Yanga kuwakosa hawa dhidi ya JKT Tanzania

Muktasari:
Wachezaji hao muhimu wataukosa mchezo wa kesho Jumatano, utakaochezwa uwanja wa Jamhuri Jijini hapa.
Dodoma. LICHA ya kocha wa makipa wa Yanga, Razack Siwa, kutotaka kutaja majina ya wachezaji watakaowakosa kwenye mchezo wa kesho, Yanga itakosa huduma ya baadhi ya mastaa wake.
Mwenyekiti wa kamati ya ufundi wa Yanga, Dominick Albinus, amesema wataendelea kukosa huduma ya mabeki wao muhimu Lamine Moro na Abdallah Shaibu 'Ninja'.
"Kuhusu Lamine hayupo kwenye msafara wa timu yetu mchezo huu, amebaki pamoja na Ninja naye hatuko naye hivyo hawatakuwepo kwenye mchezo huu muhimu" amesema Albinus.
Hata hivyo, Mwenyekiti huyo wa ufundi ametbibitisha kiungo wao Mukoko Tonombe, atakuwepo kwenye mchezo huo kufuatia kukosekana mchezo uliopita.
Yanga imetarajiwa kufanya mazoezi yake ya mwisho leo jioni kwenye uwanja wa Jamhuri kuelekea mchezo huo muhimu kwa kila timu.
Yanga ina alama 58, ikiendelea kusaka ushindi ili kufukuzana na Simba inayoongoza kwa alama 61, wakati maafande JKT wao wana alama 33 katika nafasi ya 13.
Imeandikwa na Matereka Jalilu