VIDEO: Mwisho wa Ruge Mutahaba, azikwa kwa heshima Bukoba
Muktasari:
Mawazili waliotarajiwa kuwepo kwenye mazishi ya Ruge Mutahaba ni pamoja na Hamis Kigwangala (Maliasili na Utalii), Dotto Biteko (Nishati), January Makamba(Mazingira), Angela Kairuki (Uwekezaji) na Juma Aweso (Naibu Waziri wa Maji).
Bukoba. Ibada ya mazishi ya aliyekuwa Mkurugenzi wa vipindi Clouds, Ruge Mutahaba imeongozwa na Katibu wa Parokia ya Itahwa, Anatory Kyatwa huku nyimbo za kihaya zikipamba tukio la mazishi.
Mazishi hayo yaliyofanyika katika kijiji cha Kiziru Kata ya Karabagaine Wilaya ya Bukoba na hakuna mahubiri yaliyotolewa na katibu huyo.
Baada ya kuongoza taratibu za kuweka mwili kwenye kaburi huku nyimbo zenye ujumbe wa neno la Mungu zikiendelea, umefuata utaratibu wa kuweka mashada ya maua.
Miongoni mwa walioweka mashada ya maua ni Wabunge akiwemo, Nape Nnauye na Wilfred Lwakatare pamoja na viongozi wengine wa Serikali.
Awali wakati wa tukio la kuaga mwili wake katika viwanja vya Gymkhana, Maaskofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Bukoba walimtaja Ruge kama kijana jasiri mzalendo na mfano wa kuigwa.
Askofu Desderius Rwoma ameitaka jamii kuenzi mambo mema aliyoacha huku msaidizi wake, Methodius Kilaini akisema vijana wengi wamepata mafanikio kutokana na udhubutu wake na ujasiri wa kusimamia anayoamini.