Wasafi mara Maulid Kitenge jibu ni EFM kulikoni!

Muktasari:
Tabia hiyo ya kuiga, ndio inafanya redio nyingi zifanane na Clouds FM. Kila redio inataka kuwa na vipindi kama Clouds. Mwendo huo unasababisha watangazaji nao, watangaze kama Clouds. Mtindo wa utangazaji wa B12 upo ndani ya watangazaji wa redio nyingi.
WABONGO hawatabadilika! Hulka ileile ya kugandamizia. Arrawa baada ya kuona baa ya Mushi mambo ni mpwitompwito, naye akafungua jirani. Alipoona mambo hayaendi, akanunua wahudumu wa Mushi, kwa kuamini ndio waliokuwa kivutio cha wateja!
Wamiliki wa baa wakageuka wafuga machangudoa mjini Dar, wakidanganyana, eti huongeza wateja. Waligandamizia Corner Bar, Sinza. Hawawazi kuna watu hawawezi kwenda baa yenye machangudoa kwa sababu ya kuogopa kuonekana wanunuzi au maadili yao hayawaruhusu!
Ndivyo biashara ya saluni ilivyovamiwa, kupandiana dau kwa vinyozi mpaka mabinti wenye kuosha na kufanyia scrub wateja. Unashangaa eti, mrembo fulani dili kweli. Saluni zinamgombea. Huvuta wateja!
Yalitokea Breakpoint, enzi hizo Kijitonyama. Ilipoonekana biashara inafanyika sana, kuna baa nyingine ikajengwa jirani. Tukawa tukikaa Breakpoint, jamaa anatusomesha baa yao jirani inatoa huduma ya chakula, kama Breakpoint. Jamani!
Unafungua duka la nguo kisha lingine linafunguliwa. Kutahamaki, Dar es Salaam, imejaa maduka ya nguo. Mengine yanafungwa.
Tabia hiyo ya kuiga, ndio inafanya redio nyingi zifanane na Clouds FM. Kila redio inataka kuwa na vipindi kama Clouds. Mwendo huo unasababisha watangazaji nao, watangaze kama Clouds. Mtindo wa utangazaji wa B12 upo ndani ya watangazaji wa redio nyingi. Sijui ndio nini sasa?
Utasikia watangazaji wanaigana: “Msanii ambaye wimbo ambao, studio ambayo.” Sentensi moja, ambaye, ambao, ambayo nyingi. Zile swaga za matamshi ya ki-B12. Huwa najionea kero kusikiliza redio mimi!
Ni muktadha huo wa kugandamiziana ndio ukasababisha redio zifunguliwe bila dira ya maudhui. Fulani mwenye hela, kaona redio fulani inakubalika, anaweka mzigo, anafungua ya kwake, halafu ananunua watangazaji na kuanzisha vipindi vinavyofanana na vile walivyokuwa wanafanya. Vilevile!
Matokeo yake, redio zinakuwa zinafanana. EFM waliamua kufanya tofauti na kuanzisha kipindi cha michezo asubuhi, Sports Headquarter, unasikia Wasafi FM nao wameanzisha Sports Arena, ileile asubuhi.
Watangazaji waliokuwa wanafanya Sports HQ ya EFM, wakiongozwa na Maulid Kitenge, ni haohao wamenunuliwa Wasafi kwenda kufanya Sports Arena. Kwa mantiki hiyo, Wasafii wameamua kununua ladha za EFM.
Miaka mitatu iliyopita kulitokea mapambano ya kununuliana watangazaji. EFM walifungua dirisha la usajili na kuzoazoa. Kipindi cha Power Breakfast cha Clouds FM, kikakong’otwa. Gerald Hando na Paul James ‘PJ’ walibebwa wazimawazima kwenda kufanya Joto la Asubuhi, EFM.
Ni kusema EFM waliona ujanja ni kununua ladha za Clouds FM hasa Power Breakfast. Clouds FM wakakataa unyonge, wakamrejesha PJ. Unajua nini? Clouds waliona eneo la kusoma magazeti palipwaya alipoondoka PJ. Wakamrejesha. EFM nao wakaona pigo. Maulid Kitenge, mtu wa michezo, akaziba pengo la kusoma magazeti. Na mashabiki akawapata!
Nini kinafuata? Majukumu mapya ambayo Kitenge amepewa na waajiri wake wapya, Wasafi, ni pamoja na kusoma magazeti. Utaona kuwa kipaji cha Kitenge cha kusoma magazeti ambacho kilipata nafasi kubwa EFM, ndicho kimetamaniwa na Wasafi.
Ukiwa mwanamahesabu mzuri, utagundua Wasafi asubuhi yote ni zao la EFM. Fanya kutoa na kujumlisha, gawanya na zidisha, jibu ni hilo, Wasafi ni EFM ya zamani. Jawabu ni kamili bila pointi za desimali.
Naomba nichambue jibu; Maulid ameondoka na kina Mwanaidi Suleiman pamoja na Yusuf Mkule. Hao walikuwa EFM. Ladha nzima imehamia EFM, itasikika hivyo.
EFM imepoteza ladha, itaingiza ladha tofauti. Kumbe sasa, Wasafi watakuwa na ladha ya zamani ya EFM, katika kipindi ambacho EFM itatengeneza ladha mpya!
Ni sawa na jinsi ambavyo EFM ilijimilikisha ladha ya zamani ya Clouds FM kupitia Hando na PJ. Wakati Clouds waliunda ladha tofauti walipomrejesha Masoud Kipanya, akaungana na Czer, Fredwaa na Barabara ambaye tangu na tangu, yupo tu!
PJ aliporejea Clouds FM na kurejesha ladha yake ya usomaji magazeti, EFM kupitia Kitenge walitambulisha ladha yao mpya. Hiyo ladha ambayo imeshazoeleka EFM, inakwenda Wasafi. Tukubaliane, Wasafi itakuwa Old EFM.
Wakati huohuo, EFM itatambulisha mfumo mpya wa usomaji magazeti bila Kitenge. Nini maana yake, EFM ambayo Ni redio ya zamani, inaweza kuwa na ladha mpya, wakati Wasafi itamiliki ladha ya kale ya EFM. Anyways, wanasema old is gold!
Unajua kwa nini hayo yanatokea? Jibu ni kuanzisha redio bila dira ya maudhui. Wawekezaji wanafikiria watu kuliko maudhui. Redio kuwa na majina yaleyale si vibaya, tatizo ni kuwekeza kwenye majina bila maudhui.
Ukianzisha redio kwa sababu umesikia redio fulani, utakachofanya ni kununua watangazaji wake ili redio yako iwe kama uliyoikuta.
Kumbe sasa, wawekezaji hawaanzishi redio kuleta ladha tofauti, bali wanakusudia kujifananisha na zilizopo. Uhondo ya EFM ni Leo Tena ya zamani ya Clouds FM, kipindi Dina Marios akitangaza. Dina yupo uhondoni EFM. Leo Tena ina ladha mpya Husna.
Jicho hilo la uwekezaji usio na ubunifu, inabidi mgogoro uwepo katika kugombea watangazaji.
Kitenge ni ladha zilipendwa ya Radio One. EFM walipoanzisha kipindi chao cha michezo saa 1 mpaka 2 usiku, waliiga ladha ya kale ya Spoti Leo ya Radio One. Ungewasikia Kitenge na Omar Katanga wakiunguruma. Hao walitokea Spoti Leo, Radio One.
Vipindi vilevile kasoro majina, saa zilezile, halafu inaitwa redio mpya wakati haina upya. Msemo uleule wa chupa mpya, mvinyo wa zamani. Uwekezaji gani huu?
Wawekezaji wa siku hizi kwenye vyombo vya habari, wanatengeneza mfumo wa ovyo, ionekane mtu akitaka kuanzisha redio, ajiandae kwa mamilioni ya kununua watangazaji wa redio nyingine.
Ukizitazama redio zilizopo na huduma zinazotoa, unaona kuna upungufu mkubwa wa kimaudhui. Nchi haihudumiwi inavyotakiwa na vyombo vya habari kwa sababu ya mitazamo ya majina kuliko maudhui.
Waje wawekezaji wenye kufikiria kuwahudumia Watanzania kwa namna tofauti. Huduma ya redio ina upungufu wa maudhui, maana zilizopo zinaigana.
Mpya zenye kuiga za zamani, zinakuwa kuukuu ghafla. Kama Wasafi, imekuwa kuukuu ikiwa ndani ya makaratasi yake.