Wapya Simba, Yanga wapangiwa siku yao

WATANI wa jadi Simba na Yanga wanatarajiwa kukutana kwa mara nyingine tena Septemba 25, kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii ambapo unatarajiwa kuchezwa saa 11:00 jioni kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Mchezo huo utakuwa ni mara ya tano kwa timu hizo kukutana kwa mwaka 2021 jambo ambalo ni rekodi kwa miamba hii miwili.

Mara mbili timu hizi zilikutana katika Ligi Kuu Tanzania Bara ambapo mchezo wa kwanza walitoka sare ya 0-0 kabla ya mchezo wa pili Yanga kushinda Julai 3 kwa bao 1-0.

Aidha timu hizi zilikutana pia katika Kombe la Mapinduzi Zanzibar na kisha Yanga kuondoka na taji la michuano hiyo kwenye mchezo wa fainali kwa ushindi wa mikwaju ya penalti.

Mchezo wa mwisho na wa kumbumbuka kwa timu hizi ulikuwa na mchezo wa fainali wa Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) ambapo Simba iliibuka na ushindi wa bao 1-0, bao la kiungo Taddeo Lwanga kwenye uwanja wa Lake Tanganyika Kigoma.


IMEANDIKWA NA DAUDI ELIBAHATI