Wabishi kinoma Nature, Mwana FA hawakwami popote

Muktasari:
Mwanaspoti linakuletea wasanii wa kiume ambao wamedumu kwenye game kwa muda mrefu na kila wanapotoa ngoma inahit licha ya misoto na changamoto nyingi za muziki.
UNAWEZA kujiuliza kwanini wasanii wengi wa Bongo Fleva wanakuja na kupotea kirahisi kwenye muziki na kukosa majibu ya kueleweka? Lakini wakati huohuo inabidi ujiulize kwanini washikaji wengine hawapotei kwenye game?
Wasanii wengi ambao hawapotei ni kutokana na namna ambavyo wanafanya kazi zao kwa kusikilizia upepo unavyokwenda na wanapoachia ngoma, basi hutamba kinoma.
Mwanaspoti linakuletea wasanii wa kiume ambao wamedumu kwenye game kwa muda mrefu na kila wanapotoa ngoma inahit licha ya misoto na changamoto nyingi za muziki.
PROFESA JAY
Ukiwa bungeni ukasikia jina Joseph Haule limetajwa, basi fahamu kuwa huyo ni Mzazi wa Bongo Fleva anayewakilisha wananchi wa Jimbo la Mikumi huko mjengoni, Profesa Jay huyu ni wa miaka ya 90, ambapo aliunda Kundi la ‘Hard Blasters Crew’ (HBC). Baada ya hapo alisimama na vibao vyake kama ‘Ndiyo Mzee’, Piga Makofi, Bongo Dar es Salaam, Msinitenge, Zali la Mentali na vingine vingi jambo ambalo lilibadilisha fikra za wengi kuwa muziki sio uhuni. Mpaka sasa Prof Jay bado anapiga mashuti kwa miguu yote kwa maana ya bungeni yupo na bado kwenye muziki anawasha moto.
Katika kuhakikisha hilo Mzee wa Mitulinga kama ambavyo anavyojiita, aliachia ngoma na Harmonize akiwa mjengoni inayojulikana kama Yatakwisha, akizungumzia changamoto zinazoikabili jamii.
Fid Q
Jamaa inaelezwa kuwa alianza kujiingiza kwenye game miaka ya 90. Huyu ni Farid Kubanda a.k.a Fid Q, ambaye mwaka 2000 alitoa ngoma yake ya kwanza ya ‘Huyu na Yule’ kwa kumshirikisha Mr Paul. Ngoma hiyo ilifanywa kwenye Studio za MJ Records chini ya Master Jay.
Baada ya hapo Fid Q alifiti kwenye sanaa ya muziki kwa kutoa ngoma kali zilizomfanya kutamba na kuwepo mpaka sasa. Yaani alikuwepo, yupo na ataendelea kuwepo hadi Agosti 13, mwaka huu ambayo ni mfano wa siku yake ya kuzaliwa, Ngosha ameachia albamu yake ya tatu ya KitaaOrojia yenye mikwaju 23 ikiwa na sauti za mastaa kibao.
Licha ya Fid Q kuwa kimya kwa muda mrefu, lakini kila anapoibuka na kuachia ngoma ni lazima ibambe na sasa taarifa za kunyapianyapia ni kwamba, jamaa yuko mafichoni anapika ngoma mpya.
Hakuna kinachombeba Fid Q zaidi ya ngoma zake kusheheni mashairi yenye maudhui yanayoishi na kugusa maisha ya watu na ndio sababu zimeendelea kubamba.
MR. BLUE
Miaka ya 2000 jina la Mr Blue lilianza kuchomoza kwenye anga ya Bongo Fleva. Ukiacha ngoma lakini, pia alitambulishwa vyema na staili yake ya mavazi na baada ya ngoma hiyo akashusha ile ya Mapozi. Baada ya hapo, gari la ‘Babilon Bycer’ lilikata breki na ngoma zikaanza kumwagika na mashabiki wote wakaanza kuliimba jina lake tu.
Jamaa huyu wa Micharazo Family utamueleza nini kwani, kwa jinsi anavyobadilika kulingana na mahitaji ya muziki na mashabiki zake, basi tuendelee kunywa mtori nyama tutazikuta chini.
Na sasa Mr Blue kutoka staili ya kunatanata hadi Mboga Saba ambayo alikaa muda mrefu kwenye ramani ya Bongo Fleva.
DULLY SYKES
Kibongobongo Dully Sykes ndio King wa Bongo Fleva licha ya ukongwe wake bado yupo sana kwenye sanaa.
Miaka ya 2000 alianza kutamba na ngoma zake kama Julieta, Salome, Historia ya Kweli, Kijakazi na Leah lakini ameendelea kukaza mpaka sasa yupo hewani na ngoma ya ‘Nikomeshe’ aliyomshirikisha Harmonize na inatamba kinoma.
CHEGE
Mkali huyu alijulikana sana miaka ya 2000 wakati wa Kundi la ‘TMK Wanaume Family’ tangu hapo mwanaume huyu hajawahi kupoa hata baada ya kuvunjika kwa kundi hilo.
Chege ameendelea kuuwasha moto kivyakevyake na wakati mwingine kushirikiana na swahiba wake, Mhe. Temba. Kwa sasa anatamba na ngoma mpya ya ‘Wyper’ aliyofanya na mkali kutoka Tanga, Roma Mkatoliki.
Chege naye amekuwa mtu wa kusikilizia ngoma zake, kwani amekuwa akiwasoma wasanii wa sasa wanafanya nini ndipo naye anaibuka na kuachia pini kisha anatulia tena.
AY
‘Raha Kamili’ na ‘Machoni kama watu’, hizi ni baadhi ya ngoma zilizomtambulisha vizuri kwenye Bongo Fleva. Anaitwa Ambwene Yessaya ‘AY’.
Mwanzoni mwa miaka ya 2000, alikua mmoja kati ya watu waliounda Kundi la East Coast Team lililoongozwa na Gwamaka Kaihula ‘King Crazy GK’, na mwenzake Khamis Mwinjuma a.k.a Mwana FA. Kwa sasa mkali huyo bado yupo sokoni na ngoma yake ya mwisho ‘Safari’ aliyomshirikisha mkongwe King Kiki.
Katika wimbo huu amezungumzia namna ambavyo watu wanapambana kutafuta maisha, lakini wanatakiwa wasisimame kutokana na kwamba hawajafika mwisho wa safari.
MWANA FA
“Miluzi mingi ila kubwa la mbwa sipotei,” huu ni mstari kwenye ngoma yake mpya ya ‘We Endelea Tu’, na ni dhahiri kuwa Binamu hajapotea kwenye game tangu siku alipoingia.
Mwana FA ana ngoma zaidi ya 50 na zote zimefanya vizuri sokoni tangu miaka ya 2000 na mpaka sasa anaendelea tu.
MADEE
‘Kazi yake Mola’ ndiyo ngoma iliyomtambulisha Madee a.k.a Rais wa Manzese. Nani haifahamu Tip Top Connection ambayo imewatoa wana kibao na mpaka sasa wengine wanakomaa tu. Baada ya ngoma hiyo, Madee akashusha ngoma mpya kibao ikiwemo lile swali la Hip Hop inauza ama haiuzi?. Wenzake walimponda sana, lakini ndani ya ngoma ile Madee alifikisha ujumbe ambao baadaye ukweli ulijulikana hadharani tu.
Madee hakupotea katika badala yake alikaa kwenye ramani na kung’ang’ania kwenye muziki mpaka sasa, ambapo anatamba na ngoma ya ‘Wacha Waongee’.
JUMA NATURE
Hakuna shaka kuhusu ukomavu wake, huyu ndiye msanii pekee wa Bongo Fleva aliyeweka historia ya kujaza Ukumbi wa Diamond Jubilee katika shoo yake mwaka 2003 wakati akizindua albamu yake ya ‘Ugali’.
Haihitaji kupepesa macho kumtaja ‘Kiroboto’ kuwa mkali wa muda wote kwani kila anapofanya tamasha mashabiki wa aina zote hupiga shangwe na kulipuka mwanzo mwisho.
Amekuwa ni mtu wa kusikilizia kuachia nyimbo, anaweza akatoa wimbo mmoja kwa mwaka lakini akahusika katika wimbo za wasanii wengine kama ilivyokuwa kwa Kiboko ya Mabishoo ya Harmorapa.
JOH MAKINI
Huu ni Mwamba wa Kaskazini ambao haujawahi kutikisika tangu mwanzoni mwa miaka ya 2000.
Hao, popote chochote, stimu zimelipiwa na ngoma nyingine kali ni utambulisho halisi wa Joh Makini kwenye muziki.
Joh Makini, ambaye pia anaunda kundi la Weusi amethibitisha umwamba wake kwa kudumu kwenye game zaidi ya miaka 15.
Mpaka sasa huwezi kutaja marapa watano bora ukamsahau huyu jamaa anayetamba na kibao chake cha ‘Mchele’ alichomshirikisha Young Lunya kutoka OMG.