Simba, Yanga mmesikia huko? Sillah aaga Azam!

Muktasari:
- Mgambia huyo aliyeitumikia Azam kwa misimu miwili, anamaliza mkataba alionao akiwa ameifungia klabu hiyo mabao 19, yakiwamo 11 ya msimu huu na manane ya msimu uliopita.
KIUNGO mshambuliaji wa Azam FC, Gibrill Sillah amewaaga mashabiki na uongozi wa timu hiyo leo kupitia ukurasa wake wa Instagram.
Mgambia huyo aliyeitumikia Azam kwa misimu miwili, anamaliza mkataba alionao akiwa ameifungia klabu hiyo mabao 19, yakiwamo 11 ya msimu huu na manane ya msimu uliopita.
Sillah anayeondoka akiwa ndiye kinara wa mabao kwa msimu huu wa kikosi hicho ameandika kuwa; ”Asante Azam kwa kila kitu ambacho mmenifanyia katika kipindi cha miaka hii miwili.
“Ni ngumu kwangu kuiaga klabu ambayo nina kumbukumbu nayo nzuri na mbaya na kwa kweli nitawakumbuka daima katika safari yangu ya soka.
“Naitakia mafanikio mema msimu ujao, lakini nawashukuru wachezaji wenzangu na wafanyakazi wa Azam."
Kupitia Mwanaspoti iliandika kuwa; kiungo huyo ameziweka vitani Simba na Yanga ambazo zinawania saini yake.
Licha ya timu hizo kutajwa kumwania, lakini kiungo huyo ameonyesha kutokuwa na hesabu za kusalia nchini, baada ya kuandika kuwa;
“Maisha yangu ndani ya klabu yalikuwa mepesi, nitalikumbuka soka la Tanzania na nchi kwa ujumla kwa sababu kila mtu anapenda mpira ni kama unacheza Ulaya kutokana na vaibu la mashabiki, Azam itaendelea kubaki ndani ya moyo wangu,” alimaliza hivyo.
Hata hivyo Azam ilipambana kubakiza lakini winga huyo hakukubali, licha ya kuwa na kiwango bora msimu huu Yanga ilihusishwa kuinyatia saini yake ili kuitumikia kwa msimu ujao, japo haikuwahi kuthibitishwa.