Yanga, Simba hakuna mbabe

Yanga, Simba hakuna mbabe

Muktasari:

  • Dakika 90 zimetamatika mchezo baina ya Yanga dhidi ya Simba kwa suluhu ya bila kufungana kwenye mechi ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Dakika 90 zimetamatika mchezo baina ya Yanga dhidi ya Simba kwa suluhu ya bila kufungana kwenye mechi ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Yanga wao walianza kwa kucheza pasi chache na kushambulia kwa haraka kwani kuna nyakati walipiga pasi tatu au nne wanafika langoni mwa Simba kwa kutengeneza shambulizi.

Yanga walionekana kufanikuwa kwenye kuzuia kwani langoni kwao hakukuwa na mashambulizi ya hatari kutoka kwa nyota wa Simba.

Simba walicheza mfumo wa pasi fupi fupi na kutokushambulia kwa haraka kama ilivyo kwa wapinzani wao.

Wachezaji wa Simba walionekana kucheza kwa pole pole na utulivu mkubwa ndani yake bila ya kupoteza mipira mingi.

Hawakufika langoni kwa Yanga mara kwa mara na hata aina yao ya mashambulizi hayakuwa ya kutosha kiasi kwamba hawajakosa nafasi ya wazi zaidi ya kufunga bao.

Mwamnyeto, Job
Mabeki wa kati wa Yanga, Bakari Mwamnyeto na Dickson Job walifanikiwa kwa kiasi kikubwa kucheza kwa nidhamu na maelewano ndani yake.

Uimara huo aa mabeki wa Yanga, uliwafanya kuwazuia vizuri washambuliaji wa Simba, Benard Morrison, Pape Sakho, Clatous Chama na Chris Mugalu.


Onyango, Inonga
Ushandani mwingine ulikuwa kwenye lango la Simba kati ya mabeki wao wa kati Joash Onyango na Inonga Baka dhidi ya Fiston Mayele.

Inonga na Mayele waliokuwa na kazi kubwa ya kuhakikisha Mayele wala hatetemi walifanikiwa kumzui kwa kiasi kikubwa na kila mmoja alifanya kazi hiyo ipasavyo.

Mayele kuna nyakati alipokea mpira ila alikutana na ushindani wa kutosha kutoka kwa Inonga na Onyango waliweza kumzuia.

Hapakuwa na shambulio la hatari zaidi ambalo Mayele alifanya na pengine ingekuwa nafasi rahisi kwake kufunga bao kutokana na uimara wa mabeki hao wa kati wa Simba.

Fei, Chama
Katikati mwa kuwanja kulikuwa na ushindani mwingine kati ya kiungo wa Yanga, Feisal Salum na Clatous Chama wa Simba.

Kila mmoja kwa nafasi yake alikuwa anasumbua Chama alionyesha ubunifu pindi alipokuwa na mpira mguuni kwake haswa nyakati Simba walikuwa wanashambulia.

Fei nae wala hakuwa nyuma alionyesha ubunifu alipokuwa na mpira pamoja na kupiga pasi za kuanzisha mashambulizi na nyakati nyingine alishuka chini kukaba na kuzuia mashambulizi ya Simba.

Mpaka mapumziko hakuna timu iliyofanikiwa kupata bao.

Kipindi cha pili Simba walirejea na mabadiliko wakimtoa Chama nafasi yake ikichukuliwa na Mzambia mwenzake Rally Bwalya.

Yanga walipoteza nafasi nzuri dakika ya 50 krosi nzuri ya Djuma inakosa mmaliziaji akigongeana vizuri na Moloko.

Dakika ya 55 Simba wanapata pigo kiungo wake Sadio Kanoute aliyeumia dakika ya 48 anashindwa kuendelea nafasi yake ikichukuliwa na Mzamiru Yassin huku pia wakimtoa Morrison nafasi yake ikichukuliwa na Kibu Denis.

Mwamuzi Ramadhan Kayoko dakika ya 63 alitumia busara akisimamisha mchezo kupisha wachezaji ambao walikuwa katika ibada ya mfungo wa Ramadhan kufungua akiwapa dakika moja.

Dakika tatu baadaye Yanga walimtoa Moloko nafasi yake ikichukuliwa na Denis Nkane.

Mayele dakika ya 71 anapoteza nafasi shuti lake kali linatoka upande wa pembeni akipokea krosi ndefu ya Saido.

Simba dakika ya 74 wanapoteza nafasi kichwa cha Mugalu akiruka vizuri bila kusumbuliwa kidakwa kirahisi na Diarra.

Yanga walipoteza nafasi nzuri dakika ya 75 krosi ya Aucho inapanguliwa kwa kichwa na mabeki wa Simba kisha mpira kumkuta Nkane lakini krosi yake inakosa mmaliziaji Simba wanaokoa.

Yanga walifanya mabadiliko ya pili wakimtoa Feisal nafasi yake ikichukuliwa na Farid Mussa.

Dakika ya 89 timu zote zinafanya mabadiliko Yanga wakimtoa Saido nafasi yake ikichukuliwa na Salum Aboubakar huku Simba nao wakimtoa Sakho nafasi yake ikichukuliwa na nahodha wao mkuu mshambuliaji John Bocco.


Vikosi vilivyoanza kwenye mchezo wa leo;

Yanga

Djigui Diarra, Djuma Shaban, Kibwana Shomari, Dickson Job, Bakari Mwamnyeto, Yannick Bangala, Khalid Aucho, Jesus Moloko/Nkane, Feisal Salum/Farid, Fiston Mayele, Said Ntibazonkiza


Simba

Aishi Manula, Shomari Kapombe, Mohamed Hussein, Henock Enonga, Joash Onyango, Jonas Mkude, Sadio Kanoute, Pape Sakho, Clatous Chama/Bwalya, Chris Mugalu, Bernard Morrison/Kibu.