Maajabu!, Wabrazili walioshutua ndani ya miaka 20 ya Mwanaspoti

Walianza na moto kisha...!

MBRAZIL wa kwanza kuifundisha Taifa Stars alikuwa ni Clovis de Oliveira aliyeinoa timu hiyo ya taifa kwa miaka miwili kabla ya kufutwa kazi na nafasi yake alipewa kwa muda Badru Hafidh ambaye mdogo wake, Mohammed Badru ni kocha wa Gwambina.

Ilichukua miaka tisa Tanzania kutoa nafasi kwa mara nyingine tena kwa kocha wa Kibrazil tangu kuondoka kwa Oliveira. Alifuata Julio Cesar Leal na ndani ya mwaka 2006 ndipo alipotangazwa Marcio Maximo kuwa kocha mwingine mpya kutoka Brazil kuifundisha Taifa Stars.

Maximo ndilo jina pekee la Kibrazil ambalo bado lipo masikioni kwa wadau wa soka la Tanzania kwa miaka 20 kutokana na mambo makubwa ambayo aliyafanya na maajabu hayo yalitokea wakati huo gazeti la Mwanaspoti likiwa na miaka minane sokoni.

Mwanaspoti lilikuwa mstari wa mbele akati huo kuripoti vile ambayo kocha huyo aliiongoza Tanzania kuanzia Februari 22 hadi Machi 8, 2009 kushiriki kwa mara ya kwanza Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (Chan), Ivory Coast.

Anakumbukwa kwa kuipandisha Tanzania katika viwango vya ubora wa soka duniani vitolewavyo na Shirikisho la Soka Duniani (Fifa) toka 167 hadi 108. Hakuna kocha mwingine ndani ya miaka 20 ya Mwanaspoti aliyefikia mafanikio hayo licha ya kwamba alifutwa kazi, 2010, baada ya mambo kuwa ndivyo sivyo.

Kipindi cha Maximo ndipo kulikuwa na utitiri wa makocha wengine kutoka Brazil kuja na kutamba nchini akiwamo Neider dos Santos aliyewahi kuzinoa Simba na Azam. Pia kuna Itamar Amorin, Markus Tinoco, Leornado Neiva na Nielsen Elias ambao waliwahi kufundisha timu za taifa za vijana, Yanga na Simba. Upepo wa makocha wa Kibrazili kutua nchini kufundisha soka ukabadilika badala ya kuwa makocha, sasa wakaanza kumiminika wachezaji kwa vipindi tofauti.

Kumbuka ilikuwa vigumu siku za nyuma kwa mchezaji kutoka Brazil kufunga safari akivuka maji na mabara hadi Tanzania, lakini iliwezekana kwa wachezaji saba tofauti kuwahi kucheza soka Tanzania.

Hata ujio wa wachezaji hao kuna wakati uliwachanganya watu na kushindwa kuamini ilikuwaje hata wakafunga safari masafa marefu ili kuja kukipiga katika nchi hii ambayo pengine hata baadhi ya raia wa Brazil hawakuwahi kuisikia.

Hapa chini makala hii inakuletea wachezaji hao saba waliocheza Ligi Kuu Bara ndani ya miaka 20 ya utoaji taarifa za michezo kwa gazeti la Mwanaspoti.


GABRIEL BARBOSA

Mwaka 2012, Gabriel Barbosa alitambulishwa kuwa mchezaji rasmi wa Coastal Union ya Tanga akitokea New Road ya Nepal aliyojiunga nayo mwaka 2010.

Pia aliwahi kuzichezea Paham Footbal Club, Flamengo, Santa Cruz zote za Brazil na Churchill Brothers ya India, Maruinense pamoja na Sport Club ya Jiji la Paulo Afonso.

Huyu ndiye mchezaji wa kwanza wa Kibrazili kuwahi kuja kucheza soka nchini, japo hakupata mafanikio makubwa kama ilivyotarajiwa licha ya kutua kwa kishindo.

Pamoja na kuwa alitua kwa kishindo, huku wakiwatangazia wapinzani wao kuwa watakiona cha moto, mambo yalikuwa tofauti. Waswahili husema mipango si matumizi na jamaa alichemka na Coastal wakaamua kuachana naye.

Hata hivyo, inaelezwa sababu ya Barbosa kushindwa kucheza soka nchini ni mkewe ambaye alidaiwa hakufurahishwa na mazingira ya Bongo na kumfanya mzee mzima ashindwe kuweka akili uwanjani ili kumridhisha mke na kuamua kurudi nchini kwao.

Kadhalika ni lazima ujue mapema kuwa, Barbosa ambaye aliichezea Coastal Union hana uhusiano wowote na yule wa Flamengo ambaye aliwahi kuichezea Inter Milan ya Italia - ni majina tu yanafanana.


ANDREY COUTINHO

Mwaka 2014, Yanga ilifanya uamuzi wa kumrejesha Kocha Maximo huku wakimpa jukumu la kuwa kocha wao mpya na jamaa alitua na wachezaji wawili wa Kibrazili kina Geilson Santos Santana ‘Jaja’ na Andrey Coutinho ambao aliamini angepata nao mafanikio akiwa timu hiyo yenye maskani yake Jangwani, Dar es Salaam.

Coutinho ambaye alikuwa kiungo mchezeshaji alionekana kumudu soka la Tanzania kwa kiwango kikubwa. Hata baada ya kutimuliwa kwa Maximo aliendelea kuonyesha ufundi wake akiwa na Wananchi tofauti na mwenzake, Jaja, ambaye alichemka na kuondoka katikati ya msimu.

Kiungo huyo ambaye kwa sasa yupo zake Thailand ambako anaichezea Esan Pattaya FC, anasema: “Nina kumbukumbu nyingi nikiwa Tanzania, niliishi vizuri na nilifurahia upendo wa mashabiki wa Yanga, ni wa kipee kwangu na daima nitawakumbuka.”


GEILSON SANTANA

Wengi wanamjua kwa jina la Jaja na kama mtakukumbuka 2015 wakati Yanga ikiiadhibu Azam FC kwa mabao 3-0 kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii, Uwanja wa Taifa kwa sasa kwa Mkapa, Jaja alikuwa miongoni mwa wafumania nyavu wa timu hiyo.

Mchezo huo ulimpa ujiko Jaja kwani alitupia mabao mawili likiwamo moja la kideo, lakini baada ya mchezo huo hakuonekana tena kuonyesha makali na badala yake alionekana kuwa mchezaji wa kawaida na mkataba wake ulipomalizika Yanga iliamua kuachana naye na akarejea kwao, Brazil.

Hii ni kwa kuwa mpaka anaondoka baada ya kuitumikia Yanga kwa miezi kama sita alifunga bao moja tu wakati Yanga ilipolala 2-1 mjini Morogoro dhidi ya Mtibwa Sugar.

Straika Saimon Msuva ambaye alicheza kikosi kimoja na Mbrazil huyo huku katika ule mchezo wa Ngao ya Jamii aliyong’ara akimtengenezea miongoni mwa mabao aliyofunga, anasema kilichomwangusha mshambuliaji huyo ilikuwa ni viwanja vya mikoani.

“Nakumbuka kwenye ile mechi ya hisani nilimtengenezea bao lake la kwanza na mimi nilifunga moja. Kama ligi yetu ingekuwa ikichezwa kwenye viwanja vizuri mechi zote, basi nadhani angefanya vizuri tu bila tatizo,” anasema.


EMERSON DE OLIVEIRA

Baada ya kuondoka kwa Jaja, Yanga iliamua kushusha kifaa kingine kutoka Brazil ambacho ni Emerson De Oliveira aliyekuwa akicheza nafasi ya kiungo mkabaji. Kabla ya kuamua kuja Tanzania, Emerson alikuwa akiichezea timu ya Bonsucesso FC iliyokuwa inashiriki Ligi Daraja la Pili nchini Brazil. Kama ambavyo ilikuwa kwa Jaja, basi huyo naye alichemka kuendana na mikikimikiki ya Ligi Kuu Bara.


WILKER DA SILVA

Baada ya kina Emerson na Jaja kutimka kwa aibu Yanga, watani zao waliamua kuwashusha nao Wabrazili watatu kwa mpigo. Waliwaleta Wilker da Silva na wenzake wawili na kama ilivyokuwa kwa kina Jaja, Wilker naye alichemka akiwa na Wekundu wa Msimbazi na uamuzi ambao vigogo wa timu hiyo walifikia naye baada ya kushinda kuonyesha makali yake ilikuwa ni kuvunja mkataba wake, huku akitakiwa kila la heri huko aendako.

Wilker alikuwa akisumbuliwa na majeraha ya hapa na pale, lakini baada ya kupona alionekana kuwa na uzito mkubwa na baada ya kuwa sawa kiwango chake kilionekana kuwa cha kawaida, hivyo Simba ilihitaji mshambuliaji mwingine wa nguvu kwa hesabu ya kujiimarisha kwa ajili ya Ligi ya Mabingwa Afrika.


TAIRONE
SANTOS

Alianza kuondolewa Wilker kwa kukatishwa mkataba wake halafu akafuata Tairone kabla ya Gerson Fraga kupata majeraha. Huyu alikuwa beki wa kati mwenye umbo zuri, lakini udhaifu wake hakuwa na kasi licha ya kwamba alikuwa akipata nafasi ya kucheza mara kwa mara kwenye kikosi cha kwanza cha Simba.

Licha ya uwepo wa Tairone, Simba waliona hatoshi, hivyo walitamani kuwa na beki wa nguvu zaidi, na waliamua kuachana naye ndio maana dirisha lililofuata la usajili walimsajili Mkenya Joash Onyango kwa ajili ya kuziba pengo lake.


GERSON FRAGA

Juni 2019 ndicho kipindi ambacho Simba ilitikisa kwa kusajili wachezaji watatu wa Kibrazili akiwemo Fraga na wenzake ambao ni Wilker da Silva na Tairone Santos.

Ukweli ni kwamba kati ya wachezaji hao watatu ni Fraga ambaye alionekana kuwa kwenye kiwango bora zaidi baada ya kulisoma soka la Tanzania na kwa kiasi kikubwa alilimudu na kuonyesha kiwango kizuri hata kwenye michezo ya mikoani.

Alionekana kuongeza kitu kipya kwa Simba kwenye eneo lao la kiungo, na alikuwa akifanya vizuri sambamba na Jonas Mkude, lakini bahati mbaya alipata majeraha kwenye mchezo wa ligi dhidi ya Biashara United. Aliumia vibaya goti, hivyo ilimbidi kuwa nje ya uwanja kwa karibu msimu mzima.

Kutokana na hali hiyo Simba haikuwa na jinsi zaidi ya kumpa ruhusu kiungo huyo kurejea kwao Brazil kwa ajili ya kuuguza majeraha yake. Akiwa kwao alifanyia upasuaji na kupatiwa matibabu na taratibu amekuwa akionekana kufanya mazoezi mepesi. Huyu ndiye mchezaji wa mwisho kutoka Brazil kucheza ndani ya Ligi Kuu Bara.

“Bado nina mapenzi makubwa na Simba na itabaki kuwa moja ya klabu ambayo niliichezea kwa moyo na upendo wangu wote,” anasema Fraga aliyewahi kuwa nahodha wa Coutinho anayetamba Bayern Munich akiwahi kuzichezea pia Barcelona na Liverpool wakiwa ndani ya kikosi cha timu ya vijana ya Brazil enzi hizo. Kwa sasa nafasi ya Mbrazili huyo ndani ya Simba imerithiwa na Mganda, Taddeo Lwanga.