Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Siku saba za maajabu Dabi ya Kariakoo

Muktasari:

  • Hali hiyo imewafanya mashabiki wa soka nchini kubaki njiapanda kama Dabi ya Kariakoo itapigwa Juni 15 au la kutokana na msimamo huo wa Yanga ambao ndio wenyeji wa mechi hiyo.

DABI ya Kariakoo bado ina kipengele. Hakuna anayejua kama itapigwa au la hiyo Juni 15. Hii ni kwa sababu ya msimamo wa Yanga juu ya kuisusia mechi hiyo ambayo awali ilikuwa ipigwe Machi 8.

Hali hiyo imewafanya mashabiki wa soka nchini kubaki njiapanda kama Dabi ya Kariakoo itapigwa Juni 15 au la kutokana na msimamo huo wa Yanga ambao ndio wenyeji wa mechi hiyo.

Hata hivyo, wapo wengine wanaamini tisho la Yanga ni danganya toto, licha ya kujitokeza kwa wazee na matawi ya klabu hiyo kusisitiza msimamo wa kuisusa dabi na kwamba mechi itapigwa kama kawaida, kwa sababu Bodi ya Ligi imeshatoa msimamo, mechi ipo kama kawaida na itapigwa Kwa Mkapa.

Hata hivyo, siku hazigandi, kwa sasa imesaliwa na wiki moja tu kabla ya kufika siku ya mechi hiyo yaani Juni 15 na bado dabi inaionekana kuwa na kipengele cha kufanyika kwake.

Kwa namna hali ilivyo inaonyesha wazi ndani ya wiki kabla ya tarehe ya pambano hilo kuna maajabu ambayo yatajitokeza na kuweka historia kwa pambano hilo la watani wa jadi lililoahirishwa Machi 8 na Bodi ya Ligi baada ya Simba kulalamika kuzuiwa kufanya mazoezi ya mwisho siku moja.

Yanga inaona kama Bodi ya Ligi iliwabeba Simba kwani ilishatoa taarifa mwanzoni mechi hiyo ingechezwa kama ilivyokuwa imepangwa licha ya tishio la Simba ililolitoa mapema usiku wa kuamkia Machi 8, isingecheza mechi hiyo hadi wahusisha washughulikiwe.

Hata hivyo, mchana wa mechi hiyo iliyokuwa ipigwe saa 1:00 usiku kwa Mkapa, Bodi ya Ligi ilisema mechi imeahirishwa kwa sababu za viasharia vya hatarisho la usalama na matukio yaliyohitaji kufanyiwa uchunguzi, ila hadi wanaipanga tena Juni 15 haijawahi kutoa taarifa ya uchunguzi huo.

Kanuni kwa timu isiyoenda uwanjani kucheza mechi ya ligi, imeainisha adhabu itakayoikumba Yanga ikiwamo kupoteza mchezo kwa Simba, lakini ikikatwa pointi 15 kati ya ilizonazo kwa sasa na watetezi wa taji hilo, wamesisitiza wapo tayari kwa adhabu hiyo kama bodi inaona kuna ulazima wa kuihalalisha Dabi ipigwe Juni 15 kabla haijatoa majibu ya maswali ya hairisho na mchezo wa kwanza wa Machi 8.

Hapa chini ni baadhi ya maajabu yanayoweza kutokea ndani ya wiki moja kuhusu mchezo huo namba 184 na wa marudiano baina ya timu hizo baada ya awali Simba kupoteza kwa bao 1-0, Oktoba 19 mwaka jana baada ya beki Kelvin Kijili kujifunga dakika za lala salama na kuipa Yanga ushindi uliokuwa wa nne mfulizo mbele ya watani wao hao.


KAMBI YA MAANDALIZI

Simba imeanza kambi kwa ajili ya mchezo huo, ilihali Yanga yenyewe nayo inajifua kwenye Uwanja wa KMC kujiandaa kwa mechi tatu zilizosalia kwao ikiiondoa hiyo ya dabi.

Hii ina maana Simba inajifua kwa ajili ya mchezo ambao bado hakuna uhakika kama utapigwa hiyo Juni 15 na hili ni ajabu kwa timu kujiandaa kwa mechi ‘hewa’.

Kadhalika Yanga ambao ndio wenyeji wa mechi hiyo, haifanyi promo kuhusu  mchezo huo na wala kujishughulisha na mandalizi yake kitu ambacho hakijawahi kutokea katika historia ya dabi, kwa vile tayari kocha mkuu, Miloud Hamdi amenukuliwa ratiba ilivyo kwa sasa ni kwa mechi mbili za Ligi Kuu dhidi ya Tanzania Prisons na Dodoma Jiji na fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) dhidi ya Singida BS.

Kifupi ni kwamba kwa Hamdi ishu ya dabi wala haipo na hana mpango nayo, ikiwa ni ajabu katika historia ya dabi, kwa timu kujiandaa na maandalizi ya mechi, lakini haishughuliki na mchezo uliopo mbele yao isipokuwa wa mbele zaidi.


PROMO YA AZAM

Hii ni wiki ngumu kwa Azam Media ambao ndio wadhamini wa Ligi Kuu kwa upande wa matangazo ya maudhui kwani wanaitangaza mechi, lakini bado wanapata ugumu kutokana na mashabiki kuwa njia panda wa kutojua kama mechi ipo au haipo kwa msimamo wa Yanga.

Wadhamini hao watazikutumia siku saba zilizobaki kuendelea kupiga promo, lakini ule muitikio uliozoeleka kunapokuwa na pambano la watani, huenda usiwe kiviiile, jambo ambalo linaweza pia kuwatia hasara kwa upande flani tofauti na dabi zilizopita ambapo mambo yalikuwa ni moto.

Sio kwa Azam tu, hata wamiliki wa vibanda umiza ambao kipindi cha dabi wanasikilizia promo ya mechi hiyo kutaka kujua itapigwa au la hili wajipange kwa kuhofia isije ikala kwao kama ilivyotokea Machi 8 mechi ilipoahirishwa na hili ni ajabu jingine la dabi kwa msimu huu.


MAAJABU YA BODI

Bodi inayosisitiza mechi hiyo ipo kama ilivyopangwa, inasubiriwa kuona ndani ya wiki hii ikiendelea na maandalizi ya pambano hilo bila kushirikiana na wenyeji wa mchezo yaani Yanga.

Ndani ya wiki bodi italazimika kutangaza taratibu za mchezo huo kwa mashabiki kwa maana wataingiaji na kama tiketi zitaanza kuuzwa wapi, ukiachana na zile ambazo mashabiki walizinunua kwa mechi ya Machi 8.

Pia itatangaza waamuzi watakaoiochezesha mechi hiyo ambao nao wataanza maandalizi kabla ya kushuka uwanjani siku ya Juni 15.

Bodi italazimika kuitisha mkutano wa kabla ya mechi (pre match meeting) ili kujadili walipofikia na kujua timu zitavaa uzi upi na mengine yanayohusiana na mchezo huo na bila ya shaka kwa msimamo wa Yanga watakaohudhuria ni Simba, waamuzi, watu wa bodi pekee na mamlaka zinazohusu mchezo huo wakiwamo mamlaka ya uwanja, huduma ya kwanza na wengineo tu.

Hapa itakuwa ni maajabu ya kufanyika kikao na maandalizi ya mechi kwa kuhusisha timu moja tu, lakini ikiwa bado haijafahamika kama itapigwa au la!


MASHABIKI UWANJANI

Licha ya kwamba Yanga imeshasisitiza wanayanga hawapaswi kushughulika kwa mechi hiyo, lakini ni wazi kwa wenzao wa Simba mechi wanaitaka na inaweza kushuhudiwa watakaoenda uwanjani siku ya Juni 15 wakawa ni wale wa Msimbazi.

Hata hivyo, idadi yao inategemea na ukweli kama tiketi walizokata kwa ajili ya mechi ya Machi 8 bado wanazo ili kuwaruhusu kwenda Kwa Mkapa, kwani hadi sasa hakuna mauzo ya tiketi za mechi hiyo kutokana na Yanga kukauka kama sio wenyeji wa pambano.

Maana yake itakuwa ni maajabu kwa mara ya kwanza Dabi kuhudhuruiwa na mashabiki wa upande mmoja na pengine hata idadi yao iwe ndogo kulinganisha na mechi nyingine na watani hao wa soka.


SIMBA PEKEE YAO

Kwa hali ilivyo ni wazi kama kweli mechi itapigwa Juni 15, wanaoweza kujitokeza uwanjani siku hiyo ni kikosi cha Wekundu wa Msimbazi tu, kama itakavyokuwa kwa mashabiki na wapenzi wao.

Hii itakuwa na maana msafara wa kikosi cha Simba utawahi uwanjani na kuanza maandalizi ya kukagua uwanjani, kisha kuruhusuiwa kwenda vyumbani kubadilisha nguo kabla ya kuitwa na marefa tayari kujiandaa na mtangane huo, lakini wakiwa pekee yao bila watani wao Yanga kama watashikilia msimamo wa kutoicheza mechi hiyo.

Bila ya shaka Simba watakuwa uwanjani na Simba wenzao na kushangiliwa na Wanamsimbazi kabla ya timu kuitwa na uamuzi ili kukaguliwa. Hilo litakuwa ni ajabu jingine la Dabi kwa msimu huu.


WAAMUZI UWANJANI

Kwa vile Bodi ya Ligi itakuwa imeshawatangaza waamuzi, ni wazi Juni 15 watatinga uwanjani kwa ajili ya kusimamia mchezo huo na huenda wakakutana na Simba tu watakaojitokeza kwa pambano hilo.

Waamuzi hao watakuwa na kazi ya kuiita Simba na kuikagua kisha kusubiri kwa muda wa dakika 30 na pale watakaoshindwa kuiona Yanga uwanjani, basi watapuliza filimbi kuashiria mechi imeisha na Simba kupewa ushindi wa mabao 3-0.

Ripoti ya waamuzi itawasilishwa kwenye Kamati ya Kuendesha na Usimamizi wa Ligi ambayo itarudi katika kanuni na kuwajibika kuikata Yanga pointi 15, kwa vile Yanga inazo 73 kwa sasa kupitia mechi 27, itasaliwa na 58 na kuishuka kutoka nafasi ya kwanza hadi ya pili, kuipisha Simba itakayofikisha pointi 75, kwa vile kwa sasa ina 72 kupitia pia mechi 27.


SIMBA BINGWA

Maamuzi ya kuzingatia Sura ya Tano: Mchezo kanuni ya 17 kifungua namba 44 kinachoeleza adhabu kwa timu isiyoenda uwanjani ikieleza inapoteza mechi kwa pointi tatu na mabao matatu ni wazi Simba itakuwa ndiyo bingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu.

Ndiyo Simba itangazwa kuwa bingwa mpya wa Ligi Kuu kwani kabla hata mechi za raundi mbili za mwisho zilizopangwa kupigwa Juni 18 na Juni 22 hazijachezwa, tayari Simba itakuwa na pointi ambazo hakuna timu itakayoweza kuzifikia ikiwamo Yanga hata kama itashinda mechi zilizobaki.

Yanga ikishinda mechi mbili za mwisho dhidi ya Tanzania Prisons na Dodoma Jiji itafikisha pointi 64 ambazo hata kama Simba itapoteza mechi mbili za mwisho dhidi ya KenGold na Kagera Sugar zilizoshuka daraja mapema, haitaizuia kubeba ubingwa huo iliyoukosa misimu mitatu mfululizo.

Hilo nalo litakuwa ni ajabu jingine la Simba kutoka kuusotea ubingwa tangu ilipoutwaa mara ya mwisho Julai 11, 2021 pale ilipoifunga Coastal Union kwa mabao 2-0, huku ikiwa na mechi mbili mkononi.