Vita ya usajili, Klabu Ligi Kuu Kenya zagombea wachezaji

ASA hivi sakata kubwa la uhamisho linaloendelea linamuhusisha nyota Lionel Messi. Messi ameweka wazi kuwa anataka kuitoka Barcelona ila klabu hiyo imemgandia.
Messi anajaribu kuondoka kwa kutumia kipengele kwenye mkataba wake ambao unamruhusu kuondoka akiwa mchezaji huru kama akitaka licha ya kuwa kasalia na mwaka mmoja kwenye mktaba huo na Barcelona.
Hata hivyo klabu yake imegoma kumwachia ikisema kuwa kipengele hicho kilimpa uhuru huo Messi hadi kufikia Juni 10 na kwa kuwa muda umepita hawezi kuondoka. Mawikili wa Messi nao wanahoji kuwa kipengelea hicho hakingeweza kutumika kwa sababu msimu ulisita kutokana na janga la Corona na kurejea baada ya Juni 10.
Huku vuta nikuvute hiyo ikiendelea, Shirikisho la soka Uhispania La Liga nalo limeikingia Barcelona kwa kusema kuwa halitakubali kumpa cheti cha kuondoka Messi kama mchezaji huru. Hivyo kama anataka kuondoka basi ni lazima klabu inayomtaka iwasilishe dau la Euro 700 milioni ili kuvunja kipengele cha mktaba wake huo.
Vuta ni kuvute hiyo ilimpelekea Messi kususia kujiunga na wachezaji wenzake kupimwa Corona juzi Jumapili kabla ya msimu kuanza.
Mtafaruku kama wa Messi ambapo klabu zimeonekana zikigombania mchezaji au mchezaji akizozana na klabu ikiwa imegoma kumwachilia aondoke, pia imeshuhudia katika ligi yetu. Hawa hapa wachezaji waliowahi kujipata kwenye hali kama hiyo ya kuvutana na klabu au klabu mbili kumng’ang’ania.

PETER THIONG’O
AFC LEOPARDS Vs KAKAMEGA HOMEBOYZ
Wing’a huyu chipukizi mwenye miaka 20 licha ya kuonyesha nia ya kuondoka katika klabu yake ya Kakamega Homeboyz, mdosi wa klabu hiyo Cleophas Shimanyula amekuwa akimng’ang’ania.
Hii ni licha ya kuwa mktaba wake unamalizika Oktoba 2020. Kumeshuhudiwa majibizano makali ya maneno kati ya Shimanyula na mwenyekiti wa Ingwe, Dan Shikanda kuhusiana na usajili wa Thiong’o.
Shimanyula amekuwa akiwakashifu Ingwe kwa kuwa na tabia ya kuvuruga wachezaji wa timu zingine mikataba yao inapokaribia kuisha bila ya kuzungumza na klabu zao husika.
Kulingana naye Ingwe hawana fedha za kufanya usajili wa wachezaji na ndio sababu wamekuwa na tabia  hizi.
Lakini akimjibu Shikanda alisisitiza kuwa wana pesa za kutosha kufanya usajili ila Shimanyula ndio hakuwa tayari kusikiza ofa yao.
Na huku Thiong’o akiwa amesalia na miezi miwili kwenye mktaba wake na Homeboyz, Ingwe ilimshawishi kusaini Pre-contract ya miaka miwili nao. Hii ina maana kuwa atajiunga nao kama mchezaji huru mara tu mkataba wake na Kakamega utafikia kikomo. Thiong’o alishawishiwa kutumia njia hii baada ya Kakamega kuganda kumwachia kwa nia nzuri kutokana na malumbano hayo ya mabosi wao.

JOHN AVIIRE
SOFAPAKA Vs TANTA FC (Misri)
Vuta nikuvute kati ya Sofapaka na  klabu ya Tanta kuhusiana na usajili wa straika chipukizi Aviire umedumu kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa.
Aviire aliondoka pasi na kuiambia klabu yake na kwenda kujiunga na Tanta FC, mkataba wake na Sofapaka ukiwa ungali na mwaka mzima.
Aviire alitumia kipengele cha kutolipwa mshahara wake kwa miezi mitatu kama njia ya kuikacha Sofapaka.
Alipoomba cheti cha uhamisho, Sofapaka iligoma kumpa huku ikisisitiza kuwa ni lazima Tanta itoe dau la Sh10 milioni ndiposa impe cheti hicho mchezaji huyo ili aweze kujiunga nao.
Hata hivyo Tanta haikuwa tayari kutoa dau hiloikisisitiza kwamba Sofapaka ilishindwa kumlipa mchezaji huyo mshahara wake kwa miezi mitatu na ndio sababu yake ya kutaka kuondoka. Ilipoona Sofapaka imegoma kumwachia, iliandikia FIFA barua ikijieleza na mara moja ikapokeza barua ya uhamisho na kuweza kumsajili Aviire. Hatua hiyo ikawapiga Sofapaka stopu na kumwacha mumiliki wake Elly Kalekwa akidai kaibiwa mchezaji kimabavu.

VINCENT OBURU
GOR MAHIA Vs AFC LEOPARDS
Straika Oburu akiwa na miaka 20, 2017 aliwagonganisha vichwa mashemeji hao baada ya kusaini mikataba miwili na klabu hizo.
Oburu aliibukia kutoka kikosi cha Ingwe U20 baada ya kushiriki ligi ya chipukizi na kutisha sana. Baadaye Gor ikatangaza kumsajili kwa mkataba wa miaka minne  huku nao mashemejio Ingwe wakitangaza kuwa dogo kasaini mktaba na kujiunga na timu ya kwanza.
Gor ilisisitiza kuwa imemsajili baada ya mkataba wake na Ingwe kumalizika, lakini AFC walisisitiza kwamba alikuwa tayari kasaini mkataba wa miaka mitatu nao.
Kesi hiyo ikaishia kwenye Kamati ya kinidhamu ya Shirikisho la soka nchini FKF ambapo ilidhibitika kwamba ni kweli Oburu alikuwa kasaini mikataba miwili. Aliadhibiwa kwa kufutwa kwenye sajili ya wachezaji wa ligi kuu ya KPL.
Hata hivyo Gor iliamua kuachana na kesi hiyo na hivyo kuondoa mashtaka yote dhidi yake na hapo akaweza kujiunga na Ingwe. Aliyoichezea hadi mapema mwezi huu alipoondoka na kujiunga na Wazito.

DAVID MAJAK
KAKAMEGA HOMEBOYZ Vs TUSKER FC
Mwaka jana kulizuka mtafauruku kuhusu uhamisho wa straika huyu twiga raia wa Sudan Kusini. Baada ya kuibuka mfungaji bora kwenye dimba la Chapa Dimba 2018, Homeboyz walimsaini kwa mkataba mfupi. Ulipomalizika Majak anasema Homeboyz walisileki kumpa mkataba mwingine na hapo akaamua kujiunga na Mt Kenya United na kisha baadaye akagura na kujiunga na Tusker.
Kulingana na Majak, Homeboyz walianza kulalamika kuwa ni mchezaji wao, baada ya kuisaidia Tusker FC kuwachapa magoli 3-0 kwenye mechi ya ligi kuu.
Katika malalamishi yao, mwenyekiti wa Homeboyz, Shimanyula alidai kuwa Majak alitumia majina tofauti aliposainiwa na klabu yake akisema alijitambulisha kama John Doul Tot.
Licha ya kuwasilisha kesi mbele ya FKF, chombo hicho kilisema hakina uwezo wa kufanya uchunguzi kuhusiana na madai ya Homeboyz na kuiomba iwasilishe malalamishi yao katika idara ya upelelezi. Kipindi hicho Homeboyz ilikuwa ikitaka Majak afungiwe kucheza soka ikiwemo klabu ya Tusker kuekewa vikwazo vya kufanya usajili. Hata hivyo  kufuatia majibu ya FKF, Homeboyz ilichorea stori na kuachia stori hiyo ilale. Majak angali akiichezea Tusker.

LAWRENCE OTIENO OLUNGA
KAKAMEGA HOMEBOYZ Vs KARIOBANGI SHARKS
Kwa mara nyingine, Homeboyz walijikuta wakizozana na Sharks Septemba 2019 kuhusu usajili wa fowadi chipukizi Lawrence Otieno Olunga.
Shimanyula alisema kuwa alimsajili mchezaji huyo chipukizi akiwa bado ni mwanafunzi wa kidato katika shule a upili ya Lugusi Secondary.
Baadaye kukaibuka ripoti kwamba Sharks nao wamemsajili straika huyo. Hapo kukazuka malumbano makali huku Shimanyula akimshtumu Rais wa FKF Nick Mwendwa kwa kutumia mamlaka yake kuihujumu Homeboyz kwa kuwa yeye ndiye mmiliki wa Sharks.
Sharks ilidai kuwa ilimsaini rasmi Juni 2019 mbele ya wazazi wake. Hata hivyo Shimanyula alijibu kwa kusema alikuwa akifadhili masomo ya mwanafunzi huyo kwa maagano kwamba atakuwa mchezaji wa Homeboyz.
Kesi hiyo iliwasilishwa mbele ya kamati nya nidhamu ya FKF  mpaka leo uamuzi haujawahi kutolewa.