Yaani ukizubaa tu imoo!

Muktasari:
- Yaani mchezo ukianza tu ukizubaa ghafla tu, imooo na hata muda ukiyoyoma ukizubaa nako kidogo tu watu wanaweka kitu imooo! Mwanaspoti linakuletea orodha ya mabao hayo na wafungaji wake waliotupia mapema na yale jioni vilevile.
SIMBA imetetea taji lake la Ligi Kuu Bara kwa msimu wa pili na kesho itakabidhiwa rasmi kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro mara baada ya mchezo wao na Mtibwa Sugar.
Mabingwa hao walizizidi ujanja klabu nyingine 19 ilizochuana nazo katika msimu huu wa 2018-2019.
Simba imebeba taji hilo, huku ikiwa pia imetoa Mfungaji Bora kama ilivyokuwa msimu uliopita walipobeba kombe na Emmanuel Okwi kuwa kinara wa mabao akifunga 20.
Safari hii straika wao mwingine mkali, Meddie Kagere amejihakikisha Kiatu cha Dhahabu kwa mabao yake 23 (idadi inayoweza kuongezeka kama kesho atafunga tena) licha ya ugeni wake katika Ligi Kuu Bara kwani, alisajiliwa msimu huu akitokea Gor Mahia ya Kenya.
Mpaka mechi ya juzi Jumamosi wakati Clatous Chama akifunga bao la kusawazisha dhidi ya Biashara United katika mechi iliyoisha kwa sare ya 1-1, jumla ya mabao 727, lakini katika mabao hayo yapo yale ya mapema zaidi na yale ya jioni kijua kikizama.
Yaani mchezo ukianza tu ukizubaa ghafla tu, imooo na hata muda ukiyoyoma ukizubaa nako kidogo tu watu wanaweka kitu imooo! Mwanaspoti linakuletea orodha ya mabao hayo na wafungaji wake waliotupia mapema na yale jioni vilevile.
MABAO YA MAPEMA
DAKIKA 1
Mashabiki wa soka nchini wanamuita Kelvin Sabato ‘Kiduku’, huyu ndiye anayeshikilia rekodi ya kufunga bao la mapema zaidi akitumia dakika moja kuisaidia Mtibwa kushinda mabao 4-0 dhidi ya Ruvu Shooting.
Mabao mengine katika mchezo huo yalifungwa na Salum Kihimbwa, Juma Liuzio, Jaffar Kibaya.
Naye straika wa Coastal Union, Rayzin Hafidh pia alifunga bao la dakika ya kwanza katika mchezo ambao Coastal ililala 2-1 dhidi ya Simba, kadhalika kiungo Kenny Ally aliifungia Singida United katika dakika 1 kwenye mchezo wao dhidi ya Kagera uliomalizika 2-1.
DAKIKA 2
Msimu huu ni kama ulikuwa na upepo wa magoli ya mapema kwani katika dakika hii, washambuliaji wengi walipata magoli na kuwafanya kuingia katika orodha ya kupasia mabao ya mapema.
Mshambuliaji wa Simba, Meddie Kagere ndiye alikuwa mchezaji wa kwanza kufunga bao la mapema zaidi kwa kutumia dakika 2 dhidi ya Prisons kabla ya rekodi hiyo kuja kufikiwa na kupitwa na wachezaji wengine.
Mshambuliaji Mohammed Mussa akifunga goli katika dakika hii katika mchezo dhidi ya Kagera Sugar uliomalizika kwa sare 1-1, kama ilivyo kwa mshambuliaji wa zamani wa Mbeya City, Eliud Ambokile aliifungia timu hiyo katika mchezo dhidi ya Mwadui FC.
Jaffary Kibaya wa Mtibwa naye alifunga dhidi ya Alliance mchezo uliomalizika 1-0, huku
Donald Ngoma na Dickson Ambundo nao ni kati ya wachezaji waliofunga mabao ya mapema, kila mmoja akifunga katika dakika ya pili ya mchezo. Ngoma alifunga dhidi ya Mtibwa Sugar, huku Ambundo akitupia kwenye mchezo wao na Stand United.
Katika mchezo huo wa Alliance ilishinda mabao 3-2, huku Ambundo akifunga mawili.
DAKIKA 3
Beki wa Mtibwa Dickson Daud anakuwa wa kwanza kuingia katika orodha hii baada ya kufunga dhidi ya KMC katika sare ya bao 1-1.
Mwingine ni Charles Chinonso wa Stand Utd, ambaye alifunga katika ushindi wa 1-3 dhidi ya Kagera Sugar katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Kaitaba.
Wengine ni Salim Aiyee (Mwadui) na Abdulrahaman Mussa (Ruvu Shooting), ambao wote katika mchezo wao ambao Shooting ilishinda 6-2 wachezaji hao walifunga dakika ya 3 kila mmoja.
Aiyee pia alifunga goli lingine katika mchezo dhidi ya Kagera Sugar ambao walishinda 4-0.
DAKIKA ZA MWISHO
ALEX KITENGE v YANGA
Mchezo huu ulipigwa Septemba 16 na Yanga iliyokuwa mwenyeji iliibuka na ushindi wa mabao 4-3 yaliyofungwa na Mrisho Ngassa, Ibrahim Ajib, Deus Kaseke pamoja na Andrew Vicent ‘Dante’.
Ndio mchezo wa kwanza kuzalisha hat trick Ligi Kuu ambayo iliwekwa na Alex Kitenge dakika ya 15, 59 na bao la mwisho akipiga dakika 90+ na kuongeza presha kwa Yanga huku langoni akiwa Klaus Kindoki. Mchezo huo ndio ulianza ulianza kuwachonganisha mashabiki wa Yanga na Kindoki.
ROBERT NDAKI v PRISONS
Ulikuwa mwezi wa majanga kwa timu kuachia pointi dakika za mwishoni, Mshambuliaji wa Mbao FC, Robert Kindaki aliihakikishia timu yake kubakisha alama tatu nyumbani katika mchezo uliopigwa Septemba 24.
Zikiwa zimesalia sekunde chache huku Prisons ikiamini itaondoka na alama moja ugenini, lakini mambo yakabadilika kwa bao la Kindaki.
IBRAHIM AJIB v MBAO
Staa huyo alinogesha ushindi wa maboa 2-0 walioupata Yanga, baada ya Rafael Daudi kufungua pazia ya mabao siku hiyo dakika ya 16 alipoiweka kifua mbele Yanga dhidi ya Mbao FC.
Wakati Ajibu akifanya yake siku hiyo (Oktoba 7) Juhudi Philemon naye aliinusuru Alliance kwenye kichapo baada ya kusawazisha dakika za nyongeza na mchezo kumalizika kwa sare ya bao 1-1, baada ya Abdulrahman Mussa kuiweka mbele JKT Tanzania dakika ya 70.
Lameck Chamkanga wa Biashara naye alirahisisha kazi kwa Mwadui alipojifunga dakika ya 89 katika harakati za kuokoa na kuifanya Mwadui kuibuka na ushindi wa 2-0.
ZABRON HAMIS v SIMBA
Mchezo wa pili kuzaa hat trick pale Emmanule Okwi aliponogesha ushindi wa maboa 5-1 dhidi ya Alliance baada ya mabao mengine ya Asante Kwasi na Adam Salamba.
Hata hivyo, Simba ikiamini itamaliza dakika 90 bila nyavu zao kuguswa, Zabona Khamis alionyesha umahili wake kwa kuichambua ngome ya Simba na kuachia mkwaju mkali uliomshinda Aishi Manula.
EVALIGESTUS MUJWAHUKU v MBEYA CITY
Jamaa alipindua meza kibishi unaambiwa, hadi dakika ya 80 Mbao FC iliyokuwa nyumbani ilikuwa imepigwa 2-0 mabao ya Iddy Selemani (11), na Eliud Ambokile (48).
Evaligestus Mujwahuki akaikomboa Mbao FC kwa mabao yake ya dakika 83 na lile la dakika za nyongeza na ngoma kumalizika kwa sare ya mabao 2-2 jambo lililowafurahisha Mbao na kuwa machungu kwa Mbeya City.
MARTIN KIGGI v SINGIDA UNITED
Ilikuwa siku njema kwa mkali huyo wa Alliance alipoihakikishia timu yake kubaki na alama tatu nyumbani, baada ya kungoja hadi dakika za nyongeza waliopoibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Singida United.
Naye Jaffar Kibaya alinogesha ushindi wa mabao 4-0 wakati Mtibwa ikiiadhibu Ruvu huku Kibaye baada ya kurudi kambani dakika za nyiongeza siku hiyo.
AMISS TAMBWE v PRISONS
Tanzania Prisons ikiwa katika dimba la nyumbani Uwanja wa Sokoine ilikwenda mapumziko ikiwa kifua mbele kwa bao la mkwaju wa penati kupitia kwa Jumanne Elfadhil.
Yanga ilirejea dakika 45 za kipindi cha pili kusaka ushindi katika mchezo huo ulioshuhudia kadi nyekundu za Mrisho Ngassa (Yanga) na Laurian Mpalile (Prisons).
Ajibu alijibu mapigo dakika ya 76 kabla ya Tambwe aliyetokea benchi kutupia dakika ya 85 na dakika za nyongeza na kuondoka na ushindi wa mabao 3-1.
WENGENE HAWA HAPA
Said Dilunga naye alitupia moja Ruvu ilipolala dhidi ya Lipuli 2-1, Steven Mganga alitupia mbili nyavuni kwenye ushindi wa mabao 2-0 Lipuli FC dhidi ya Mbeya City, Makambo aliipaisha Yanga ilipoilaza 3-2 Ruvu.
Naye David Mwasa aliiokoa KMC kwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Mbao FC na Hafidh Mussa akaibeba Stand United kwenye sare ya bao 1-1 dhidi ya Alliance. Donald Ngoma alifanya kweli dhidi ya Singida Utd, Jacob Masawe (Stand Utd) dhidi ya Mwadui mchezo ulimalizika kwa Mwadui 1-2 na Stand Utd.
Kwa mara nyingine tena Donald Ngoma vs Kagera Sugar mchezo ulimalizika Azam Fc 2-0, Miraj Athuman (Lipuli) Vs Lyon mchezo ulimalizika Lyon wakishinda 2-0, Ismail Mhesa vs Singida ambapo Singida Utd walishinda 2-1, Peter Mapunda (Mbeya City) dakika 88 katika mchezo wao dhidi ya Lipuli ambao Mbeya City waliibuka na ushindi wa 3-0, Idd Seleman (Mbeya City) dakika 90+ katika mchezo wao dhidi Coastal Union uliomalizika kwa 1-0 na Mohammed Kapeta (Mbeya City) aliyefunga goli la kuchomoa dakika 90+ katika mchezo wao dhidi ya Lyon uliomalizika kwa sare 2-2.