Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Waleteni hao tumalizane Taifa

Muktasari:

  • Tayari bingwa wa ligi hiyo ni Azam FC yenye pointi 59 ambayo leo inacheza na JKT Ruvu mechi ya kukamilisha ratiba kwani hata ikifungwa, hakuna kitakachobadilika.

WALETENI hao. Klabu za Yanga na Simba leo Jumamosi zinacheza mechi ya kufunga pazia la Ligi Kuu Bara msimu wa 2013/14, matokeo yoyote hayawezi kubadili jambo lolote katika msimamo wa ligi hiyo, lakini timu hizo zimetambiana kujenga heshima huku kila moja ikiona inachelewa kuingia uwanjani.

Tayari bingwa wa ligi hiyo ni Azam FC yenye pointi 59 ambayo leo inacheza na JKT Ruvu mechi ya kukamilisha ratiba kwani hata ikifungwa, hakuna kitakachobadilika. Yanga ipo nafasi ya pili ikiwa na pointi 55 ambazo haziwezi kufikiwa na timu nyingine iliyo chini yake, Mbeya City ipo nafasi ya tatu ikiwa na pointi 46.

Simba moja ya klabu kongwe nchini, yenyewe ina pointi 37 katika nafasi ya nne, ikifungwa inaweza kujiweka katika nafasi hata ya kushika nafasi ya sita kwani Kagera Sugar na Ruvu Shooting zinaweza kufikisha pointi 38 kutoka 35 walizonazo, hivyo Wekundu wa Msimbazi wana kila sababu ya kuhakikisha wanafanya vizuri kulinda heshima.

Yanga ambao ni mwenyeji wa mchezo huu, tayari imehamisha kambi yake kutoka Kunduchi hadi katikati ya jiji la Dar es Salaam na kujichimbia katika moja ya hoteli jana Ijumaa jioni. Timu hiyo iliyo chini ya Kocha Hans Van Der Pluijm ilikuwa ikijifua katika Uwanja wa Boko Veteran kwa mazoezi ya mara moja kwa siku.

Chini ya Pluijm, Yanga leo itaambulia medali tu katika mchezo wa leo hata kama ikifungwa na watani wao baada ya kujihakikishia kushika nafasi ya pili, lakini kama hilo halitoshi kukata kiu yao, kubwa ni kutaka kuwanyamazisha Simba ili kuthibitisha ubora wao.

Akizungumzia maandalizi yao, Pluijm alisema: “Tunaweza kuwa na wakati mzuri wa maandalizi lakini inapokuja mechi wachezaji wakafanya tofauti, sitegemei hilo kutokea.’’

Tambwe, Messi chini ya ulinzi

Pluijm alisema amezungumza na mabeki wake kutofanya makosa ya kuwasahau kiungo mshambuliaji Ramadhan Singano ‘Messi’ na mshambuliaji, Amissi Tambwe kwani walikuwa mwiba mkali kwao katika mchezo wa Nani Mtani Jembe Desemba mwaka jana ambapo Yanga ilipokea kipigo cha mabao 3-1.

“Siku zote sitaki kuona nikiwapa presha wachezaji wangu kwa kuwaambia nani achungwe, lakini nimewaambia tunahitaji kuwa makini na wachezaji hao (Messi na Tambwe), nimeyaona makali yao lakini kama tutacheza kwa kufuata mbinu zetu hakuna kibaya kitakachotokea, najua mpira ni mchezo wa makosa lakini sitarajii makosa ya kizembe kutokea,” alisema Pluijm raia wa Uholanzi.

Simba yahama uwanja Zanzibar

Kambi ya Simba ilikuwa Zanzibar na kikosi chake kilikuwa kinafanya mazoezi Uwanja wa Fuoni, lakini ililazimika kuhamia Uwanja wa Amaan kwa mazoezi hayo baada ya mvua kunyesha na kuharibu sehemu ya kuchezea ‘pitch’.

Juzi Alhamisi na jana, Simba chini ya kocha Zdravko Logarusic ilikuwa ikifanya mazoezi kwa dakika 180 kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 5:00 asubuhi lengo likiwa ni kujiweka fiti kwa mchezo wa leo Jumamosi.

Kikosi kamili cha Simba kilitarajiwa kurejea Dar es Salaam, jana jioni tayari kwa kuivaa Yanga Uwanja wa Taifa ambao una nyasi asilia tofauti na zile za Amaan.

Katika mazoezi ya timu hiyo, chini ya Logarusic aliyeonekana kuwa mkali kuliko wakati wowote, dhamira ikiwa ni kutaka kuiona Simba ikiibuka na ushindi..

“Tunawaheshimu Yanga kuanzia kocha wao na hata wachezaji, tunataka kushinda mechi hiyo lengo likiwa ni kutaka kuwafariji mashabiki wetu, tukicheza kwa nidhamu yetu tunaweza kushinda lakini tunatakiwa kuwa makini kutokana na aina ya timu tutakayocheza nayo,” alisema Logarusic raia wa Croatia.  

Rekodi

Katika mechi tano zilizopita, Yanga ilionekana kuwa vizuri baada ya kushinda mechi mbili, kuanzia Machi 5, 2011 wakongwe hawa walipokutana siku hiyo mechi ilimalizika kwa sare ya bao 1-1, wakakutana tena Oktoba 29 mwaka huo na Yanga wakaibuka washindi kwa ushindi wa bao 1-0.

Simba iliamka kwa kishindo Mei, 6, 2012 baada ya kuwashushia kipigo watani wao kwa ushindi wa mabao 5-0 ambao bado unawatesa Yanga mpaka sasa, kama huamini hilo onyesha kiganja chako kwa shabiki wa Yanga usikie majibu yake.

Hawakuishia hapo walikutana tena Oktoba 3, mwaka huo, mchezo ulimazika kwa sare ya bao 1-1, Yanga waliamka tena Mei, 18, 2013 wakafunga msimu kifua mbele kwa ushindi wa mabao 2-0 kabla ya kukutana tena Oktoba, 20 mwaka huo na kutoshana nguvu kwa sare ya mabao 3-3.

Mwisho hata kama haikuwa mechi ya ligi kama zilizotangulia watani hawa wa jadi walikutana tena Desemba 22, mwaka jana na Simba iliibuka na ushindi wa 3-1 katika mchezo wa kirafiki ulioandaliwa na mdhamini wao, Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) uliopewa jina la Nani Mtani Jembe.

Mwamuzi mwanajeshi

Mwamuzi ni Dominic Nyamisana kutoka Dodoma, ni mwanajeshi wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Atasaidiwa na Jesse Erasmo na Charles Simon. Kwa Nyamisana hii ni mara yake ya kwanza kuwachzesha watani wa jadi. Mwamuzi wa akiba ni Hashim Abdallah.

Uchaguzi tishio kwa wachezaji

 Timu zote hizi zitaingia katika harakati za uchaguzi wa viongozi wao kuanzia mwezi ujao, hilo limekuwa tishio kubwa kwa wachezaji wa timu zote na tayari kuna taarifa kwamba mchezaji yeyote atakayefanya vibaya au mchezo mchafu na kusababisha timu yake kufungwa kirahisi, anaweza kujiweka katika wakati mgumu kuvaa jezi ya timu hiyo msimu ujao.

Vikosi hatari hivi hapa

Kwa vyovyote Yanga leo Jumamosi inatarajiwa kuwakilishwa na: Deo Munish ‘Dida’, Mbuyu Twite, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kelvin Yondani, Frank Domayo, Simon Msuva, Hassan Dilunga, Didier Kavumbagu, Mrisho Ngassa na Hamis Kiiza.

Simba: Ivo Mapunda, Nassoro Masoud ‘Chollo’, Issa Rashid ‘Baba Ubaya’, Joseph Owino, Donald Mosoti, Jonas Mkude, Ramadhan Singano ‘Messi’, Said Ndemla, Amissi Tambwe, Amri Kiemba na Horoun Chanongo.

Hatma ya mikataba ya makocha

Makocha wote, Pluijm na Logarusic wanamalizia mechi yao ya mwisho katika ajira za miezi sita walizoingia mwanzoni mwa mzunguko wa pili wa ligi hiyo.

Tayari imeshaelezwa kuwa atakayeibuka na ushindi mechi hii anaweza kuwa katika nafasi nzuri ya kupatiwa mkataba wa muda mrefu hali ambayo inaongeza ugumu kwa kuwa hakuna kocha atakayekubali kirahisi timu yake ifungwe.

Burudani kwa buku saba tu

Mashabiki watakaokwenda kushuhudia mchezo wa Simba na Yanga watatakiwa kulipa Sh. 7,000 kwa viti vya bluu na kijani, Sh. 10,000 viti vya rangi ya chungwa, Sh. 20,000 kwa VIP C na B wakati VIP A kiingili kitakuwa Sh. 30,000.

Vita ya kushuka daraja

Mechi kali za leo ni mbili tu, Yanga na Simba ambazo zinasaka heshima tu lakini Uwanja wa Jamhuri Morogoro nyasi zake zitawaka moto kwa kuzishuhudia Prisons na Ashanti United zikicheza kati yao kuwania nafasi ya kubaki ligi kuu.

Ashanti na Prisons zote zina pointi 25 katika mechi 25 zilizocheza, hivyo timu itakayofungwa itakuwa imeshuka daraja lakini zikipata sare ya kufanana, ni ama Ashanti itashuka kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa au Mgambo itakuwa katika wakati mgumu na huenda ikashuka kama haitoshinda mechi yake na Mbeya City.

Mechi nyingine

Michezo mingine itakayochezwa leo Jumamosi ni kati ya Rhino Rangers na Ruvu Shooting (Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora), Mbeya City na Mgambo Shooting (Uwanja wa Sokoine, Mbeya), Oljoro JKT na Mtibwa Sugar (Uwanja wa Sheikh Kaluta Amri Abeid, Arusha) na Coastal Union na Kagera Sugar Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.