Yanga, Simba ni moto chini

Wachezaji wa Yanga wakifanya mazoezi kwenye Uwanja wa Bora uliopo Kijitonyama jijini Dar es Salaam jana Jumatatu.
Picha na Michael Matemanga.
Muktasari:
- Tathmini ya kiufundi inaonyesha Yanga imesajili vizuri kwenye idara nyingi uwanjani zaidi ya Simba ambayo imechukua wachezaji wengi vijana na kununua mastaa wachache, ingawa vijana wake ni machachari kwenye kiungo.
KIPINDI cha kwanza cha uhamisho na usajili wa wachezaji wa Ligi Kuu Bara msimu ujao kinakamilika kesho Jumatano saa 6.00 usiku.
Simba imefumua kikosi chake, huku Yanga ikaifanya marekebisho kidogo lakini imeipiga bao Simba kwenye idara nyingi uwanjani.
Simba na Yanga zimemaliza usajili wao kwa asilimia kubwa na mashabiki wao kila mmoja anasubiri kuona timu hizo ambazo ni wapinzani wakubwa watakachofanya kwenye Ligi Kuu Bara msimu ujao huku Yanga ikiwa ni bingwa mtetezi inayojiandaa na Ligi ya Mabingwa Afrika.
Tathmini ya kiufundi inaonyesha Yanga imesajili vizuri kwenye idara nyingi uwanjani zaidi ya Simba ambayo imechukua wachezaji wengi vijana na kununua mastaa wachache, ingawa vijana wake ni machachari kwenye kiungo.
Makipa
Yanga ina makipa; Ali Mustapha’ Barthez’ na Deogratius Munishi ‘Dida’ ambao ni wazoefu kwa kiasi chake ingawa kitakwimu hawamfikii Abel Dhaira wa Simba ambaye ni raia wa Uganda atakayesaidiana na Andrew Ntalla. Ntalla hana uzoefu wowote kwenye michuano mikubwa, lakini ameonyesha kipaji cha aina yake.
Mabeki
Simba imemchukua Joseph Owino wa URA ya Uganda na beki wa Vital’O ya Burundi, Kaze Gilbert (wanasajili wiki hii) ambao inaamini kwamba wakishirikiana na wazalendo kama Nassor Masoud, Shomari Kapombe, Issa Rashid ‘Baba Ubaya’, Haruna Shamte, Rahim Juma na Hassan Khatib mambo yataenda.
Bosi wa Kamati ya Usajili wa Simba, Zakaria Hanspoppe alitamka kwamba: “Tumeshamaliza tatizo sugu lililokuwa linatukabili kwenye safu ya ulinzi baada ya kumpata Owino (Joseph) na yule beki wa Vitalo (Kaze Gilbert) ni wachezaji ambao tumewafuatilia kwa karibu na kujiridhisha nao.”
Yanga, beki yake ambayo haijabadilishwa na ambayo haipitiki kirahisi inaongozwa na Kelvin Yondan’ Vidic’, Nadir Haroub ‘Cannavaro, Rajab Zahir, Mbuyu Twite, Juma Abdul, David Luhende na Oscar Joshua.
Viungo
Hapa zote zimesheheni ingawa kwa viwango tofauti. Timu zote zina wachezaji wazuri na wazoefu wa nafasi hii ingawa wa Yanga wameizidi Simba kwa uzoefu, viungo mahiri wakabaji na hata wachezeshaji wakati Simba ina viungo wachezeshaji kuliko wakabaji.
Yanga ina viungo wakabaji; Athuman Iddi ‘Chuji’, Frank Domayo na Salum Telela huku Haruna Niyonzima ‘Fabregas’ na Hamis Thabit wakicheza kama viungo wachezeshaji na wakati mwingine Domayo hucheza kama kiungo mchezeshaji pia wakati Simba ina Jonas Mkude na Wiliam Gallas, wanaocheza kama viungo wakabaji na wachezeshaji ni Ramadhan Chombo ‘Redondo’, Mwinyi Kazimoto, Amri Kiemba, Abdallah Seseme na Abdulhalim Humoud ambaye hata hivyo bado usajili wake haujakamilika.
Mawinga
Katika nafasi hii uzoefu pekee ndio utakaowabeba Yanga kuliko Simba ambayo wachezaji wake wengi ni machachari. Winga zote za Yanga na Simba zina kasi ingawa Yanga winga zake zina uzoefu kuanzia ligi za ndani na hata kimataifa.
Yanga wana mawinga Mrisho Ngassa, Simon Msuva na Abdallah Mguhi lakini Wekundu hao wa Msimbazi wana winga hatari pia ambazo ni Edward Christopher, Haruna Chanongo, Marcel Kaheza, Ramadhan Singano ‘Messi’ na Ibrahim Twaha’Messi’.
Mastraika
Simba ina washambuliaji Zahoro Pazi, Sino Agustino na Betram Mombeki, lakini hata hivyo Hanspoppe amethibitisha kwamba wataongeza straika mmoja kabla dirisha halijafungwa.
Yanga ina washambuliaji watano mpaka sasa ambao ni Jerrson Tegete, Didier Kavumbagu, Shaban Kondo, Said Bahanuzi, Hussein Javu na endapo itamalizana na Hamis Kiiza watakaouwa sita na habari za ndani zinasema kamati ya usajili inawinda straika mwingine mmoja.
Kwa ulinganisho wa vikosi hivyo viwili Yanga imeizidi kete Simba kwa kiasi fulani na huenda ikawa na kikosi cha kwanza imara zaidi wakati Simba italazimika kuvuta subira wachezaji wake wapate uzoefu zaidi na kucheza soka la kuvutia.
Kocha wa Simba, Abdallah Kibadeni aliliambia Mwanaspoti kuwa majibu yatapatikana uwanjani na watu wasubiri kuona na si kuwahukumu kwa hisia. Kocha huyo amethibitisha kusajili wachezaji 26 wazalendo ambao anaamini kwamba wana ubora wa kubeba heshima ya Simba na kuwapa ubingwa msimu ujao.
“Watu wanasema kuwa hatutafanya vizuri lakini ni mapema mno kusema hivyo kwani ligi bado haijaanza, tukianza ligi ndio tutajua mbivu na mbichi,” alisema Kibadeni ambaye ndiye kocha bora wa msimu uliopita.
Kocha Msaidizi wa Yanga, Fred Felix Minziro alisema kuwa anaamini kwamba Simba haijiamini kutokana na aina ya timu waliyonayo na wala haitamani kukutana na Yanga.
Maoni ya makocha wengine
Makocha wazalendo Joseph Kanakamfumu na Kennedy Mwaisabula wameipa nafasi kubwa Yanga kufanya vizuri msimu ujao kutokana na kikosi chao kizuri tofauti na Simba ambayo inajengwa upya.
“ Yanga wana wachezaji wazoefu na wazuri halafu kikosi chao hakijabadilika bali wameongeza tu baadhi ya watu kuziba mapengo na pia hata ukiangalia kwenye ushambuliaji ndio wamejaza watu wengi hiyo itaongeza ushindani sana na watafunga sana tofauti na Simba ambao wanaijenga timu yao, ukiangalia hata usajili wao ni wa kawaida hivyo wasitarajie kupata mafanikio msimu ujao na hata ule mwingine, itawachukua muda kulingana na kikosi walichonacho,” alisema Kanakamfumu.
“Yanga timu yao haijabadilika na wana wachezaji ambao ni wazuri tofauti na Simba ambao wana kazi ya kutengeneza kikosi chao na wasitarajie kutisha msimu ujao na hata matokeo yoyote kwao hayatawaathiri kwa sababu wanatengeneza kikosi lakini Yanga wana timu imara hivyo wakipata matokeo mabaya msimu ujao lazima watu wahoji,” alisema Mwaisabula.