Wasanii 10 kunufaika na viwanja vya bei chee

Muktasari:
Mkuu huyo wa wilaya aliyasema hayo wakati wa kumkabidhi kiwanja balozi wa kampuni hiyo na nyota wa filamu, Jacob Steven (JB), na kumtaka kuitangaza vyema kampuni hiyo.
Dar es Salaam. Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Hashim Mgandilwa ameiagiza kampuni ya uuzaji Viwanja ya Datum ya jijini Dar es Salaam, kuwapatia viwanja kumi wasanii kwa bei nafuu.
Mkuu huyo wa wilaya aliyasema hayo wakati wa kumkabidhi kiwanja balozi wa kampuni hiyo na nyota wa filamu, Jacob Steven (JB), na kumtaka kuitangaza vyema kampuni hiyo.
Katika hafra hiyo iliyofanyika katika eneo hilo la viwanja, mkuu huyo wa wilaya aliwataka wananchi kuwa na utaratibu wa kununua maeneo yaliyopimwa ili kuepuka migogoro na serikali, pia kuwasaidia katika majanga kama ya moto na magonjwa.
Alisema, mtu anapoishi kwenye eneo lilipimwa ni rahisi gari ya zimamoto au ya wagonjwa kufika kwa urahisi na kutoa msaada tofauti na yule ambaye anaishi kwenye eneo ambalo halijapimwa.
Pia, mkuu huyo wa wilaya aliwataka wawekezaji kuwekeza wilayani hapo kwa kuwa kuna akiba ya zaidi ya viwanja mia nne kwa ajili ya viwanda na magodauni.
JB aliishukuru kampuni ya Datum kwa kumpa fursa hiyo na kuahidi kuitangaza vyema kampuni hiyo huku akiwahamasisha wasanii wenzake kununua maeneo yaliyopimwa.