Utamu upo Kwa Mkapa

WAKATI Simba ikiwa imeshamalizana na Al Ahly ya Misri katika mechi iliyopigwa jana usiku, leo ni zamu ya Yanga itakayoshuka kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kuvaana na Mamelodi ya Sundowns ya Afrika Kusini, huku vita nzima ya mchezo huo unatarajiwa kuwa eneo la kiungo.

Yanga inavaana na Mamelodi katika mechi ya mkono wa kwanza ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa ikiwa ni saa 24 baada ya Simba kumalizana na watetezi Al Ahly, huku ikiwa na kumbukumbu ya kuwahi kupewa kipigo cha jumla ya mabao 6-5 na Wasauzi walipokutana katika michuano hiyo mwaka 2001.

Yanga yenye rekodi tamu kwa mechi za nyumbani kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa na hasa ikicheza usiku ikishinda mara tano, itavaana na Mamelodi iliyozoea kucheza mechi zake mara nyingi mchana, lakini zote zikiwa zinaundwa na kutegemea mashambulizi na mabao kupitia viungo.

Vikosi vyote vimeonekana kusheheni mafundi katika eneo hilo na kuna uwezekano mkubwa mechi hiyo ikaamuliwa na mastaa wanaocheza eneo la kiungo zaidi kwa timu zote mbili kwani ndilo eneo hatari zaidi kwa kila upande.

Kutokana na soka la kisasa, mawinga nao wanaingia kwenye mfumo na kuwa viungo ambapo kwa Yanga hadi sasa ina viungo zaidi ya 10, ambapo wale wanaopata nafasi ya kucheza mechi hutengeneza muunganiko bora na kuifanya timu kuwa katika ubora wa hali ya juu.

Hali hiyo pia ipo kwa Mamelodi ambayo ina viungo zaidi ya 12 wenye ubora wa juu na kutokana na mifumo mbalimbali wachache wanaopata nafasi ya kucheza mechi mara kwa mara wamekuwa na hatari zaidi kwa mpinzani kuliko eneo lingine la timu hiyo na hapo ndipo unapojiuliza goma hili linaishaje kwa leo.


YANGA                 BALAA

Yanga mara nyingi imekuwa ikiwatumia viungo watano katika mechi na mshambuliaji kusalia mmoja ambapo Khalid Aucho, Mudathir Yahya, Maxi Nzengeli, Stephane Aziz Ki na Pacome wamekuwa wakianza mara kwa mara huku Salum Abubakari ‘Sure Boy’ na Agustine Okrah nao wakipata nafasi kwa muda mfupi.

Muunganiko wa mastaa hao kutoka mataifa tofauti ndani ya Yanga umekuwa hatari katika kutengeneza umbo la timu na kuanzisha mashambulizi, ikiwemo kuzalisha mabao jambo linalowafanya mashabiki wa Yanga kutembea vifua mbele kila timu yao inapotajwa wakiamini wanaweza kumfunga mpinzani yeyote.

Jambo hilo linaweza kuonekana leo mbele ya Mamelodi ambayo imekuwa tishio katika misimu ya karibuni ya michuano ya CAF.

Wachezaji wa Yanga eneo la kiungo katika Ligi Kuu Bara wameifungia timu hiyo zaidi ya mabao 35 ambapo Aziz amefunga 13, Nzengeli tisa, Mudathir manane na Pacome saba, hapo ni mbali na asisti walizotoa wakisaidiana wenyewe kwa wenyewe na kwa wachezaji wengine.

Hata katika michuano ya CAF msimu huu tangu mwanzo eneo hilo limekuwa likitoa mabao ambapo Pacome amefunga mabao matatu, Mudathir mawili na Aziz moja.

Pacome ndiye mchezaji anayeshika nafasi ya pili katika orodha ya wafungaji wa michuano hiyo hadi sasa akiasisti pia moja, akiwa nyuma ya Sankara Karamoko aliyekuwa akiichezea Asec Mimosas ya Ivory Coast ambaye hata hivyo aliuzwa Wolfsberger ya Austria katika dirisha la usajili la Januari.

Kwa namna hiyo, nyota huyo aliyekuwa na timu ya taifa ya Ivory Coast iliyokuwa Ufaransa kwa mechi mbili za kirafiki za kimataifa ni wazi ndiye aliyeshikilia mchezo huo kwa upande wa Yanga, iwapo atacheza kama alivyofanya katika mechi zote za makundi za timu hiyo akiwa ndiye kinara wa timu.

Kama Pacome hatakuwa kwenye fomu nzuri basi jukumu linawezwa kubebwa na Aziz KI kwani amekuwa akiamua mechi kubwa na ngumu, iwapo tu atakuwa na utulivu na kuishinda vita dhidi ya viungo na mabeki wa Mamelodi ambao huenda wamekuwa wakimfuatilia tangu droo ilipopangwa.


MAMELODI NAO

Kwa upande wa Mamelodi hali iko hivyo pia kwani mastaa wake wengi ni viungo na wamekuwa wakifunga zaidi kutokana na namna mfumo ulivyo.

Ukimtoa nahodha Themba Zwane ambaye hatakuwepo kwenye mechi hiyo kutokana na kadi tatu za njano kumekuwa na rundo la mastaa wanaocheza eneo la kiungo Mamelodi na kwa ubora mkubwa.

Thembinkosi Lorch, Teboho Mokoena, Marcello Allende, Rucas Ribeiro Costa, Gaston Sirino, Bongani Zungu,Grant Kekana, Thapelo Maseko, Junior Mandieta na Terrence Mashengo ni miongoni mwa viungo wanaopata nafasi mara kwa mara kwenye kikosi cha Masandawana.

Costa ndiye kinara wa ufungaji katika Ligi Kuu Afrika Kusini akiwa na mabao 10, lakini viungo wengine kama Sirino, Mashengo  na Allande nao wamekuwa wakifunga na kufanya vizuri kwenye eneo hilo.

Sambamba na hao pia mshambuliaji Peter Shalulile amekuwa akicheza kwa ushirikiano mkubwa na viungo hao kama ilivyo kwa Clemet Mzize au Kennedy Musonda wa Yanga.

Mamelodi inayonolewa na kocha Rhulani Mokwena inatumia mfumo wa 3-4-2-1 ikijaza viungo na kushambuliaji lango la adui kwa namba kubwa, wakiipata timu isiyocheza kwa nidhamu huzinyoosha, kitu ambacho Yanga ya Migueal Gamondi imeshaisoma mapema na leo itakuwa ni kazi moja tu.

Lakini pale inapocheza ugenini mara nyingi utumia mfumo wa 3-4-3 ikimbana adui mwanzo mwisho kuanzia eneo lake mwenyewe, kitu ambacho Yanga itaamua kutumia mfumo wa 4-4-2 au ile ya 4-3-3 ikitegemea kasi ya mawinga inaweza kuwaotea Mamelodi na kazi ikawa nyepesi kwa Mkapa.


WAAMUZI

Mechi hiyo inachezeshwa na Amin Mohamed Omar kutoka Misri atakayekuwa kati akisaidiwa na  Mahmoud Ahmed na Ahmed Hossam wote kutoka Misri, huku kwa upande wa marefa wasaidizi kwa kutumia video (VAR) kuna Mahmoud Ashor na  Mahmoud Elbana nao wanatokea Misri.

Timu zote zinapaswa kuwa makini katika kuepuka kufanya makosa kwani, waamuzi hao hawachelewi kuliamsha, huku kazi kubwa ikiwa kwa kiungo aliyerejea kutoka majeruhi, Khalid Aucho na mabeki  Ibrahim Bacca na Dickson Job anayeweza kuanzia pembeni kucheza nafasi ya Yao Kouassi aliyekwama kuiwahi mechi hiyo kwa majeraha aliyonayo licha ya juhudi zilizokuwa zinafanywa. Yao atacheza mechi ya marudiano kwa mujibu wa taarifa za kitabibu, kwani kuwahishwa sasa ni kuhatarisha afya yake.


WASIKIE WADAU

Winga wa zamani wa Yanga, Said Maulid ‘SMG’ anasema mechi hiyo itakuwa ngumu kwa pande zote mbili, lakini ameweka wazi kwamba Yanga inaweza kupata ushindi kama itakuwa na wachezaji wake wote na wakawa timamu kiafya.

“Pamoja na ukubwa wa Mamelodi, lakini Yanga kwa sasa ina kikosi imara. Wachezaji wake wana ubora mkubwa pia wana kiu ya kufika mbali, utakuwa ni mchezo mzuri kutazama hususani eneo la kiungo ambapo timu zote mbili zimesheheni mafundi na kwa upande wangu naona Yanga inaweza kushinda kama itakuwa na mastaa wake wote na watacheza kwa umoja kama ambavyo waekuwa wakifanya,” anasema SMG.

Kocha wa zamani wa Yanga, Charles Pawasa anasema viungo wa timu hiyo aliyowahi pia kuichezea miaka ya zamani wengi wao wana uchu na kupata mafanikio, na pia kila mmoja anapambania nafasi hivyo hiyo ni chachu ya kufanya vizuri mbele ya Mamelodi.

“Ukiangalia eneo la kiungo la Yanga lina wachezaji wengi ambao kila mmoja ananjaa ya kufanya vizuri ili aendelee kuaminiwa, hiyo itaisaidia timu kwani kila mmoja atataka kuonyesha ubora wake dhidi ya wachezaji wakubwa kama wale wa Mamelodi na hapo mechi itakuwa na ushindani mkubwa na atakayeshinda vita hiyo basi anaweza kushinda mechi,” anasema Mkwasa.

Kocha wa Dodoma Jiji, Francis Baraza anasema Yanga inawachezaji wengi bora ambao wanaweza kuidhibiti Mamelodi na kupata ushindi nyumbani huku akiwataka wasiogope.

“Mpira unachezwa uwanjani, ukiiangalia Yanga ya sasa inawachezaji wazuri na wanaweza kufanya kile wanachokifanya kwa kila timu. Wanatakiwa kujiamini na kwenda kupambana wakiwa kifua mbele kwani hakuna timu isiyofungika na uwezo wa kuwafunga Mamelodi wanao,” alisema Baraza. Baada ya mechi leo usiku, Yanga itasafiri hadi Afrika Kusini ambapo mechi ya marudiano itapigwa Ijumaa ijayo ya Aprili 5 kwenye Uwanja wa Loftus Versfeld uliopo mjini Pretoria yalipo maskani ya Mamelodi Sundowns na mshindi wa jumla atatinga nusu fainali. Endelea kutufuatilia kupitia mitandao yetu ya kijamii kupata uhondo zaidi. Maoni: 0658-376 417.