Vijimambo vya Fountain Gate

Muktasari:
- Timu hizo zimekuwa na mwendelezo wa matukio ya kusisimua nje ya uwanja. Itakumbukwa mwaka jana ilimsimamisha ofisa habari, Issa Liponda na baadaye ikamrejesha kuendelea na majukumu, katika tukio lililokuwa kama sinema.
MSIMU wa 2024/25 uko mbioni kumalizika, lakini ndani ya msimu huu kuna mambo flani yametokea katika kikosi cha Fountain Gate na Foutain Gate Pricess ambayo yafurahisha.
Timu hizo zimekuwa na mwendelezo wa matukio ya kusisimua nje ya uwanja. Itakumbukwa mwaka jana ilimsimamisha ofisa habari, Issa Liponda na baadaye ikamrejesha kuendelea na majukumu, katika tukio lililokuwa kama sinema.
Cheki matukio mengine ambayo Mwanaspoti inakusogezea yaliyoacha wadau na mashabiki wa soka wakifurahi, lakini kwa upande mwingine wakijiuliza kulikoni?
ISHU YA UJAUZITO
Septemba 18, mwaka jana, Fountain Gate Princess ilitangaza kuvunja mkataba na mchezaji wake Mkenya Peris Oside baada ya kudaiwa kupata ujauzito akiwa kikosini. Mambo hayo!
Taaarifa iliyotolewa na timu hiyo ilieleza kuwa imevunja mkataba ilioingia na mchezaji huyo wa miaka miwili baada ya makubaliano ya pande mbili. Lakini, baada ya malalamiko ya mchezaji huyo uongozi ulimsimamisha kazi mmoja wa viongozi, ingawa haikuelezwa kwanini.

KOCHA KUTIMULIWA
Desemba 29, mwaka jana, timu hiyo ilitangaza kuvunja benchi la ufundi la timu ya wanaume yaani Fountain Gate lililokuwa likiongozwa na Kocha Mohamed Muya baada ya kumalizika kwa mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Yanga, ambapo ilipoteza kwa mabao 5-0 katika Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam.
Lakini, wakati Muya akiondoka na kutua Mkenya Robert Matano, kuna ishu ya kocha huyo mpya kudaiwa kwamba wakati kikosi hicho kipo Mbeya na gari la timu hiyo likirudi nyuma, aliguswa na hivyo kuumia jambo lililomfanya kwa muda kuwa nje ya timu akijiuguza hadi aliporejea, kisha akasepa zake kwao kwenda kujiuguza. Hatima ya Matano haifahamiki hadi sasa iwapo atarudi au la!

ISHU YA NOBLE
Wiki kadhaa zilizopita uongozi wa Fountain Gate ulimsimamisha kipa John Noble kwa makosa yanayodaiwa kuwa ni ya uzembe kwenye mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Yanga - timu hiyo ikikubali kichapo cha mabao 4-0.
Noble alifungwa mabao mawili kati ya manne waliyofungwa na Yanga akicheza kwa dakika 45 za kipindi cha kwanza kabla ya benchi la ufundi kumtoa na kumwingiza kipa mwingine, Ibrahim Parapanda ambaye naye alifungwa mawili, lakini akiokoa hatari nyingi langoni. Katika mechi hiyo Fountain Gate ilifungwa na Yanga mabao 9-0 baada ya awali kufungwa 5-0 katika mechi ya mzunguko wa kwanza, Desemba 29, 2024.
Baada ya mchezo kumalizika, kocha wa timu hiyo, Matano alimlaumu Noble kwa 'kupeana' mabao akimaanisha kwamba kipa huyo ni kama alitoa zawadi kwa wapinzani wao. Hata hivyo, licha ya klabu huyo kumsimamisha na kisha kumtaka kufika mbele kamati ya maadili hakuna taarifa yoyote iliyotolewa, huku kukiwa na madai kwamba alishaondoka nchini. Noble ni raia wa Nigeria. Sakata la kipa huyo pia lilianza kuchunguzwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Manyara ambayo nayo haijaweka wazi uchunguzi wake ulipofikia.

PRINCESS KUTIMKA UWANJANI
Ukiachana na timu ya wanaume, ile ya wanawake, Fountain Gate Princess, Mei 17,2025, ilitimka uwanjani na haikurudi kumalizia kipindi cha pili ikiwa ugenini dhidi ya mabingwa wapya wa Ligi Kuu ya Wanawake, JKT Queens.
Mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam hadi kipindi cha kwanza kilipomalizika JKT Queens ilikuwa mbele kwa mabao 3-0 yaliyofungwa na Anastazia Katunzi, Jamila Rajabu na Stumai Abdalah.
Sababu za kutoendelea kwa mchezo huo ni kitendo cha Fountain Gate Princess kutorudi uwanjani kipindi cha pili, huku ikidaiwa timu hiyo haikuridhishwa na uamuzi wa waamuzi katika baadhi ya matukio.
Hata hivyo, baadaye Kamati ya Mpira wa Miguu wa Wanawake ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) iliitoza faini ya Sh2 milioni.