Yanga kiburi sana

Muktasari:
Kocha Marcio Maximo ameangalia mazoezi ya timu yake akarudia na mechi ya Morogoro dhidi ya Mtibwa Sugar (Yanga walifungwa mabao 2-0) akasema msinitanie lazima kikosi kibadilike na pointi tatu dhidi ya Prisons kesho Jumapili zipatikane.
LIGI Kuu Bara inaingia katika mechi zake za pili leo Jumamosi na kesho Jumapili lakini imebainika kwamba Yanga kiburi sana.
Kocha Marcio Maximo ameangalia mazoezi ya timu yake akarudia na mechi ya Morogoro dhidi ya Mtibwa Sugar (Yanga walifungwa mabao 2-0) akasema msinitanie lazima kikosi kibadilike na pointi tatu dhidi ya Prisons kesho Jumapili zipatikane.
Amebadilisha kiungo kwa kumwingiza Andrey Coutinho na beki ya kushoto amefumba macho kwa kumwanzisha kwa mara ya kwanza Edward Charles ambaye amesajiliwa akitokea JKT Ruvu. Coutinho ambaye alikuwa majeruhi anachukua nafasi ya Hamis Kiiza anayerudi benchi huku Charles akichukua namba ya Oscar Joshua ambaye ameumia.
Hiyo inamaanisha kwamba beki ya Yanga itasimamiwa na Juma Abdul, Edward Charles, Kelvin Yondani na Nadir Haroub ‘Cannavaro’, viungo watakuwa ni Mbuyu Twite, Haruna Niyonzima na Hassan Dilunga wakati mbele yao watakuwepo Mrisho Ngassa, Genilson Santos ‘Jaja’ na Coutinho.
Ngassa alikuwa akicheza zaidi winga lakini sasa Maximo amepanga kumtumia kama straika wa katikati ili kulazimisha ushindi kwa kuwachosha mabeki. Msaidizi wa Maximo, Leonardo Neiva alisema,“ Tumefanya mabadiliko hayo baada ya kuona kuwa Jaja anaweza kucheza vizuri zaidi akiwa pembeni na karibu ya Ngassa hivyo tunatumia ujanja wa Ngassa kuhakikisha tunapata kitu.”
Lakini Maximo amefanya kiburi cha kitaalamu kwa kuwarudisha benchi Simon Msuva (pichani) na Kiiza.
“Msuva atasubiri kwa Coutinho na Kiiza kwa Niyonzima.
Tunaangalia zaidi jinsi tutakavyofunga mabao mengi, pia jinsi timu itakavyokuwa ikishambulia,kupata ushindi wa kwanza,” alisema Neiva.
Ndanda tayari imejikita kileleni mwa ligi hiyo baada ya kuiangamiza Stand United mabao 4-1 wikiendi iliyopita wakati Yanga wako katika nafasi ya 13 kwenye msimamo wa ligi hiyo inayoshirikisha timu 14.
Simba Vs Polisi Morogoro
Leo Jumamosi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Simba itacheza na Polisi Moro, Simba inaingia katika mchezo huo ikiwa na kumbukumbu ya sare ya mabao 2-2 dhidi ya Coastal Union wikiendi iliyopita wakati Polisi wataingia wakiwa na kumbukumbu ya kupoteza mabao 3-1 kwa mabingwa watetezi Azam.
Kocha wa Simba, Mzambia Patrick Phiri alisema, “Tumekuwa kambini Zanzibar kwa wiki nzima, tumefanya mazoezi magumu hususan katika safu ya ulinzi ambayo ilituangusha kidogo kwenye mchezo uliopita.
“Licha ya kwamba nitawakosa wachezaji watano bado nina kikosi cha ushindani ambacho kinaweza kunipatia matokeo mazuri, ni changamoto kwangu na wachezaji, kwani nitalazimika kupanga kikosi upya ili kuhakikisha tunashinda na hata wachezaji kama kipa Peter Manyika na Hussein Sharif ‘Casillas’ ambao watawania namba badala ya Ivo,” alisema Phiri ambaye amewatoa hofu wana Simba kuhusiana na mchezo huo.
Simba itawakosa kipa Ivo Mapunda, mabeki Adam Miraji, Issah Rashid ‘Baba Ubaya’, Abdi Banda na mshambuliaji Raphael Kiongera ambao wote ni majeruhi.
Kocha wa Polisi Morogoro Mohammed Rishaard Adolf alisema: “Tulipoteza kwa Azam lakini tumejipanga kufanya vizuri kwenye mechi ya Simba, tumeandaa kikosi kizuri na tuna imani mchezo utakuwa mzuri.”
Azam Vs Ruvu Shooting
Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Azam FC leo Jumamosi watacheza na Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi nje kidogo ya Dar es Salaam. Azam inaingia katika mchezo huo ikiwa na kumbukumbu ya ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Polisi Morogoro wikiendi iliyopita wakati Ruvu Shooting wakiingia na kumbukumbu ya kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Prisons.
Msemaji wa Ruvu Shooting, Masau Bwire alisema; “Tunatambua kuwa Azam ina rekodi nzuri ya kutopoteza michezo ya nyumbani lakini watambue kuwa rekodi hazidumu milele na sisi tumejipanga vizuri kuhakikisha tunapata ushindi wetu wa kwanza msimu huu.”
Mbeya City Vs Coastal Union
Kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya, kikosi cha Mbeya City kitaingia vitani kupambana na Coastal Union ya Tanga. Timu zote mbili zinaingia uwanjani zikiwa bado hazijaonja ushindi wa kwanza wa ligi. Mbeya City ilitoka sare tasa na JKT Ruvu wikiendi iliyopita wakati Coastal walipata sare ya mabao 2-2 ugenini dhidi ya Simba.
Kocha Msaidizi wa Mbeya City, Suleman Jabir alisema : “Tutamkosa mchezaji mmoja tu ambaye ni Erick Mawala lakini Deogratius Julius na Steven Mazanda wanaendelea vizuri. Tumejiandaa vizuri pamoja na kuwajenga wachezaji kisaikolojia kwani mchezo wa kwanza tulitoka sare.”
Kocha wa Coastal Union, Yusuf Chippo alisisitiza watacheza kwa tahadhari kubwa licha ya kutotaka kufunua mbinu zake.
Mgambo JKT Vs Stand United
Maafande wa Mgambo JKT, watakuwa wenyeji wa Stand United kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga. Mgambo inaingia kwenye mchezo huo ikiwa na kumbukumbu ya ushindi wa bao 1-0 mbele ya Kagera Sugar wikiendi iliyopita wakati Stand United wako mkiani mwa ligi na wanaingia kwenye mchezo huo wakiwa na kumbukumbu ya kipigo cha mabao 4-1 kutoka kwa Ndanda. Timu hiyo ya Shinyanga tayari imeanza kuzua hofu kama kweli itaweza kuibuka kidedea mbele ya Mgambo inayonolewa na Bakari Shime.
Mtibwa Vs Ndanda
Leo Jumamosi Mtibwa Sugar pia itakuwa kwenye uwanja wake wa nyumbani wa Manungu huko Turiani, Morogoro kuwakaribisha vinara wa ligi hiyo Ndanda FC ya mkoani Mtwara. Ndanda inacheza ligi kwa mara ya kwanza iko kileleni mwa msimamo baada ya ushindi wao wa mabao 4-1 dhidi ya Stand United ugenini Mjini Shinyanga.
Mtibwa nayo inaingia katika mchezo huo ikiwa na kumbukumbu ya ushindi wa mabao 2-0 mbele ya Yanga wikiendi iliyopita, mchezo huo ulichezwa Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.
JKT Ruvu na Kagera Sugar
Maafande wa JKT Ruvu watakuwa kwenye uwanja wa Azam Complex, Chamazi Jumapili kuwakaribisha Kagera Sugar. Ruvu inaingia uwanjani ikiwa na pointi moja baada ya kutoka sare na Mbeya City wikiendi iliyopita wakati Kagera wanaingia uwanjani baada ya kufungwa bao 1-0 na Mgambo JKT ya Tanga.
Kocha wa JKT Ruvu, Felix Minziro alisema:“Kikosi changu kipo tayari kwa mapambano, nimefanya kazi kubwa na safu ya ushambuliaji ili waweze kufunga mabao kuiwezesha timu kupata matokeo.”
Kocha wa Kagera Sugar, Jackson Mayanja alisema: “Licha ya kwamba tulipoteza mchezo wa kwanza si kwamba tutaingia uwanjani vichwa chini, tutapambana kuhakikisha tunapata matokeo.”