Yanga gonga gonga nyingi

Uchezaji huo ulifanywa na wachezaji wake kwenye mechi yao ya juzi Alhamisi dhidi ya Chipukizi ambapo walishinda bao 1-0 mfungaji akiwa Genilson Santos ‘Jaja’.
Muktasari:
- Uchezaji huo ulifanywa na wachezaji wake kwenye mechi yao ya juzi Alhamisi dhidi ya Chipukizi ambapo walishinda bao 1-0 mfungaji akiwa Genilson Santos ‘Jaja’.
KOCHA mkuu wa Yanga, Mbrazili Marcio Maximo, anataka kikosi chake kicheze soka safi la pasi zenye malengo na kuvutia ‘gonga’ ya moja, mbili unaachia kwa haraka.
Uchezaji huo ulifanywa na wachezaji wake kwenye mechi yao ya juzi Alhamisi dhidi ya Chipukizi ambapo walishinda bao 1-0 mfungaji akiwa Genilson Santos ‘Jaja’.
Maximo alisema: “Timu ipo vizuri, inacheza vile ninavyotaka. Inamiliki mpira, wanacheza kwa pasi nzuri fupi na ndefu, moja...mbili wanaachia, hawakai na mpira wanacheza haraka ndicho nilikuwa nakitaka.
“Tumeshinda bao moja mechi hii lakini nimefurahi namna wachezaji wangu walivyocheza kwa kufuata maelekezo kiujumla wameanza vizuri.”
Hata hivyo Maximo ameisifu Chipukizi kwa kuwapa mazoezi mazuri kwa sababu waliweka ulinzi nyuma na kuifanya safu yao iwe ngumu kupitika.
Kikosi kilichocheza
Katika kikosi cha wachezaji 11 walioanza kucheza dakika 45 za mwanzo, kipa alikuwa, Dida, mabeki wa pembeni kulia ni Juma Abdul na kushoto ni Oscar Joshua.
Mabeki wa kati ni Yondani na Cannavaro, Twite alicheza kiungo mkabaji na kiungo mshambuliaji ni Dilunga, Niyonzima alicheza winga ya kulia na Mbrazili Andrey Coutinho alicheza winga ya kushoto wakati Ngassa alicheza straika wa pili nyuma ya Jaja aliyecheza namba tisa.
Wachezaji 11 waliocheza kipindi cha pili kipa ni Kaseja, mabeki wa pembeni Salum Telela alicheza beki ya kulia na kushoto ilichezwa na Edward Charles.
Mabeki wa kati ni Rajab Zahir na Said Juma Makapu, Omega Seme alicheza kiungo mkabaji na Nizar Khalfan alicheza kiungo mshambuliaji, winga ya kulia ilichezwa na Msuva na Kiiza alicheza winga ya kushoto wakati mastraika wa kati walikuwa ni Tegete na Bahanuzi.
Manyama alitoka na akaingia Amos Abeil, Tegete akaingia Javu, Kiiza aliingia Hamis Thabit. Kikosi kilichoanza kilikuwa bora zaidi ya kilichocheza kipindi cha pili.
Ngassa, Niyonzima, Coutinho na Jaja waliingarisha safu ya ushambuliaji ikawa na mwelewano mzuri. Ngassa alicheza nyuma ya Jaja lakini hakutulia sehemu moja, alishirikiana vizuri na Niyonzima, Coutinho kumchezesha Jaja hadi wakapata bao hilo pekee sawa na kwenye ulinzi wakina Cannavaro, Yondani, Mbuyu, Juma na Oscar no walishirikiana vizuri kuifanya ngome kuwa imara.