Wanaotuhumiwa kuuza tiketi feki wadakwa Zanzibar

Unguja. Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar (ZAECA) imekamata wauzaji tiketi kinyume na utaratibu wa mashindano ya Kombe la Mapinduzi ambayo fainali zake zinafanyika leo Jumatano Uwanja wa Amaan kisiwani hapa.

Waliokamatwa ni Obadian Ambukalo Mwatapala (28) Mkurugenzi wa Kampuni ya Unicust Technologies Limited na Aliya Mwakusalo ambaye ni Mtendaji wa kampuni hiyo pamoja na madalali wawili wa uuzaji tiketi hizo Baraka Mwaso Baraka (40) na Shadrack Khamis Juma (28).

Taarifa iliyotolewa na mamlaka hiyo imeeleza kuwa Kamati ya Mashindano iliingia mkataba wa utengenezaji tiketi kwa ajili ya mashindano ya Kombe la Mapinduzi na kampuni hiyo ambayo ilianza kutengeneza tiketi za ziada kinyume na utaratibu.

Imeeleza kuwa kamati ya mashindano imeingia hasara ya Sh 60 milioni ambapo kwa mechi moja pekee ya fainali kati ya Simba na Yanga imeokoa Sh 10 milioni.

"Watuhumiwa wote wamekamatwa na tayari  tunakamalisha mahojiano ili hatua za kisheria zichukuliwe juu yao, tunawaomba wadau wa michezo wote kununua tiketi kwenye vituo vilivyoanishwa na kusaidia kutoa taarifa kwa watu wanaouza tiketi kinyume na taratibu," imeeleza taarifa hiyo.