Prisons: Fountain? Hawa mbona tunao!

Muktasari:
- Prisons ililazimisha sare hiyo ugenini kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, mjini Babati Manyara baada ya wenyeji kutangulia kwa bao la kipindi cha kwanza kupitia Edger William kabla ya Oscar Mwajanga kuchomoa kipindi cha pili na ssa wanasikilia marudiano Jumatatu.
MATOKEO ya sare ya 1-1 dhidi ya Fountain Gate katika mechi ya kwanza ya mtoano (play off) kuwania kubaki Ligi Kuu imewapa mzuka mabosi wa Tanzania Prisons waliodai mechi haijaisha hiyo na wapinzani wao wajiandae kupasuka Jumatatu watakaporudiana Uwanja wa Sokoine.
Prisons ililazimisha sare hiyo ugenini kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, mjini Babati Manyara baada ya wenyeji kutangulia kwa bao la kipindi cha kwanza kupitia Edger William kabla ya Oscar Mwajanga kuchomoa kipindi cha pili na ssa wanasikilia marudiano Jumatatu.
Mshindi wa jumla wa hatua hiyo atajihakikisha kubaki Ligi Kuu Bara kwa msimu ujao na itakayopoteza itaenda kujiuliza dhidi ya Stand United ili kusalia au kushuka kuzifuata KenGold na Kagera Sugar zilizotangulia mapema na kuipisha Stand kupanda daraja kuzifuata Mtibwa Sugar na Mbeya City.
Katika Ligi Kuu iliyomalizika Jumatano, Prisons ilimaliza nafasi ya 13 kwa pointi 31, huku Founatain Gate ikiwa nafasi ya 14 kwa pointi 29 na kufanya timu hizo kuparuana katika mchujo huo na kwa sare ya juzi iliwafanya mabosi wa klabu hiyo kutamba mechi haijaisha hadi iishe Jumatatu.
Mtendaji Mkuu wa Prisons, John Matei aliliambia Mwanaspoti baada ya sare ya mchezo wa awali, kwa sasa akili na nguvu kubwa zinaelekezwa Sokoine na matarajio yao ni kushinda ili kumaliza hesabu za Ligi Kuu.
Matei alisema tayari uongozi umeshatekeleza wajibu wao kwa kuweka dau kubwa kwa wachezaji kuanzia mechi ya awali na Jumatatu wanahitaji kuongeza zaidi kuhakikisha wanashinda na kuanza maandalizi ya msimu ujao.
“Tutakuwa nyumbani mbele ya mashabiki wetu, tunayo nia na sababu za kushinda mchezo huo japo tunajua haitakuwa kazi rahisi sana, lakini uongozi ulishaweka mazingira mazuri na hamasa kwa wachezaji ni kubwa,” alisema Matei na kuongeza;
“Tulianza kuweka mzigo mechi iliyopita, hivyo hii ni endelevu, kwakuwa tutakuwa nyumbani na tunajivunia bao la ugenini tunahitaji kulinda sana matokeo haya ili kumaliza kazi mapema.”
Kocha Mkuu wa timu hiyo, Aman Josiah alisema matokeo waliyopata si mabaya sana, hivyo kazi inahamia Sokoine kuhakikisha hawafanyi makosa akieleza kuwa mechi hiyo hitaji lao ni ushindi.
“Niwapongeze vijana kwa kazi nzuri japokuwa tulihitaji tumalize shughuli ugenini, lakini kwakuwa tunazo dakika 90 nyingine tunaenda kumalizia nyumbani ili tuwe salama,” alisema kocha huyo aliyeipokea timu hiyo kutoka kwa Mbwana Makatta.