Wapiga mbizi 238 kusaka bingwa wa taifa

Muktasari:
- Waogeleaji hao watatoka kwenye klabu mbalimbali zilizosajiliwa na Baraza la michezo pamoja na wanachama wa Chama cha kuogelea Tanzania (TSA).
WAOGELEAJI zaidi ya 238 wanatarajia kushiriki mashindano ya wazi ya klabu bingwa ya Taifa yaliyopangwa kufanyika siku mbili kuanzia kesho na keshokutwa kwenye bwawa la kuogelea la Shule ya Kimataifa ya Tanganyika (IST).
Waogeleaji hao watatoka kwenye klabu mbalimbali zilizosajiliwa na Baraza la michezo pamoja na wanachama wa Chama cha kuogelea Tanzania (TSA).
Akizungumza na Mwanaspoti, Katibu wa kamati ya maandalizi ya Chama cha kuogolea Tanzania (TSA), Michael Livingstone amesema kuwa wanatarajia waogeleaji zaidi ya 238 kushiriki katika mashindano hayo yanayotarajia kushirikisha pia waogeleaji kutoka nje ya Tanzania.
"Kigezo cha ushiriki ni waogeleaji watoke kwenye klabu zilizo sajiliwa na Baraza na watatakiwa kuwa wanachama wa TSA hatuwezi kushirikisha waogeleaji ambao hawatambuliki licha ya kutambulika kama mashindano ya wazi." Alisema
Livingstone alisema kuwa mashindano hayo yatashirikisha waogeleaji wenye umri kuanzia miaka nane (8) na wenye miaka 15 na zaidi huku akitaja baadhi ya klabu zilizotoa waogeleaji kuwa ni Dar, Bluefins, MIS, CR, Braebum Sharks, FK, Riptide, Premier, TALISS-IST, Pigec, MSC, BISA na Wahoo
Amesema kuwa kutakuwa na makundi manne ikiwa ni lile la umri wa miaka minane na 10, 11 mpaka 12, 13-14, na 15 ambapo muogeleaji atakayeibuka wa kwanza atapata pointi 20 huku wale wa pili na tatu watapata pointi 16 na 14 mtawalia.
“Waogeleaji watakaomaliza katika nafasi ya tatu za juu watapata vikombe kulingana na makundi yaliyopo ya umri, kutakuwa na medali. Haya ni mashindano ya TSA na yapo kwenye kalenda ya chama, hivyo waogeleaji wenye vigezo wanatakiwa kushiriki katika mashindano haya,” amesema.
Amesema staili nne za kuogelea zitashindaniwa katika mashindano hayo ambazo ni backstrokes, butterflies, individual medleys, breaststrokes kwa uogeleaji wa umbali wa juu mita 800, kati mita 400-200 na chini mita 50.