Hiki kingewapata Namungo FC

Gumzo kubwa wiki hii lilikuwa likihusu timu ya Namungo FC ambayo ilitua wiki iliyopita nchini Angola kwa ajili ya pambano la Kombe la Shirikisho barani Afrika dhidi ya CD de Agosto ya huko. Mara baada ya kutua nchini humo wachezaji wote walitakiwa kuwekwa karantini katika hoteli waliyofikia wakielezwa kuwa vipimo vinaonyesha kuwa watatu kati yao wana maambukizi ya Covid-19.

Hata hivyo, Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) limeifuta mechi iliyokuwa ichezwe Jumapili kutokana na tukio hilo ambalo lilileta taharuki kwa pande zote mbili.

Kwa upande wa uamuzi wa kuifuta mechi hiyo inaweza kuwa ni faida kwa Namungo FC - hii ni kutokana na namna walivyofanyiwa mara baada ya kuambiwa wabaki tu hotelini.

Tukio kama lile la kuwekwa wote karantini kwa ghafla lingeweza kuwaathiri kisaikolojia na hata ingetokea wakacheza mechi na timu hiyo, ingeathiri kiwango chao cha uchezaji.

Kuhudumiwa kwa namna ile kama vile sio binadamu kunaweza kuwapa wachezaji mpasuko wa hisia na hatimaye wakakosa furaha na kuwa wanyonge, hivyo ingekuwa vigumu kucheza kwa kujiamini.

Hali kama ile ni kawaida pia kuwakuta wachezaji wakiwa katika hali ya hofu au woga na kupata msongo wa mawazo vingeweza kuwapata wachezaji hao pamoja na viongozi walioambatana nao.

Mchezaji anapokuwa katika hali ya matatizo ya kiakili anaweza kushindwa kuzingatia maelekezo wakati wa mafunzo au mazoezi na mechi matokeo yake ni kucheza kwa kiwango cha chini.

Baada ya uamuzi huo wa CAF timu hiyo iliondoka nchini humo juzi mchana na kurudi Tanzania, lakini wachezaji watatu waliogundulika kuwa na maambukizi ya Covid-19 na kiongozi mmoja walibaki.


HATIMA WACHEZAJI COVID-19

Tangu kulipuka kwa janga la Covid-19 mwishoni mwa mwaka juzi hakuna mwanamichezo ambaye yupo katika michezo ambaye ameripotiwa kufariki dunia. Mwaka jana, Desemba, mastaa kama Sadio Mane wa Liverpool na Cristiano Ronaldo wa Juventus ni moja kati ya wachezaji waliogundulika kuwa na maambukizi, lakini walikaa karantini kwa siku 14 na baadaye waligundulika kupona na kutokuwa na maambukizi.

Vilevile Kocha wa Arsenal, Mikael Arteta na Zinedine Zidane wa Real Madrid walipata pia maambukizi ya corona, lakini tahadhari zote walichukua kama walivyofanya Mane na Ronaldo.

Hapa tunapata picha kuwa corona haina nafasi kwa mwanamichezo ambaye bado anaendelea kucheza mara kwa mara kama sehemu ya maisha yake.

Mazoezi na kushiriki michezo kunawafanya kuwa na miili timamu yenye afya njema na kinga imara.

Hivyo wachezaji wale watatu wa Namungo hawapaswi kuwa na hofu wala wasiwasi na hatima yao, kwani baada ya siku 14 za karantini kupita watarudi tena kuwajibika katika timu yao.


KUWALINDA MATATIZO YA AKILI

Ili mchezaji kucheza katika kiwango bora na kufanya vizuri zaidi anahitaji kuwa na utulivu wa kiakili kuweza kucheza kwa kujiamini wakati wote wa mchezo.

Kukabiliana na hali kama hii wachezaji hupewa msaada wa kisakolojia toka kwa wataalamu wa tiba, wanasaikolojia na benchi la ufundi na viongozi.

Kipindi cha wachezaji wale kuwa karantini ni mazingira yanayoweza kuwaathiri kiakili zaidi, hivyo ni muhimu kuwapa faraja kwa kuwasiliana na watu ambao watawapa furaha na sio kuwapa shinikizo.

Ni muhimu kuzingatia zaidi lishe bora yenye mchanganyiko wa vyakula na huku wakitumia zaidi protini, mbogamboga, matunda na maji ya kutosha.

Wakiwa karantini hawatakiwi kuacha kufanya mazoezi mepesi na ya kunyoosha viungo hata kama wako katika eneo dogo. Mazoezi yanaboresha afya ya mwili na pia kuondoa matatizo ya kiakili.

Katika mazingira yale wanatakiwa kutumia muda mwingi kujiburudisha na muziki mzuri utakaowapa hisia za furaha, hii inasadia kuondokana na msongo wa mawazo hivyo kupata utulivu wa kiakili.

Watumie mitandao kwa uangalifu kwani hivi sasa kuna janga la taarifa zinazoweza kuwapa hofu. Wanaweza kutumia muda wao zaidi kuangalia mechi za mpira au kucheza gemu za mpira wa miguu.

Wapate mapumziko na kulala angalau saa 6 hadi 8 kwa usiku mmoja ili kuweza kuupa mwili nafasi na kinga kukabiliana na maambukizi hayo.

Washikamane na ushauri wa wataalamu wa afya ili wasiweze kueneza maambukizi kwa kuzingatia njia zote za kujikinga ikiwamo kunawa mikono kwa maji tiririka au vitakasa mikono na kuvaa barakoa.

Watoe taarifa mapema kwa daktari wa timu pale watakapoona wanapata dalili zisizo za kawaidia ikiwamo kuumwa kichwa, kikohozi kikavu, homa, kushindwa kupumua, uchovu na koo kuuma.

Imeandikwa na Dk Shita Samweli