Huyo Sarpong mazoezini balaa!

Sarpong anauzwa, inaletwa mashine nyingine Yanga

YANGA wanachanganyikiwa na ufanisi wa safu yao ya ushambuliaji, kwani imekuwa ikishindwa kuzalisha mabao ya kutoshwa kwenye mechi, lakini kitu cha ajabu ni kwamba mastraika wao wanapokuwa mazoezini ni balaa kwa kucheka na nyavu.

Ipo hivi. Mshambuliaji aliyekumbwa na ukame wa mabao ni Michael Sarpong ambaye mara ya mwisho mashabiki kushangilia bao lake ni walipotoa sare ya bao 1-1 dhidi ya Simba, mechi iliyopigwa Novemba 7, lakini sasa unaambiwa huko mazoezini hashikiki.

Katika mazoezi ya juzi jioni kule katika kambi yao iliyopo Kigamboni, Sarpong amekuwa ni moto mkali akiwapa wakati mgumu makipa wawili wanaopishana katika lango la timu hiyo Metacha Mnata na Faruk Shikhalo.

Mazoezi hayo Sarpong alianza na Mnata kwanza akampiga bao kali akifanikiwa kuwazidi akili mabeki wake huku kipa huyo akionekana kama kushtukizwa na akili ya mshambuliaji huyo ambaye aliupeleka mpira chini kwa shuti la hesabu kali.

Hakuishia hapo jamaa akafanya kweli tena akimfunga mara mbili safari hii akiwa Shikhalo kwa mabao ya mashuti makali.

Sarpong katika mazoezi hayo ndio alikuwa mfungaji bora akifunga mara tatu huku akifuatiwa na Ditram Nchimbi ambaye naye mara ya mwisho kufunga ilikuwa ni msimu uliopita akikaribia kutimiza mwaka bila kufunga katika ligi.


Msikie Shikhalo

Akizungumzia kiwango cha Sarpong, Shikhalo alisema kinachotokea kwa mshambuliaji wao huyo ni bahati mbaya lakini haina maana ni mchezaji mbovu.

Shikhalo alisema siku ambayo Sarpong atafunga katika mechi litakuwa bao muhimu kwake ambalo linaweza kumshusha presha kutokana na ukame ambao umemkuta wa mabao na kwamba mashabiki waendelee kumuamini.

“Mazoezini anafanya vizuri karibu washambuliaji wote wanafanya vizuri mazoezini lakini bahati mbaya wamekuwa na ukame huo katika mechi, hata Sarpong amekuwa bora sana mazoezini,” alisema kipa huyo raia wa Kenya.