Usajili wachezaji kimataifa wafunguliwa leo

Monday July 19 2021
usajiliii pic
By Ramadhan Elias

BAADA ya jana kumalizika kwa Ligi Kuu Tanzania Bara na Simba kuibuka Bingwa wa ligi hiyo kwa mara ya nne, leo rasmi limefunguliwa dirisha la usajili wa wachezaji wa kimataifa.

Taarifa iliyotolewa na Ofisa Habari na Mawasiliano wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Cliford Mario Ndimbo imeeleza kuwa dirisha hilo la usajili na uhamisho wa kimataifa kwa klabu za Ligi Kuu (VPL), Daraja la Kwanza (FDL), Daraja la Pili (SDL) na Ligi Kuu ya Wanawake (SWPL) msimu 2021/2022 limefunguliwa leo Julai 19, 2021 na litafungwa Agosti 31,2021.

TFF imezitaka klabu kufanya usajili na kukamilisha uhamisho wa kimataifa katika kipindi hicho kilichopangwa na kama kuna changamoto yeyote inayohitaji utatuzi, klabu iwasiliane na Idara ya Mashindano ya TFF mapema.

Sambamba na hilo TFF imesisitiza kuwa hakutakuwa na muda wa ziada baada ya kufungwa kwa dirisha hilo la usajili.

Tayari baadhi ya timu ikiwemo Azam na Yanga zimeanza na usajili wa baadhi ya wachezaji wa kigeni tayari kwa msimu ujao.

Advertisement