Watano Simba wapewa Azam

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Bara Simba leo Jumatano watakuwa wageni wa Azam kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara utakaopigwa kuanzia saa 1:00 usiku kwenye Uwanja wa Azam Complex.

Kocha wa Simba, Pablo Franco alisema pamoja na wasaidizi wake wametumia muda wa kutosha kuangalia michezo mbalimbali ya Azam msimu huu kwenye ligi pamoja na ile dhidi ya Simba lakini kutakuwa na sura tano zitakazoingia kwenye kikosi cha kwanza.

“Kwenye kikosi changu kuna baadhi ya wachezaji hawakupata nafasi ya kucheza kwenye mechi iliyopita ili kuwapa muda wa kupumzika kutokana na kucheza mechi nyingi mfululizo,” alisema Pablo na kuongeza;

“Wachezaji waliokosekana kwenye mechi iliyopita watakuwepo dhidi ya Azam kwani hata mbinu tutakazokwenda nazo ni tofauti na ilivyokuwa mara ya mwisho kuonekana uwanjani, kulingana na uhitaji wa ushindi kwenye mchezo huo, tutaingia na mabadiliko ya kimbinu kulingana na yale tuliyoyafanyia mazoezi pamoja na wapinzani wetu walivyo.

“Tunafanya yote haya kuhakikisha tunapata ushindi na kuongeza pointi katika msimamo wa ligi ili kupunguza zile alizokuwa nazo kinara kwani tunaamini ushindani ni mkubwa, hakuna anayeweza kufahamu kesho itakuwaje kutokana na mbio za ubingwa zilivyo,” alisema kocha huyo.

Wachezaji wa kikosi cha kwanza Simba ambao hawakucheza mechi ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho (ASFC) ni Aishi Manula, Shomary Kapombe, Joash Onyango wakati Sadio Kanoute na Pape Sakho wao waliingia kipindi cha pili.

Pablo alisema hakuna mechi rahisi Simba inapokutana na Azam bali kunakuwepo na ushindani wa kutosha kwenye maeneo mbalimbali kulingana na ubora wa timu zote mbili.

Ndani ya mwaka huu, timu hizo zimekutana mara mbili, awali katika raundi ya kwanza ya Ligi Kuu Bara Januari 1, ambapo Simba ilishinda 2-1 kwa mabao ya Sadio Kanoute na Pape Sakho, la Azam likifungwa kwa tiktaka ya Rodgers Kola na mara ya pili zilikutana kwenye fainali ya Kombe la Mapinduzi, Simba ikishinda kwa bao la Medie Kagere.