Yanga: Tunaitaka Simba tu fainali

Unguja. Yanga imefuzu hatua ya fainali ya Kombe la Mapinduzi zitakazofanyika keshokutwa Jumatano Januari 13 kwenye Uwanja wa Amaan kisiwani hapa lakini wamesema kiu yao ni kukutana na Simba tu.

Simba wanasubiri mchezo wa nusu fainali ya pili itakayoanza saa 2:15 usiku wa leo Jumatatu dhidi ya Namungo ambapo mshindi ndiye atakayecheza na Yanga.

Yanga wamefuzu fainali hizo baada ya kuifunga Azam kwa mikwaju ya penati 5-4 baada ya dakika 90 kutoka sare ya bao 1-1.

Akizungumza na Mwanaspoti Online, Makamu Mwenyekiti wa klabu ya Yanga, Fredrick Mwakalebela amesema kuwa walikuja huku wakiwa na lengo la kutwaa ubingwa na kwamba wanaamini watabeba ubingwa huo ulioachwa na Mtibwa Sugar.

Amesema kuwa yeyote atajayepita kati ya Simba au Namungo watakuwa tayari kucheza nao lakini shauku kubwa ni kucheza na watani zao na ndicho kilichopelekea washangilie kwa nguvu kuona wanafuzu hatua hiyo.

"Unadhani kwanini tumefurahi, lengo lilikuwa ni kufuzu fainali hilo moja, pili ni kutwaa ubingwa na ubingwa utanoga zaidi tukicheza na Simba, tunataka tuwaonyeshe kuwa tuna uwezo wa kumfunga Simba.

"Hata asipopita basi Namungo naye ajiandae ingawa sio lengo letu kubwa kama tunavyotaka kukutana na Simba na njia pekee ya wao kutocheza na sisi ni kufungwa," ametamba Mwakalebela