WABISHI: Wazawa walioamua kukomaa
Muktasari:
- Mfungaji Bora msimu uliopita ni Amissi Tambwe ambaye mpaka sasa ana mabao saba, akiwa nyuma ya Kichuya lakini raia huyo wa Burundi licha ya kasi yake ya kufunga amekabwa koo na wazawa wanaokula naye sahani moja.
NANI alikuwa akijua kuwa mgombea wa Republican, Donald Trump angeshinda kiti cha urais wa Marekani katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika wiki iliyopita? Hakuna aliyekuwa akimpa nafasi kutokana na sera zake tata, lakini wapigakura walitumia nafasi yao kumpa urais akiwa Rais wa 45 wa taifa hilo kubwa.
Vivyo hivyo katika Ligi Kuu Bara iliyokamilisha duru lake la kwanza wiki iliyopita, hakuna aliyetarajia kama Shiza Kichuya angeweza kuwafunika nyota wa kimataifa katika mbio za ufungaji.
Duru hilo la limemalizika likiwa na sura tofauti, kubwa ikiwa ni mapinduzi makubwa yaliyojitokeza kwa wazawa kukabana koo na wageni katika hatua mbalimbali.
UFUNGAJI
Hatua ya kwanza ya mageuzi ni katika msimamo wa wafungaji na mpaka sasa kinara wa mabao ni winga teleza, Kichuya akiwa na mabao tisa.
Kichuya nyota yake ilianza kung’aa mapema kwa kutangulia kuanza kupindua karata muhimu katika kikosi chake cha Simba kwa kumpoteza Laudit Mavugo aliyekuwa na jina kubwa, lakini staa huyo aliyetokea Mtibwa alionekana kuwa na msaada zaidi kuliko Mrundi huyo.
Akiwa Simba, Kichuya ambaye ni fundi wa anayetumia mguu wake wa kushoto akifunga pasipo kutarajiwa, pia ndiye kinara wa mabao na hata kwenye mechi ambazo alikuwa akifichwa na mabeki pinzanil Simba ilionekana jinsi ilivyokuwa ikiyumba kupata ushindi.
TAMBWE AKABWA KOO
Mfungaji Bora msimu uliopita ni Amissi Tambwe ambaye mpaka sasa ana mabao saba, akiwa nyuma ya Kichuya lakini raia huyo wa Burundi licha ya kasi yake ya kufunga amekabwa koo na wazawa wanaokula naye sahani moja. Simona Msuva na Rashid Mandawa wamemng’ang’ania akilingana nao mabao kitu ambacho siyo cha kawaida kwa Mrundi huyo.
Hata hivyo, utamu zaidi ni kwamba katika tano bora ya ufungaji kuna jina moja tu la staa wa kigeni nalo ni Tambwe, ambaye amezingirwa na wazawa watupu akiwemo nahodha wa Azam, John Bocco na Abdulrahman Mussa wa Ruvu Shooting walio na mabao sita kila mmoja kisha kufuatiwa na orodha ndefu ya wenye mabao matano.
NDUSHA HOI KWA MO, MZAMIRU
Simba bado inaendeleza mapinduzi ambapo licha ya kibali chake kuchelewa kiungo raia wa DR Congo, Mussa Ndusha ameshindwa kupenya katika mafundi Mzamiru Yassin aliyeliteka dimba la juu katika kikosi cha timu hiyo ambapo hata kama kuna kiungo akitoka bado jicho la Kocha, Joseph Omog litaangukia kwa mzawa mwingine, Mohamed Ibrahim ‘MO’. Haitashangaza endapo Simba itaamua kumpiga chini Ndusha na nafasi yake kuchukuliwa na mchezaji mwingine.
BOCCO NAYE MBISHI
Azam FC licha ya ujio wa makocha wa kigeni kutoka Hispania ambao inadaiwa hawakuwa wakivutiwa na nahodha, Bocco, lakini makocha hao wamelazimika kumkubali kwa shingo upande na bahati nzuri amewabeba kwelikweli kwani alikuwa akifunga mabao muhimu kama kawaida yake.
Bocco aliwazidi kete mpaka wageni akiwamo Francisco Zukumbawira mwenye mabao matatu ambaye amezidiwa hata na kinda, Shaaban Idd mwenye mabao manne.
CHIDIEBELE APINDULIWA STAND
Stand United ‘Chama la Wana’, nako mgeni Abaslim Chidiebele ameshindwa kuonyesha kile kilichotarajiwa. Raia huyo wa Nigeria amefunikwa na wazawa na amemezwa na mkongwe Adam Kingwande na Pastory Athanas wenye mabao mawili kila mmoja katika kikosi hicho.
MABEKI KAZI IPO
Katika ulinzi nako mambo yanaonekana kuwa magumu ambapo ukianza na kikosi cha Yanga wazawa, Andrew Vincent ‘Dante’ na Kelvin Yondani wameonekana kumkaba koo Vincent Bossou raia wa Togo wakipishana katika kuitumikia safu ya ulinzi ya timu hiyo wakimfichia aibu nahodha wao, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ ambaye bado hajafanikiwa kurudisha makali yake. Wakati mambo yakiwa hivyo kwa Yanga, Simba nako kazi kama hiyo imekuwa ikifanyika kwa Novatus Lufunga kufanikiwa kumweka nje Juuko Murshid wa Uganda, licha ya beki huyo kuwa katika kikosi cha panga pangua cha taifa lake kitakachoshiriki Fainali za Kombe la Mataifa Huru Afrika mwakani.
Azam nako bado mpaka sasa hakujajulikana hatma ya mkongwe Pascal Wawa akiendelea kusota nje licha ya kupona majeraha yake akiwashuhudia wazawa Aggrey Morris na David Mwantika wakiongoza ukuta wa timu hiyo.