Chama la Wana lawapiga 'stop' mashabiki

Muktasari:
- Stand iliyowahi kutamba kwa misimu kadhaa Ligi Kuu, kwa sasa inaisaka tena nafasi hiyo iliyoikosa kwa muda mrefu, huku ikitoa matumaini msimu ujao kufanya hivyo.
ILI kuhakikisha wanatimiza ndoto ya kurejea Ligi Kuu msimu ujao, Stand United 'Chama la Wana' imepiga marufuku muingiliano wa mashabiki kambini kwa wachezaji, ikiwa ni mkakati wa kuwapa uhuru nyota wake kujiandaa na play-off, huku ikitamba yeyote aje.
Stand iliyowahi kutamba kwa misimu kadhaa Ligi Kuu, kwa sasa inaisaka tena nafasi hiyo iliyoikosa kwa muda mrefu, huku ikitoa matumaini msimu ujao kufanya hivyo.
Chama la Wana yenye makazi mjini Shinyanga, ilimaliza ya tatu katika Ligi ya Championship kisha iliifunga Geita Gold katika play-off ya kuwania kupanda Ligi Kuu na sasa inasubiri kibonde wa play-off ya Ligi Kuu kati ya TZ Prisons au Fountain Gate ambazo juzi zilitoka sare na zinarudiana Jumatatu.
Katibu Mkuu wa timu hiyo, Fredi Masai alisema uongozi umeipania sana mechi ya play off na kwa sasa wameimarisha ulinzi kambini kwa wachezaji na hakuna muingiliano wowote ili kila mmoja atimize wajibu wake.
Alisema pamoja na sapoti na muunganiko uliopo wa ndani na nje ya uwanja, lakini hawawezi kumwamini yeyote kwa kipindi hiki na ndiyo sababu ya kuzuia mashabiki kuwatembelea wachezaji kambini.
“Nia si mbaya, bali kuweka mazingira ya wachezaji kujiandaa na mechi ijayo, kila mmoja atimize wajibu wake, hatuwezi kumwamini yeyote kwa kuwa tunayo malengo makubwa msimu huu.”
“Sisi hatuna presha, yeyote aje tu, tunahitaji kumaliza mchezo hapa hapa Kambarage Shinyanga, tukishinda mabao matano au zaidi inaweza kutupa muelekeo na hatma yetu msimu ujao,” alisema kigogo huyo.
Kocha Mkuu wa timu hiyo, Juma Hussein alisema kwa sasa wachezaji wanaendelea na mazoezi kujiandaa na dakika 180 za kuamua hatma yao, akitoa pongezi kwa vijana wake namna wanavyoonesha ari na morali.
“Kisaikolojia wako fiti na tunaendelea kurekebisha na kusahihisha makosa ya kiufundi, kimsingi tunahitaji tucheze Ligi Kuu msimu ujao, lazima tuwaheshimu wapinzani lakini hatuwaogopi,” alisema Kocha huyo.