Vita ya ubingwa Ligi Kuu Bara ngoma inogile msimu ujao

Kikosi cha timu ya Azam ya jijini Dar es Salam kikiwa kwenye mazoezi ya kujiandaa na ligi kuu Tanzania bara
Muktasari:
Jitihada zote hizo zinalenga kuziandaa timu hizo kwa ajili ya kuwania ubingwa wa ligi hiyo itakayoanza Septemba 20 mwaka huu.
TIMU zinazoshiriki Ligi Kuu Bara msimu ujao ziko katika harakati za kujiimarisha na wachezaji wa timu hizo wanakiona cha moto sasa kwa kukimbizwa ufukweni na kupewa mazoezi mazito viwanjani na kwenye gym ili wawe fiti.
Jitihada zote hizo zinalenga kuziandaa timu hizo kwa ajili ya kuwania ubingwa wa ligi hiyo itakayoanza Septemba 20 mwaka huu.
Jumla ya timu 14 zitashiriki ligi hiyo lakini ni dhahiri kuwa timu nne zinapewa nafasi kubwa zaidi ya kuutwaa ubingwa huo.
Timu zinazopewa nafasi kubwa ya kuchukua ubingwa huo ni pamoja na mabingwa watetezi, Azam FC, mabingwa wa mara 24 wa ligi hiyo Yanga, mabingwa wa mara 18 wa ligi hiyo Simba.
Pia, timu iliyoleta upinzani mkubwa msimu uliopita ya Mbeya City nayo inapewa nafasi ya kuweza kutwaa taji hilo.
Timu za Ndanda FC na Stendi United ambazo zimepanda daraja msimu huu zinaweza kutoa upinzani mkubwa lakini hazifikiriwi katika kutwaa ubingwa huo.
Pamoja na kutopewa nafasi hiyo ya kutwaa ubingwa lakini hakuna anayezibeza timu hizo hasa kutokana na changamoto waliyoitoa Mbeya City msimu uliopita.
Timu nyingine za Kagera Sugar, Mtibwa Sugar, Coastal Union, Polisi Morogoro, JKT Ruvu, Ruvu Shooting, Mgambo FC na Prison zinaonekana kuwa ni washiriki wa kudumu na lolote linaweza kutokea kwao.
Tuziangalie timu zinazopewa nafasi ya kutwaa ubingwa huo, je, umewahi kujiuliza mwonekano wa timu hizo katika msimu huo?
Yanga
Kikosi cha kwanza cha Yanga ambacho kwa sasa kinanolewa na Mbrazili Marcio Maximo, kinatarajiwa kuwa na mabadiliko kidogo. Yanga imewasajili Wabrazili wawili, Andrey Coutinho na Geilson Santos ‘Jaja’ ambao ni dhahiri watakuwa kikosi cha kwanza.
Kikosi hicho kitakuwa na kiraka, Mbuyu Twite ambaye atapandishwa kucheza nafasi ya kiungo mkabaji kuziba pengo la Frank Domayo aliyetimkia Azam na Juma Abdul akicheza kwenye nafasi ya beki wa kulia alikokuwa anacheza Twite.
Nafasi hiyo ya beki wa pembeni itawaniwa na Salum Telela.
Katika safu ya ushambuliaji kutakuwa na mabadiliko makubwa ambapo Coutinho na Jaja wanatarajia kuwaweka benchi Jerry Tegete na Simon Msuva.
Haruna Niyonzima ‘Fabrigas’ anaweza pia kuanzia benchi kutokana na umahiri wa Hassan Dilunga. Licha ya ubora wa makipa Juma Kaseja na Ally Mustapha ‘Bathez’ ni dhahiri kuwa, Deogratius Munishi ‘Dida’ ataendelea kuwa chaguo la kwanza la Maximo.
Mchezaji wa zamani wa Pan African, timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ na Yanga, Augustino Peter maarufu kama Peter Tino anasema : “Yanga wana kikosi kizuri kwa sasa ila wanatakiwa kuwa na morali ya juu kuweza kuwania ubingwa.”
Tino anadai kilichoiangusha timu hiyo msimu uliopita ni kujiamini kupita kiasi kitu ambacho inabidi wajiepushe nacho.
Kikosi cha Yanga kitakuwa hivi: ‘Dida’, Juma Abdul, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kelvin Yondani, Twite, Mrisho Ngassa, Hassan Dilunga, Jaja, Emmanuel Okwi na Coutinho.
Simba
Timu hiyo yenye maskani yake Mtaa wa Msimbazi Kariakoo jijini Dar es Salaam itaendelea kuwa na kocha wake, Zdravko Logarusic.
Kikosi cha Simba kitakuwa na mabadiliko makubwa hasa ikizingatiwa kilimaliza katika nafasi ya nne msimu uliopita.
Kocha Logarusic ataendelea kumtumia Ivo Mapunda kama chaguo lake la kwanza golini, Issa Rashid ‘Baba Ubaya’ na Nassoro Masoud ‘Cholo’ watalazimika kuanzia benchi kuwapisha Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ na Edward Charles ambaye yuko kwenye rada za Simba.
Eneo la kiungo linaweza kuwa na mabadiliko kidogo iwapo Pierre Kwizera anayewindwa na klabu hiyo kama atapatikana.
Mchezaji huyo anaweza kucheza kama kiungo mshambuliaji akichukua nafasi ya Amri Kiemba huku Jonas Mkude akipangwa kama kiungo mkabaji.
Endapo Logarusic atatumia mfumo wa kuchezesha mastraika wawili, Mkenya Paul Kiongera anaweza kupata nafasi ya kuanza pamoja na Mrundi Amissi Tambwe huku Ramadhani Singano ‘Messi’ na Haruna Chanongo wakitumika kama washambuliaji wa pembeni.
Kocha wa Simba, Zdravko Logarusic anasema, “Nataka wachezaji wanne hadi sita watakaosajiliwa wawe ni chaguo la kwanza kwenye kikosi changu ila hilo litategemea uwezo wao.”
Kikosi kitakuwa hivi: Ivo, Edward , Tshabalala, Joseph Owino, Donald Mosoti, Mkude, Chanongo, Kwizera, Tambwe, Kiongera na Singano.
Azam
Kikosi cha Mabingwa watetezi, Azam FC kinaweza kuwa na mabadiliko kidogo hususan katika safu ya ushambuliaji kutokana na kuongezeka kwa washambuliaji Leone Saint-Preux, Ismail Diarra na Didier Kavumbagu kikosini hapo. Kocha Omog ataendelea kumtumia Kipre Tchetche kama mshambuliaji anayetokea pembeni huku Kavumbagu akipewa nafasi ya kucheza kama straika wa kati nyuma ya John Bocco.
Katika lango lao, kipa kinda, Aishi Manula ataendelea kupata nafasi ya kukaa golini huku kiraka Shomari Kapombe aliyesajiliwa msimu huu akiwa na nafasi kubwa ya kucheza kama beki wa kulia kutokana na umahiri wake. Sehemu ya kiungo itaendelea kukamatwa na Kipre Bolou na Sure Boy kutokana na Domayo aliyesajiliwa na klabu hiyo kufanyiwa upasuaji hivi karibuni.
Mshambuliaji wa zamani wa Simba, Yanga na Taifa Stars, Zamoyoni Mogella anasema, “Azam walichukua ubingwa lakini kikosi chao hakikuwa cha ushindani mkubwa, wanatakiwa kuwa makini kwa sasa kwa kusajili wachezaji wenye uwezo wa juu na wanaoweza kuleta ushindani mkubwa kikosini mwao.”
Kikosi cha Azam msimu mpya kitakuwa hivi: Aishi Manula, Kapombe, Erasto Nyoni, Said Moradi, Aggrey Morris, Bolou, Bocco, Sure Boy, Leone Saint-Preux, Kavumbagu, Tchetche.
Mbeya City
Klabu hiyo bado inaendelea kupata huduma ya kocha wao, Juma Mwambusi.
Kikosi cha Mbeya City kinatarajiwa kuwa na mabadiliko kidogo msimu ujao kutokana na wachezaji wote muhimu waliokuwa na timu hiyo msimu uliopita kusalia kikosini hapo.
Kocha Mwambusi ataendelea kuwatumia Antony Matogolo na Steven Mazanda kama viungo wa kati na kiungo Peter Mwaliyanzi aliyesajiliwa msimu huu atalazimika kuanzia benchi kutokana na uzoefu mkubwa aliokuwa nao Mazanda.
Mabeki Hassan Mwasapili, Deo Julius na Yohane Morris wakitarajiwa kuendelea kuiongoza safu ya ulinzi ya timu hiyo.
Katika safu ya ushambuliaji Saady Kipanga atalazimika kuanzia benchi kumpa nafasi Temi Felix aliyesajiliwa kikosini hapo msimu huu.
Washambuliaji wengine Deus Kaseke, Mwagane Yeya na Paul Nonga wataendelea kutumika pamoja na Temi.
Kocha na mchambuzi wa soka nchini Joseph Kanakamfumu anasema : “Mbeya City haijabadilika sana kuanzia wachezaji mpaka kocha lakini itakabiliwa na upinzani mkubwa sana msimu ujao, timu nyingi zimeshaitambua na zitakuwa zinaikamia, hivyo wanatakiwa kutafuta wachezaji kadhaa wa kigeni kuongeza nguvu ili kuwa na mwonekano mpya.”
Kikosi chao kinatarajiwa kuwa hivi: David Burhan, Peter Antony, Mwasapili, Julius, Morris, Matogolo, Mwagane, Mazanda, Paul Nonga, Temi na Kaseke.