Wagosi wa Kaya waipania Yanga

WAKATI kocha Cedric Kaze akipiga hesabu za kuvuna alama tatu kwenye mechi yao ya ugenini jijini Tanga, wenyeji wao Wagosi wa Kaya, wamechimba mkwara mapema kwamba Yanga wasitarajie mteremko katika mchezo huo wa Ligi Kuu Bara utakaopigwa Uwanja wa Mkwakwani.

Nyota wa Coastal Union, wamedai kuwa kupoteza kwao dhidi ya JKT Tanzania kumewapa hasira za kuimaliza Yanga watakaovaana nao Machi 4.

Mmoja ya nyota hao, beki Hans Masoud amesema kupoteza mchezo wao wa juzi dhidi ya JKT Tanzania, imeongeza presha kikosini, huku akisisitiza mchezo ujao na Yanga, lazima kieleweke.

Coastal Union katika msimu uliopita ilikuwa na matokeo mazuri ikimaliza nafasi ya nne, lakini kwa sasa hali imeonekana kuwa ngumu kwani inashika nafasi ya 13 kwa pointi 23 na kuwa miongoni mwa timu zinazokwepa kushuka daraja.

Juzi timu hiyo inayonolewa na Juma Mgunda, ikiwa jijini Dodoma ilijikuta ikichezea kipigo cha mabao 2-0, matokeo ambayo yanaongeza presha kabla ya kuwavaa Yanga katika mchezo ujao.

Masoud alisema matokeo hayo si rafiki kwao ukizingatia timu nne zinapaswa kushuka daraja na kwamba kwa sasa hesabu zao zinahamia kwenye mechi ijayo dhidi ya Yanga.

Alisema makosa waliyoyafanya na kujikuta wakilala kwa kichapo hicho, anaamini benchi la ufundi liliona wapi waliokosea, hivyo mchezo ujao lazima wafanye kweli.

“Matokeo siyo mazuri kiujumla, lazima tujipange upya na mchezo ujao dhidi ya Yanga ambapo tutakuwa nyumbani, kocha atakuwa aliona wapi tulikosea ili kusahihisha,” alisema Masoud.

Nyota huyo wa zamani wa Alliance FC, aliongeza kuwa pamoja na hali waliyonayo hawatakata tamaa wala kuchoka, isipokuwa matumaini yao ni kumaliza ligi nafasi nzuri.

Beki huyo alisema ushindani umekuwa mkali sana hasa kwa timu zinazopambana kushuka daraja na kwamba malengo yao ni kusaka ushindi kwa mechi zilizobaki ikiwamo ya Kombe la Shirikisho la Azam dhidi ya Ihefu.

“Baada ya mechi yetu ya Ihefu ndio tunaingia kwenye kazi rasmi kuwakaribisha Yanga, hatutakuwa na mzaha katika michezo iliyobaki kutokana na presha iliyopo,” alisema Kinda huyo.

Mara ya mwisho kwa timu hizo kukutana jijini Tanga, zilishindwa kufungana kwa kutoka suluhu katika mchezo wa ligi ya msimu uliopita na katika mechi ya kwanza msimu huu Yanga ilishinda jijini Dar kwa mabao 3-0.