JICHO LA MWEWE: Namna Benchikha alivyorusha taulo lake asubuhi tu

Muktasari:

  • Alikuwa anataka kuondoka kabla ya mechi kumalizika. Mioyoni mwa viongozi walikubali ombi lake kwa sababu pia lilihusisha na afya ya mkewe. Hata hivyo, walimwomba amalizie mechi za ligi zilizobaki kabla ya kwenda Uwanja wa Ndege na kurudi zake Afrika Kaskazini.

NILIPENYEZEWA wiki iliyopita Abdelhak Benchikha alikuwa amemtumia meseji ya simu ya mkononi bosi mmoja mkubwa wa Simba akimwambia anataka kuondoka klabuni hapo muda wowote kuanzia sasa.

Alikuwa anataka kuondoka kabla ya mechi kumalizika. Mioyoni mwa viongozi walikubali ombi lake kwa sababu pia lilihusisha na afya ya mkewe. Hata hivyo, walimwomba amalizie mechi za ligi zilizobaki kabla ya kwenda Uwanja wa Ndege na kurudi zake Afrika Kaskazini.

Ombi la kwanza lilitokana na ukweli mwenyewe alidai kilichomleta kilikuwa ni Ligi ya Mabingwa Afrika. Kumbe alikuwa na kitu moyoni. Alitaka kuongeza wasifu wake kama kocha kwa kuipeleka Simba mbali katika michuano hii.

Pengine mbali zaidi ya nusu fainali. Mbali zaidi ya fainali kwa kuchukua ubingwa wenyewe. Ubingwa ambao Simba hawajachukua wala yeye mwenyewe hajawahi kuchukua. Hata hivyo, ndani ya miezi sita ya kwanza tu ameshindwa kuchukua, lakini hajaona dalili kama ndoto yake inaweza kufanikiwa.

Ni wazi ndoto za Benchikha na Simba zimeshindwa kuoana. Alikotoka alikuwa na wasifu mzuri tu. msimu uliopita tu, amechukua Kombe la Shirikisho akiwa na USM Alger. Lakini amewahi kuchukua ubingwa wa Super Cup mwaka huo huo tena kwa kuifunga Bingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Al Ahly. Kumbuka kabla ya hapo aliwahi kuchukua na RS Berkane ya Morocco.

Kuna tabia ya ufundi wa makocha na ubora wa wachezaji kusaidiana. Roy Keane aliwahi kumwambia Sir Alex Ferguson katika ugomvi wao maarufu kocha huyo asingebeba taji lolote bila ya wachezaji kama yeye kuwa katika ubora wao.

Ni suala la Yai na Kuku. Kipi kilianza. Jose Mourinho pamoja na ubora wake, lakini alikuwa mtumizi mzuri wa pesa kupata wachezaji anaowataka. Pep Guardiola anakumbukwa kwa soka safi, lakini anakumbukwa kwa kubebwa na Lionel Messi pale Barcelona pamoja na kina Xavi Hernandez na Andres Iniesta.

Amefika Manchester City amefungua pochi kubwa kuwaleta mastaa ambao wanamfanyia kazi. Pamoja na uhodari wake, unadhani Pep anaweza kutwaa taji la Ligi Kuu England akiwa na Brentford? Ni kitu ambacho hakifikiriki.

Arsenal waliwahi kumtaka Mikel Arteta mara mbili. Mara ya kwanza aliwaambia alihitaji bajeti kubwa kukifumua kikosi kizima. Hawakuafikiana naye. Wakaenda kwa Unai Emery ambaye baadaye alichemsha. Wakarudi tena kwa Arteta na kumkubalia sharti lake la kumpa kitita kikubwa cha pesa. Leo Arteta anaingia katika kundi la makocha ambao wametumia kiasi kikubwa cha pesa ndani ya muda mchache.

Benchikha anajua ubora unaotakiwa katika kikosi ambacho kinaweza kumpa mataji. Nadhani hajaona ubora huo. Januari ndio kwanza aliletewa Pa Jobe na Freddy Michael. Ni washambuliaji ambao wanaweza kumpa Ligi ya Mabingwa wa Afrika? Sidhani. Hata mashabiki wa kawaida wa Simba wanafahamu hilo.

Naambiwa viongozi pia waliafiki Benchikha aende kwa sababu hata kuna baadhi ya madai yake yalikuwa magumu kufikiwa. Wachezaji ambao alianza kuwatajia anawataka bei zao zilianzia Dola 300,000 na kuendelea.

Kwa Algeria au Tunisia hiyo ni pesa ya kununulia chapati, lakini kwa huku kwetu ni pesa nyingi. Unaweza kuwaelewa mabosi wa Simba. Kufikia hapo ndoto zao zikawa zimeenda tofauti. Benchikha amefahamu itakuwa ngumu kupata wachezaji wa kutimiza ndoto zake, lakini hapo hapo hawa waliopo hawatoshi kumpeleka anakotaka kwenda.

Zaidi ya hayo, unajiuliza kama Benchikha alikuwa karibu na tajiri wa timu Mohamed Dewji. Mara nyingi makocha wakubwa huwa wanakuwa karibu na matajiri wa timu kwa ajili ya kujua mipango mikubwa ya timu katika siku za usoni.

Wenzetu huwa wanaita ‘project’. Tajiri na kocha wanaunganisha mawazo yao kutaka kujua namna gani unaweza kuifanya timu tishio katika siku za usoni. Hii ni bima kubwa kwa kocha. Sidhani kama Benchikha alipata kujua mawazo ya tajiri.

Kilichonishangaza kuhusu Benchikha ni namna ‘hana njaa’ sana na pesa.

Mara nyingi makocha huwa hawaombi kuondoka kwa sababu kuomba kuondoka ni mtego. Kocha akiomba kuondoka mwenyewe huwa halipwi. Kocha akifukuzwa huwa analipwa pesa.

Nadhani Benchikha ameona ni bora aondoke zake mwenyewe bila ya kusubiri kufukuzwa kwa sababu inawezekana mkataba alioingia na Simba ni mfupi na angeweza kuondoka bure mwishoni mwa mkataba huo bila ya kupata pesa yoyote huku pia heshima yake ikiwa imetetereka vya kutosha. Mkataba wake ni wa mwaka mmoja na nusu, hivyo ilitegemewa aondoke mwishoni mwa msimu ujao.

Nadhani amegundua asingeweza kubadili chochote kuanzia sasa hadi wakati huo. Muda ungekuwa mchache kuipeleka Simba mbali zaidi kwa aina ya wachezaji alionao, pia kwa aina ya bajeti ambayo Simba wanayo kwa sasa.

Nini kinafuata? Kuondoka kwake kunaipa Simba nafasi ya kuanza upya. Naambiwa Simba wamepania kuachana na kundi kubwa la wachezaji ambao wanaamini hawana msaada kwa sasa katika kikosi chao.

Wapo kina Clatous Chama, Saido Ntibazonkiza, Henock Inonga na wengineo.

Ina maana mwanzo wa msimu mpya ujao Simba itakuwa na kocha mpya, pia kundi kubwa la wachezaji wapya.

Unaweza ukawa mwanzo mzuri kwa Simba ingawa kama tunavyoelewa wakati mwingine inakuwa ngumu kuunganisha timu kwa urahisi kama kila mtu anajikuta ni mpya kikosini.

Hata hivyo, hilo ni jambo ambalo mashabiki wa Simba wanatamani kuliona. Ili mradi tu wasajiliwe wachezaji wenye viwango hasa vya kuchezea Simba.

Wasiwe kama hawa ambao wamesajiliwa katika madirisha machache yaliyopita. Wengi hawana hadhi ya kuchezea Simba.