Musa Mbisa hataki tena presha Ligi Kuu

Muktasari:
- Timu hiyo ambayo ilisubiri hadi mchezo wa mwisho wa play off dhidi ya Fountain Gate, imekuwa na matokeo yasiyoridhisha kwa misimu kadhaa kukumbwa na presha ya kukwepa kushuka daraja.
KIPA wa Tanzania Prisons, Musa Mbisa amesema presha waliyokutana nayo msimu ulioisha hivi karibuni, hawatarajii kujirudia msimu ujao, akiiweka mtegoni timu hiyo juu ya hatma yake.
Timu hiyo ambayo ilisubiri hadi mchezo wa mwisho wa play off dhidi ya Fountain Gate, imekuwa na matokeo yasiyoridhisha kwa misimu kadhaa kukumbwa na presha ya kukwepa kushuka daraja.
Mbisa ambaye alikuwa miongoni mwa makipa ghali kikosini tangu alipotua kwa Maafande hao kutokea Coastal Union, walimaliza Ligi nafasi ya 13 kwa pointi 31 na kujinusuru kupitia play off kwa mabao 4-2 dhidi ya Fountain Gate.
Mbisa amesema hawakuwa na mwanzo mzuri kabla ya kuonesha mabadiliko mzunguko wa pili, akikiri presha waliyokutana nayo haikuwa nyepesi lakini wanashukuru kubaki salama.
Amesema kwa sasa hana uhakika wa kubaki kikosini, akieleza muda ukifika utaamua msimu ujao kukipiga wapi, akieleza matumaini yake msimu ujao ni kuona Prisons ikifanya vizuri.
“Ligi ilikuwa ngumu, hatukuwa na mwanzo mzuri lakini malengo yametimia kwa kubaki salama Ligi Kuu, presha ilikuwa kubwa kwakuwa Fountain Gate walitupa upinzani mkali.”
“Kujua hatma yangu Prisons tusubiri msimu ujao, kwakuwa naweza kubaki au nisibaki, kwa jumla niwashukuru mashabiki lakini niwaombe waendelee kushirikiana na timu ili kuwa bora,” amesema kipa huyo.
Nyota huyo aliyewahi kutikisa Mwadui (kwa sasa Bigman), alikiri ushindani wa namba kikosini, akieleza hali hiyo ilimpa nguvu kujituma kuhakikisha anapata namba kikosi cha kwanza.