagame lipo juu ya waandaaji wa michuano hiyo (Cecafa), mamlaka zinazosimamia mpira nchini (TFF) na klabu zenyewe.
Akizungumza na Mwanaspoti jana Ijumaa, Mkumbwa alisema kitu alichofanya Waziri wa wizara hiyo, Bernard Membe bungeni, ni kutoa hadhari juu ya hali ya usalama ilivyo nchini humo na siyo kuzikataza timu hizo kwenda kushiriki mashindano hayo.
“Alichofanya waziri ni kutoa tahadhari juu ya hali ya usalama, kwamba hakuna mazingira rafiki kwa michezo kutokana na hali ya usalama ilivyo pamoja na huduma nyingine,” alisema
“Baada ya hapo mamlaka zinazohusika kama TFF, waandaaji wa michuano hiyo na timu wanabaki na uamuzi wao, yeye waziri alitoa tu ushauri na ukipewa ushauri uamuzi wa mwisho ni wako,” alisema.
Uongozi wa Yanga, ulikuwa unakutana jana Ijumaa usiku kujadiliana mambo mbalimbali ikiwa pamoja na ushiriki wao katika mashindano ya Kombe la Kagame, ingawa Mwanaspoti linatambua kuwa mabingwa hao hawatakwenda tena Sudan kutokana na hali tete ya usalama.
Katika mahojiano yaliyochapishwa na Mwanaspoti Mei 25 mwaka huu, Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga alisema waliandika barua TFF ili kutaka ufafanuzi kabla ya kushiriki michuano hiyo ambayo yatafanyika katika mji wa Darfur Kaskazini.
Katika mahojiano hayo, Sanga alisema: “Tunataka kujiridhisha, kwa sababu hatutaki sisi kuwa sehemu ya kuleta amani wakati hatupo salama. Kwa hiyo ni kazi ya TFF kuwasiliana na Serikali ili kupata ufafanuzi.”
Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe akizungumza bungeni wiki iliyopita alisema mji wa Darfur si salama na watu wanaokwenda huko wamekuwa wakivaa mavazi maalumu yanayozuia risasi kupenya.
Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage alisema jana Ijumaa kutoka Dodoma kuwa wanasubiri kauli rasmi ya Serikali kupeleka timu Sudan.
“Cecafa waache kuangalia masilahi yao, sisi tulikwenda kucheza na Shandy katika mji huo hakuna hoteli, mimi nililala sebuleni kwenye hosteli, kwa hiyo sitashangaa kama Darfur hakuna hoteli kama alivyosema Waziri Membe bungeni,” alisema Rage.
Rage alisema Simba mara zote inaposafiri kwenda kucheza nje huwa inawasiliana na Wizara ya Mambo ya Nje pamoja na balozi kwa hiyo hawawezi kufanya lolote kwa kukurupuka tu bila kuishirikisha serikali.
Rage alishangaa kuwa kama Al Hilal na El Merreikh ambazo ni za Sudan zimejitoa itakuwaje kwa timu kutoka nchi nyingine ziende.
Mwenyekiti wa Cecafa, ambaye pia ni Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Leodegar Tenga alisema jana Ijumaa kuwa: “Si Cecafa wala TFF linapofika suala la usalama tukabishana na serikali, tunasubiri jibu la serikali.”