Yaliyowakumba Namungo yanatukumbusha uzalendo

WIKI iliyopita kuna vitendo vya kikatili michezoni viliikumba Klabu ya Namungo katika safari ugenini wakiwafuata wenyeji wao 1º de Agosto huko Angola katika mchezo wa kwanza wa mtoano wa Kombe la Shirikisho Afrika.

Kwa mujibu wa matukio ambayo yaliripotiwa tangu kufika kwa timu hiyo nchini humo unaweza kupata picha jinsi gani bado kuna mataifa hayajajua kushindana kwa mbinu za uwanjani na kuwa na vita nje ya uwanja kuwaondolea utulivu timu wenyeji kabla ya mchezo.

Uwepo wa mlipuko wa ugonjwa wa Covid 19 na taratibu zake za vipimo bahati mbaya bado Shirikisho la Soka Afrika (Caf) halijajua jinsi gani baadhi ya klabu zinavyotaka kutumia kama fursa ya kuziumiza timu zingine kabla ya kukutana uwanjani.

Hili pia lilikuwa linakwenda kuikumba Namungo nchini Angola inaonyesha wazi wenyeji wao kuna mpango maalumu waliupanga kwa wageni wao ili kuhakikisha wanavuna kabla kukutana uwanjani au wasikutane kabisa.

Kitendo cha kupimwa wachezaji wote kama wana maambukizi na kuwabaini watatu kisha kung’ang’ania timu nzima ikae karantini ulikuwa ni ukatili uliopitiliza kwa wawakilishi hawa na bahati mbaya inawatokea Namungo ambayo ni klabu changa inayoshiriki kwa mara ya kwanza mashindano.

Kwa matukio ya namna ile endapo yangekuwa yameikumba klabu kutoka Kaskazini mwa Afrika inawezekana tungeshasikia taarifa nzito ya waliofanya vitendo vile hata kupewa adhabu kali, lakini bado taarifa mpya inasubiriwa ya kipi kitaamuliwa.

Tuachane na hilo hebu tujiulize tunajifunza kipi sisi kama Tanzania hasa huku Bara katika matukio haya ambayo yanaikumba Namungo lakini pia yakiwa ni ya kawiada kwa klabu zinazoshiriki mashindano ya Afrika mara kwa mara?

Hapa kwetu tumekuwa na kasumba tofauti eti bado mgeni ukiacha huduma za msingi ambazo anatakiwa kupewa, lakini bado kuna ulimbukeni wa kuwapokea wageni na kuwapa taarifa za timu pinzani hasa ile ya nyumbani kisha unawapa taarifa hizo timu ngeni.

Inawezekana hata hao wageni kuna wakati wanatushangaa jinsi gani tumekuwa na akili kinyume chake katika jinsi gani tunavyofanya mambo ya kukomoana hapa ndani lakini baadaye tusijue kama tunajiandalia moto mbaya.

Nimekuwa nikisafiri mara kwa mara mataifa mbalimnbali katika mashindano ya Afrika, lakini katika uzoefu wangu sijawahi kuona eti tunafika taifa fulani tunakutana na watu wanatushangilia hasa wa ndani ya taifa tunalokwenda.

Isiishie hapo katika uzoefu huo, sijawahi kuona taifa tunalokwenda eti tunakutana na timu pinzani ya ile ambayo tunakwenda kukutana nayo inakuja na kutoa siri za timu pinzani kwa timu mgeni ili waifunge.

Matukio haya inawezekana yapo hapa nyumbani tu na tumeamua kuendelea nayo, na sio kitu cha ajabu kukuta mashabiki wa timu fulani wakienda uwanjani na kuanza kuishangilia timu pinzani.

Upo ujinga mwingine zaidi wa hata kununua jezi za timu pinzani na kuzivaa ilimradi tu kuhakikisha timu ya nyumbani inapoteza, unaweza kujiuliza akili zetu zimekufa kwa kiwango gani mpaka tunafikia eneo kama hilo.

Nilichogundua ni jambo moja wengi ambao huongoza kufanya ujinga wa namna hii inawezekana hawajawahi kabisa kusafiri na timu moja kwenda nje ya nchi na kuangalia jinsi timu za huko zinavyoishi wakati wa mashindano ya namna hii.

Pengine ambacho unaweza kushuhudia ni pale unapoifunga timu ya kwao kisha wale mashabiki wa timu pinzani wakati mnapita ndio watawapa hongera na hata kujitambulisha kuwa wao ni mashabiki wa timu pinzani wa ile ambayo imefungwa.

Kabla ya mchezo na hata wakati wa mchezo hutawaona hata mmoja akishangilia au hata kuvaa jezi zenu na kila mmoja anakuwa na habari zake hakuna ambaye atakushangilia wala kukupa nguvu ili ushinde, na zaidi utakutana na mashabiki wa timu husika na watakupa ishara ya kwamba umekuja kufungwa tu.