Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Yanga, Azam, Simba, Namungo tukutane palepale, muda uleule!

TAMBO zimeanza mapema, mashabiki wa klabu zilizotinga nusu fainali wakipigana mkwara kwamba leo wanaenda kumaliza mambo.

Michuano ya Kombe la Mapinduzi imefikia patamu, wakati mechi za nusu fainali zikitarajiwa kupigwa leo kusaka timu mbili za kucheza fainali ya msimu huu itakayopigwa Alhamisi kwenye Uwanja wa Amaan, visiwani hapa.

Kama ilivyokuwa msimu uliopita kwa Yanga na Azam kuvaana mapema saa 10:15 jioni, kisha usiku watani wao Simba kumalizana na Namungo katika mechi ya usiku, ndivyo leo ratiba ilivyo na mashabiki wa timu zote wametambiana; ‘eti tukutane palepale, katika muda uleule’.

Katika mechi hizo za msimu uliopita, Yanga iliing’oa Azam kwa mikwaju ya penalti 5-4 baada ya sare ya 1-1 ndani ya dakika 90, kisha usiku Simba kuisasambua Namungo kwa mabao 2-1, yaliyotiwa kambani na Meddie Kagere na MIraj Athuman aliyeibuka Mfungaji Bora.

Miraji kwa sasa ameachana na Simba na anakipiga KMC iliyopo Ligi Kuu Bara, ila Kagere yupo japo hajaonyesha makali hadi sasa licha ya kucheze mechi mbili za awali za makundi.

Timu hizo zote za Tanzania Bara zilishakutana kwenye mechi zao za duru la kwanza la Ligi Kuu, Yanga ikiitambia Azam kwa mabao 2-0, huku Simba ikiinyoa Namungo kwa bao 1-0 lililowekwa kimiani ‘jioni’ na Kagere kwa kichwa cha kuchupia.

Timu zote kwa jana zilitumia kufanya maandalizi ya mwisho, lakini Simba pia ikifanya utalii wa ndani wa kutembea maeneo tofauti na kitalii kama njia ya kuweka vichwa vyao kwa utulivu kabla ya kuwasha moto usiku wa leo, huku kiungo Mnigeria akitarajiwa kuliamsha tena.

Katika mechi iliyopita ya kukamilisha ratiba ya makundi dhidi ya Mlandege aliingia kipindi cha pili na kucheza dakika kama 15 na kuonyesha uwezo mkubwa, huku mashabiki wakimshangilia kwa soka lake tofauti na Cheick Moukoro na Shiboub Sharraf waliokuja kwa majaribio kusaka kusajiliwa Msimbazi.

Katika mechi za leo Yanga inatarajiwa kuchezesha majembe yake ya kikosi cha kwanza waliokosa mechi za makundi, huku Azam na Namungo zikijipanga kutumia nyota wake wale wale waliokiwasha kwenye mechi zao zilizopita. Azam juzi jioni ilikamilisha makundi kwa kugawa kipigo kinene dhidi ya Yosso Kids iliyotangulia kufunga kabla ya kulala 5-1, huku Idris Mbombo akitupia mawili na kuchaguliwa nyota wa mchezo na kukomba Sh500,000.

Kocha wa makipa wa Azam, Idd Abubakar alisema mechi yao sio ya kisasi, ila wamejipanga kushindana uwanjani.

“Tumecheza na Yanga hivi karibuni kwenye Ligi ya Bara walitufunga mabao 2-0 ni hali ya mchezona msimu uliopita walitutoa kwa penalti ila kwa sasa tunataka kushinda ili tutinge fainali kurudisha heshima katika michuano hii tuliyobeba mara tano,” alisema Idd.

Kocha wa Yanga, Cedric Kaze alisema mashabiki wao watarajie kuona soka tamu pia hata wale nyota waliokosekana kwenye mechi zilizopita ikiwamo hata wachezaji ambao hawakuwepo tangu awali akiwemo Saido Ntibayonkiza.

Nao Simba na Namungo nao wametambiana kila moja akitamba lazima kieleweke kwa kubeba ubingwa wa michuano hiyo.

Kocha Mkuu wa Simba, Pablo Franco alisema mashabiki wao watarajie mabadiliko makubwa ya kikosi chao ambacho amedai ni cha ushindi.

“Tunaifahamu Namungo sio timu ya kuibeza, ina wachezaji wazuri, ila tunahitaji ushindi tu. Kikosi changu kitakuwa na mabadiliko makubwa kulingana na mazoezi yetu ya mwisho leo (jana) usiku,” alisema Pablo na kuongeza;

“Tupo vizuri na tayari kukabiliana na wapinzani wetu. Tutegemee mchezo mzuri kikubwa waamuzi wazingatie sheria za soka.”

Kwa upande wa Namungo kupitia kocha wao wa makipa Josiah Steven alisema wapo imara kuivaa Simba.

“Simba ni timu imara ila watarajie kukutana na upinzani mkubwa, kwani hata sisi tunahitaji ushindi kupitia wao.” alisema Steven.